Wednesday, November 30, 2011

HAYA NDIYO YATOKANAYO NA TAMASHA LA UTAMADUNI WA MTANZANIA KWA JAMII ZA WANARUKWA NA KATAVI

Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda (MB) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) wakati wa Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania lililowasilishwa na Jamii za wanaRukwa na Katavi katika Kijiji cha Makumbusho Jijini Dar es Salaam.

Lilikuwa ni tamasha la aina yake lililodumu kwa muda wa siku tatu mfululizo kuanzia tarehe 25-27 Novemba 2011 katika Kijiji cha Makumbusho Kijitonyama Jijini Dar es Salaam. Tamasha la aina hii huandaliwa kila mwaka kwa ushirikiano wa Makumbusho ya Taifa na Jamii husika. Mwaka huu ilikuwa ni zamu ya jamii za wanaRukwa na Katavi.
Katika Tamasha hili la aina yake lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakuu Serikalini na wageni kutoka nje ya nchi tofauti na inavyokuwaga katika miaka mingine iliyopita. Katika maonesho hayo jamii za wanaRukwa na Katavi zilipata fursa pana ya kuonyesha tamaduni zao zikiwepo mila za jadi, vyakula vya asili, zana mbalimbali, ngoma, nyimbo, tiba asilia, na mambo mengine mbalimbali.
Akizungumza wakati wa kufunga Tamasha hilo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (MB) ambaye pia ni mwanaRukwa alisema kuwa, miogoni mwa mambo tuliyojifunza katika Tamasha hilo na ambayo tunatakiwa tuondoke nayokwenda kuyafanyia kazi ni pamoja na:-
ü  Umuhimu wa kuenzi na kuendeleza mila zetu.
ü  Umuhimu wa kuhifadhi mila na desturi zetu vizuri.
ü  Kutenga maeneo maalum kwa ajili ya kuhifadhi tamaduni, mila na desturi zetu (Makumbusho).
ü  Kuwa na siku maalum ya utamaduni wa mwanaRukwa na Katavi kwa ajili ya kudumisha tamaduni zetu .
ü  Umuhimu wa kuhusisha masuala ya Utamaduni na Utalii.
ü  Kuwepo na Kamati maalum itakayosaidia na kusimamia yaliyojifunzwa wakati wa Tamasha hilo.
Aidha katika hotuba yake ya kufunga Waziri Mkuu alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) kuwa mstari wa mbele kusimamia hayo mambo katika utekelezaji wake. Kwa upande wa wanaRukwa waishio Dar es Salaam  aliwomba na kuwapa jukumu la kuanzisha umoja wa wanaRukwa na Katavi (UMARUKA) kwa ajili ya kuimarisha umoja na mshikamano amabao umekuwa ukilegalega.

KATIBU TAWALA MKOA WA RUKWA NA MKUU WA WILAYA YA MPANDA KWA PAMOJA WALIWASILISHA TAARIFA YA FURSA ZA UWEKEZAJI ZINAZOPATIKANA MKOANI RUKWA WAKATI WA KILELE CHA TAMASHA HILO.

Fursa za uwekezaji katika Mkoa wa Rukwa zilinadiwa wakati wote wa Tamasha hilo. Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima (kulia) na Dkt. Rajab Rutengwe wakifanya kazi hiyo wakati wa kilele cha Tamasha hilo.

Ze Orijino Komedi walikuwepo kutoa burudani motomoto.

Ubunifu ni Nguzo ya Tamaduni zetu. Hizo ni baadhi ya ngoma zilizokuwa zinatumika kuburudisha wakati wa tamasha hilo. 

No comments:

Post a Comment