Tuesday, December 20, 2011

MKUU WA MKOA WA RUKWA AWATAKA WAWEKEZAJI KUTOKA UTURUKI KUNUNUA MAKAA YA MAWE NA CHAKULA NCHINI BADALA YA KUAGIZA KUTOKA NJE

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya (MB) akitoa nasaha zake kwa viongozi wa kampuni ya TPM Mining ya Uturuki. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe. Dkt. Rajab Rutengwe. Nyuma ni makaa ya mawe yenye jumla ya tani 300 yaliyoagizwa na kampuni hiyo kutoka China kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) ameiomba Kampuni ya Uwekezaji ya Uturuki inayojishughulisha na uyeyushaji na ununuzi wa madini ya shaba wilayani Mpanda kununua makaa ya mawe na vyakula vinavyozalishwa nchini badala ya kuagiza kutoka nje kama wanavyofanya hivi sasa.
Akiwa ziarani wilayani Mpanda leo katika kujionea shughuli mbalimbali za Kampuni hiyo Mkuu huyo wa Mkoa alionyeshwa makaa ya mawe yatakayotumika na kampuni hiyo kwa ajili ya shughuli za kuendeshea mitambo ya uzalishaji yakiwa yameagizwa kutoka China na vyakula mbalimbali vikiwa vimeagizwa kutoka nchini Uturuki.
Mkuu huyo wa Mkoa aliwaeleza waturuki hao kuona ni jinsi gani wataweza kutumia makaa ya mawe ambayo huzalishwa nchini Tanzania kwa wingi tofauti na hivi sasa wanavyoagiza kutoka China.
Kuhusu vyakula alisema kuwa vipo vyakula vingi vinavyozalishwa hapa nchini kitu ambacho hakuna haja ya wao kuendeleza kuagiza vyakula kutoka nchini kwao na kwa kufanya hivyo kunatoa tafsiri mbaya kuwa hawaamini kile watanzania wanachokizalisha.
Aliendelea kusema kuwa wakinunua bidhaa za ndani watakuwa wakiongeza ajira nchini na kuongezea matumizi ya rasilimali za taifa kwa kufaidika wao wenyewe na taifa kwa ujumla. Kuhusu wafanyakazi aliiasa Kampuni hiyo kuhakikisha kuwa inawalipa vizuri wafanyakazi wake kwa wakati kuepusha uonevu na migogoro isiyokuwa ya lazima.
Katika nasaha zake kwa Kampuni hiyo aliishauri kuhakikisha kuwa shaba inayozalishwa nchini inaongezewa thamani hapahapa nchini kabla ya kusafirishwa ili kuiletea Serikali mapato yanayokidhi na kuondokana na utaratibu wa kizamani wa kusafirisha nje ikiwa ghafi. Aidha alisisitizia ushirikiano kwa kampuni hiyo na Serikali pamoja na wananchi wa Mpanda ili kuleta ufanisi katika kazi zao.
Kampuni ya TPM Mining kutoka Uturuki imekuwa ni Kampuni ya kwanza kutoka nje kuanza kuwekeza katika mji wa Mpanda kwenye sekta ya Madini baada ya jitihada kubwa za Serikali katika kunadi fursa za uwekezaji zinazopatikana Mkoani Rukwa.
Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa Uzalishaji kiwandani wa kampuni hiyo aliyefahamika kwa jina moja la Ndugu Mermet  amesema kuwa Kampuni hiyo imeingia nchinimwezi februari mwaka 2011 na kutokana na ushirikiano mkubwa walioupata kutoka kwa viongozi wa serikali wilayani Mpanda wamepiga hatua kubwa katika kujenga miundombinu ambapo katika kipindi cha miezi mitatu ijayo wataanza uzalishaji.
Aliendelea kusema kuwa Kampuni hiyo imeshatoa ajira za muda kwa watanzania wapatao 70 na kwamba idadi yao itaongezeka na kupewa ajira za kudumu pale uzalishaji utakapoanza rasmi. Kwa mujibu wa meneja hyo idadi ya wafanyakazi wageni ambao ni waturuki wapo 18 ambao kazi yao kubwa ni kuwapa mafunzo watanzania ambapo baadae wataondoka na kubaki watano au saba kwa ajili ya usimamizi na kuwaachia watanzania kazi za uzalishaji katika kampuni hiyo.
Kaimu meneja wa Kampuni hiyo aliongeza kwa kusema kuwa jumla ya misaada yote waliotoa kwa jamii ya Tanzania mpaka sasa ina thamani ya shilingi milioni 50 ikiwa ni vitanda 40 kwa ajili ya kuwasaidia watoto wachanga walivyovikabidhi kwa Mama Salma Kikwete na vingine walivitoa mkoani Rukwa na Kigoma. Thamani ya kila kitanda kimoja ni dola za kimarekani 2500 ambazo ni zaidi milioni 4 za kitanzania. Mchango mwingine ni pamoja na kisima chenye thamani ya shilingi milioni 13.

No comments:

Post a Comment