Saturday, December 17, 2011

MKUU WA MKOA WA RUKWA AIOMBA TANESCO ISIKATE UMEME KUFANIKISHA MAANDALIZI YA SENSA YA WATU NA MAKAZI MKOANI RUKWA

Mkuu wa Mkoa wa  Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya (MB) kulia na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) ameliomba shirika la Uzalishaji na Usambazaji Umeme nchini (TANESCO) kuhakikisha upatikanaji wa Umeme unakuwa wa uhakika Mkoani Rukwa katika kipindi hiki cha maandalizi ya Sensa ya watu na makazi itakayokamilika mwezi februari mwaka 2012.
Sensa ya Watu na Makazi inategemewa kufanyika mwakani (2012) ambapo zoezi hilo litafanyika nchi nzima. Lengo kuu la Sensa ni kuweza kutambua idadi ya watu pamoja na kuainisha mahitaji yao muhimu yakiwemo huduma za jamii na kuweza kuyafanyia kazi kwa kuyaingiza katika mipango ya kitaifa na bajeti kwa ujumla.
Akizungumza na Timu ya sensa ya Mkoa wa Rukwa ambayo pia yeye ni mwenyekiti na ile ya sensa kutoka Tume ya Taifa ya Takwimu ofisini kwake akipokea taarifa na mkakati wa maandalizi ya zoezi hilo alisema kuwa ataiandikia barua TANESCO kuwafahamisha juu ya zoezi hilo na kuwaomba wajitahidi kuhakikisha kuwa umeme unakuwepo mkoani humo kwa kipindi chote hicho cha maandalizi kuhakikisha ufanisi cha zoezi hilo ambalo linakwenda na muda.
Mkuu huyo wa Mkoa aliendelea kusema kuwa ni lazima tufikie azma ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ya kuendelea kutambua makazi ya wananchi wote wa Tanzania kupitia Sensa ya mwaka 2012 ili nchi iweze kuwa na mipango endelevu.
Zoezi hilo la maandalizi linahusisha utengaji wa maeneo rasmi kwa ajili ya kuhesabia zikiwemo kaya pamoja na maeneo muhimu yenye huduma za kijamii. Kwa kuanzia Timu hiyo inayoongozwa na Bwana Mugambi kutoka Tume ya Taifa ya Takwimu imejipanga kuanza na maeneo magumu ambayo ni tarafa za Mtowisa na Kipeta zilizopo katika Wialaya ya Sumbawanga.
Kwa upande mwingine Mkuu huyo wa Mkoa aliitaka Timu hiyo ya Sensa kwenda mbali zaidi katika zoezi hilo kwa kutaka kujua ni sababu zipi zinazopelekea wananchi kutotumia vituo maalum vya biashara vilivyojengwa na Serikali kwa gharama kubwa na badala yake kuendelea kufanya biashara zao katika maeneo yasiyo rasmi (mitaani) na kwamba pengine wanaweza kuja na majibu yatakayoweza kuondoa tatizo hilo.
Kwa upande wake Katibu wa tume ya Sensa Mkoa wa Rukwa ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa huo Alhaj Salum Mohammed Chima amesema changamoto kubwa inayokabili Sekretarieti za Mikoa nchini ni ushirikishwaji hafifu katika upangaji wa bajeti za kitaifa hali inayopelekea Mikoa kupewa bajeti ndogo ukilinganisha na ile inayopelekwa wizarani.
Sensa ya mwisho iliyofanyika Agosti 2002 wakazi wa mkoa wa Rukwa walikuwa 1, 136, 354 na ambapo mpaka kufikia mwaka 2010 Mkoa huo unakiksiwa kuwa na wakazi 1, 503, 183 ambao ni ongezeko la asilimia 3.6% kwa mwaka.

No comments:

Post a Comment