Monday, October 24, 2011

MKUU WA MKOA WA RUKWA ACHANGISHA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 3.9 KUFANIKISHA TAMASHA LA UTAMADUNI WA MWANARUKWA LITAKALOFANYIKA TAREHE 25-27 NOVEMBA 2011

Tangu mwaka 1994 Baraza la Makumusho la Taifa limekuwa likifanya matamasha mbalimbali ya kuhusisha makabila tofauti ya Kitanzania.

Matamasha hayo huwa na lengo la kuonyesha Utamaduni wa kimila na desturi za jamii fulani kwa kuhusisha maendeleo na mafundisho yake.

Mambo hayo ya kimila ni pamoja na Lugha, chakula, utamaduni, mavazi, sanaa, zana za kimila, na mambo mengine ya kijamii.

Mwaka huu kwa mara ya kwanza kabisa Jamii za wanarukwa zimepata fursa ya kuonyesha tamaduni zao kuanzia tarehe 25-27 Novemba 2011 katika viwanja vya makumbusho vilivyopo Kijitonyama Jijini Dar es Salaam. (Pichani Mbunge wa Jimbo la Kwela Ndugu Ignas Malocha akitoa mchango wake kwa Mkuu wa Mkoa Rukwa)

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alilazimika kuendesha harambee ya kuchangishana ili kuweza kuharakisha maandalizi ya Tamasha hilo, Mwenyewe binafsi alianza kwa kutoa mchango wa Millioni moja na wadau wengine kuendelea kuchangia akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda aliyechangia kwa kujipiga faini baada ya kuchelewa kwenye kikao hicho ambapo aliahidi shilingi Milioni Mbili.

 Fedha alizoahidi Waziri Mkuu sio katika zile alizochangisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa bali ni sehemu ya mchango wake katika kufanikisha tamasha hilo.

Maandalizi ya Tamasha hilo bado yanaendelea na michango bado inaendelea kutolewa, kwa yeyote mwenye uwezo na nia anaombwa kuchangia kuweza kufanikisha Tamasha hilo muhimu.


Msanii Mkongwe Nchini Komandoo Hamza Kalala akionyesha mchango wake kwa wanajamii ya wanarukwa, Kulia nia Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi kwa upande wa Dar es Salaam Mama Mwangaza na Katibu wake  Ndugu Santo.

Baadhi ya wadau waliohudhuria kwenye kikao hicho cha maandalizi

Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliyemaliza muda wake Bw. Daniel Ole Njoolay na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliyekabidhi kijiti kwa Injinia Manyanya (Daniel Ole Njoolay) akisalimiana na jamii ya wanarukwa wanaoishi Jijini Dar es Salaam

Waandishi wa habari nao hawakuwa nyuma kuandika na kuuliza maswali mbalimbali kuhusu Tamasha hilo, hapo wakimuhoji Mkuu wa Mkoa wa Rukwa

1 comment:

  1. Naanza sasa kuingiwa na matumaini makubwa sana kwenye mwelekeo mzima wa wanarukwa kwenye ulimwengu wa utandawazi. Fursa hii imechelewa kutufikia kwa kweli. Tumekuwa na historia nyingi japo zimekuwa zikivalishwa gamba la kutisha mfano Uchawi,mazingaombwe,uganga wa jadi nk. Sasa naingiwa na furaha kwani maana halisi ya tafsiri hizo haikuwa kama unavyotakiwa kuwa. Huo ni utamaduni wetu na ndio asili yetu wana rukwa.Makabila mengine yamekuwa yakijitokeza tangu zamani sana na sasa wamekuwa mbali sana na sanaa zao zimekuwa kwenye makumbusho na kununuliwa kwa thamani kubwa sana. Nakuombea mafanikio mema mkuu wa mkoa na wana rukwa kwa ujumla

    Ahsante sana.

    George Nkwera - UK

    ReplyDelete