Saturday, December 24, 2011

MKUU WA MKOA WA RUKWA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA KATIKA HOSPITALI KUU YA MKOA HUO, ABAINI MAPUNGUFU MBALIMBALI NA KUYATOLEA MAAGIZO

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali Kuu ya Mkoa huo kufuatia malalamiko yaliyokuwa yamejitokeza kuhusu huduma mbovu inayotokana na upungufu wa vifaa katika Wodi ya wazazi.

Kufuatia malalamiko hayo Mkuu huyo wa Mkoa akiambatana na Kamati kuu ya Chama Tawala katika Mkoa huo waliamua kufanya ziara ya kushtukiza  kujionea hali halisi ya huduma katika hospitali hiyo.


Katika ziara yake hiyo alibaini mapungufu mbalimbali yakiwemo upungufu wa vyandarua kwenye baadhi ya vyumba katika wozi za wazazi ambapo aliagiza kamati ya Hospitali hiyo kuondoa mapungufu hayo katika kipindi cha wiki moja ijayo, kinyume na hivyo wajiandae kuwajibika.


Uhaba wa gloves kwa ajili ya kusaidia kinamama wajawazito pia ni tatizo kubwa katika hospitali hiyo ya Mkoa. Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt. Marwa alisema MSD ndio wanaohusika na usambazaji wa gloves hizo na kwamba kuna tatizo katika uzalishaji na usambazi unaopelekea uhaba mkubwa wa vifaa hivyo, alisema gloves zilizopo ni kwa ajili ya dharura tu.


Hali hiyo inapelekea kina mama wajawazito kulazimika kwenda hospitalini hapo na gloves zao wenyewe. Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya alitolea tamko suala hilo na kusema ni bora MSD wawe wazi kama wameshindwa kugawa gloves hizo ili Mkoa utafute njia mbadala ya kuweza kupata vifaa hivyo badala ya kuwategemea wao.


Mapungufu mengine ni idadi ndogo ya madaktari na manesi katika hospitali hiyo, Mkuu wa Mkoa alisema kutokana hospitali hiyo kuwa na vibali vya ajira 47 na manispaa vibali 20, yeye pamoja na kamati husika kwenye hospitali hizo wataenda kuziona mamlaka husika ili vibali hivyo viweze kufanyiwa kazi haraka na watumishi hao waweze kupatikana.


Aliendelea kusema kuwa kwa wale watumishi wa hospitali 16 waliomba mkataba baada ya kustaafu kuna haja ya wao kupewa nafasi kama bado wanahitajika katika nafasi zao za kutoa huduma. Mkuu wa Mkoa alisema "hatuwezi kuitupa hi nguvu kazi tuliyonayo, itabidi tuendelee kuitumia kama bado inatusaidia huku tukiendelea kutafuta nguvu mpya".


Injinia Manyanya alitoa wito kwa wale wahitimu wa sekta ya afya wanaochaguliwa kuja kufanya kazi Rukwa kuwa wasiogope kuja kwani hakuna tatizo lolote na yote mabaya yanayosemwa kuhusu Rukwa hayana ukweli wowote. "Mimi nimekaa Rukwa nimeona maisha ya hapa ni mazuri hakuna tatizo lolote" alisema Injinia Manyanya. 


Kutokuwepo kwa mtaalam wa kuendesha mashine ya kutolea dawa na kumsaidia mzazi kupumua baada ya kutoka kwenye dawa ya usingizi ni pungufu jingine katika hospitali hiyo. Injinia Manyanya ameiomba Wizara husika kuleta mtaalam wa mashine hiyo au kumpeleka mtumishi mmojawapo kutoka katika hospitali hiyo kwenye mafunzo ya jinsi ya kuendesha mashine hiyo.


Mapungufu mengine yaliyobainika ni kwenye vitanda vya kuhifadhia watoto wachanga (Incubators) kuwa havifanyi kazi vizuri. Alimuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga kutoa mashine moja (Incubator) kwa hospitali ya Mkoa katika tatu walizopewa na Kampuni ya uwekezaji ya TPM Mining kutoka Uturuki iliyowekeza kwenye uyeyushaji na ununuzi wa madini ya shaba Wilayani Mpanda. 


