Wednesday, November 9, 2011

KILELE CHA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA UHURU MKOA WA RUKWA KUFANYIKA WILAYANI NKASIKilele cha sherehe za Miaka 50 ya Uhuru kitaifa yatafanyika kuanzia tarehe 1-9 Desemba katika viwanja vya Mwalim Julius Kambarage Nyerere Kilwa Road Dar es Salaam. Katika kilele hicho Mgeni rasmi atakuwa Mh. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kimkoa Kilele cha sherehe hizo zitafanyika katika Wilaya ya Nkasi na Mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella M Manyanya (MB).

Uamuzi wa kuteua wilaya ya Nkasi iwe mwenyeji wa sherehe hizo ulifikiwa na kupewa baraka na kikao cha Kamati Kuu ya Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru Mkoa wa Rukwa ambayo Menyekiti wake alikuwa Kaimu Mkuu wa Mkoa Mhe. Joyce Mgana (Pichani) ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi. 

Kamati hiyo ya sherehe ililazimika kukaa na kufikia makubaliano hayo baada ya kupata barua kutoa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iliyoagiza Mikoa kuteua wawakilishi watakaoshiriki kwenye kilele cha Sherehe hizo kitaifa jijini Dar es Salaam.

Aidha barua hiyo ilitahadharisha uteuzi huo usiathiri maadhimisho ya kilele cha sherehe hizo kwenye ngazi ya Mkoa ambapo Mkuu wa Mkoa ndio atakuwa mgeni rsmi kama ilivyoelekezwa kwenye muongozo wa kitaifa.

Miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao hicho ni pamoja na hilo la Wilaya ya Nkasi kuwa mwenyeji wa sherehe za Miaka 50 ya Uhuru kimkoa, Kamati kumteua Ndugu Salum Shilingi ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ndogo ya wataalam ya Mkoa ya Miaka 50 ya Uhuru kuungana na wawakilishi kutoka Mikoa mingine katika kutoa taarifa kwa Katibu Mkuu TAMISEMI namna Mikoa ilivyojipanga kushiriki kwenye sherehe zitakazofanyika kwenye Viwanja vya Mwl. J.K. Nyerere- Barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam tarehe 11/11/2011.

Miongoni mwa taarifa atakazoenda kuziwakilisha mwakilishi huyo kwenye kikao cha kamati hiyo ndogo ya Katibu Mkuu ni aina na idadi ya uwakilishi kwenye maonesho hayo kutoka Rukwa ambayo jumla yake ni washiriki 61 ambao ndani yake wamo Viongozi wa Chama na Serikali,  Wazee kumi waliozaliwa tarehe 9 Desemba 1961, Wajasiriamali wawili na wataalam kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa na Halmashauri zake.

Taarifa nyingine atakazoenda kuziwakilisha ni maeneo ambayo Mkoa au Halmashauri za Mkoa zimepanga kuonyesha ambayo ni Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Utawala Bora, Uwekezaji, Utalii, Huduma za Jamiii, Uchumi, Mipango Miji na Hifadhi ya Mazingira.

Jambo lingine la mwisho atakaloenda kuliwakilisha mwakilishi huyo ni makisio ya bajeti ambayo Mkoa umepanga kutumia katika ushiriki huo, Mpaka tunaruka hewani bajeti hiyo bado ilikuwa ikiandaliwa. 

1 comment:

 1. Nakushukuru sana kwa kutuhabarisha habari hizi muhimu sana kwa maendeleo yetu wana rukwa. Binafsi naona kumekuwa na jitihada nzuri sana upande wa serikali na taasisi zake katika kusukuma maendeleo ya rukwa tatizo naliona ni upande wa mwananchi mmojammoja. Watu bado tunaendeleo kugubikwa na blanketi la kihistoria kuwa rukwa ni mkoa usio na maendeleo. Mengi yamefanyika na mazuri sana. jitihada zielekezwe kwenye uhamasishaji wa watu kuongeza bidii katika kufanya kazi za maendeleo na kujitolea.
  Uamuzi wa kupeleka sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru kimkoa wilayani Nkasi naupongeza sana kwani hii itakuwa fursa kwa wana nkasi kujivunia na kujikumbusha tulikotoka wapi tupo na wapi tunataka Nkasi,Rukwa na Tanzania kwa ujumla tunataka tuwe miaka 50 ijayo. Mkuu wa Wilaya mama Mgana jitihada zake wote tunazijua katika kuhimiza maendeleo ya wilaya na mkoa kwa ujumla.
  Ahsante sana na endelea kutuhabarisha hususan sisi ambao tuko nje ya nchi kwa sasa.

  George Nkwera
  Sumbawanga - Kwa sasa UK

  ReplyDelete