Kwenye upande kuna mapungufu kuwa baadhi ya manesi hawajalipwa posho zao za muda wa ziada na hivyo Mkuu wa Mkoa kuagiza malipo hayo yafanyike mara moja kutokana na fedha za malipo hayo kuwa zilishatumwa katika Mfuko wa hospitali kuwezesha malipo hayo. 


Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa alitoa muda wa siku tisa (9) kwa kamati ya hospitali kuhakikisha kuwa mapungufu aliyoyatolea maagizo yawe yamekwisha fanyiwa kazi. Alisema "nitakuja tena kukagua baada ya siku tisa nikikiuta hali bado ipo hivi nikute mmeshaandika barua ya kujiuzuli maana kazi itakuwa imewashinda"

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) akisalimiana watumishi wa Hospitali kuu ya Mkoa wa Rukwa mara baada ya kuwasili hospitalini hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akisaini Kitabu cha wageni kwenye Ofisi ya Mganga Mkuu wa hospitali hiyo.

Mhe. Eng. Manyanya akiwaeleza watumishi na viongozi wa Hospitali kuu ya Mkoa wa Rukwa lengo la ziara yake ya kushtukiza kuwa na taarifa kuwa huduma katika wodi ya wazazi ni ya kusikitisha.

Wajumbe wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa wa Rukwa wakati akitoa maelekezo mbalimbali.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akihutubia watumishi wa hospitali kuu ya Mkoa wa Rukwa katika ofisi ya Mganga Mkuu wa hospitali hiyo.
Hapo akizungumza na baadhi ya ndugu za wagonjwa walikua hospitalini hapo kutembelea ndugu zao, aliwaasa ndugu hao kuonyesha upendo wa dhati kwa ndugu zao hasa katika kipindi hiki ambacho wanakabiliwa na maradhi.


Msafara ukielekea kwenye wodi ya wazazi hospitalini hapo


Kaimu Mganga Mkuu Hospitali Kuu ya Mkoa Rukwa Dkt. Marwa akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya.
Kamati kuu ya Chama Tawala Mkoa wa Rukwa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya, Mbunge wa Sumbawanga Mjini CCM Mhe. Aeshi Hillal wa pili kushoto, Bi Maufi ambaye ni Katibu wa CCM Mkoa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Mhe. Sabas Katepa wakifuatilia mwenendo wa huduma ya afya katika katika Hospitali Kuu ya Mkoa Rukwa.  


Mtoto huyu anaitwa Rachel Richard, alizaliwa nyumbani katika maeneo ya Majimoto wilayani Mpanda akiwa na uvimbe unaopelekea mguu wake wa kulia kujikunja, anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa uvimbe na mguu ili aweze kuondokana na matatizo hayo. Kwa yeyote mwenye uwezo anaweza kuwasiliana na uongozi katika hospitali ya Mkoa na kutoa msaada wowote kufanikisha upasuaji huo. Mama wa mtoto huyo anaitwa Miriam Nassoro.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) akiwa amemshika mtoto aliyejulikana kwa jina moja la Stella mara tu baada ya kuzaliwa hospitani hapo.


Mashine ya kumsaidia mama mzazi kupumua baada ya kutoka kwenye dawa ya usingizi katika hospitali ya Mkoa Rukwa, Mashine hii haina mtaalam ya kuiendesha, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ameziomba mamlaka husika kuleta mtaalam wa kuendesha mashine hiyo au kumpeleka mafunzoni mtumishi katika hospitali hiyo aweze kuendesha mashine hiyo.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na msafara wake wakiwasalimia wazazi waliokuwa mapumziko baada ya kujifungua.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akitoa maagizo kwa Kamati ya Hospitali ya Mkoa wa Rukwa.

No comments:

Post a Comment