Sunday, December 25, 2011

MKUU WA MKOA WA RUKWA AZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake jana.

Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ofisini kwake. Kulia ni Mussa Mwangoka (Mwananchi-Rukwa), Sammy Kisika (Star TV na RFA-Rukwa), na Petty Siame (Daily News/ Habari Leo- Rukwa) Kushoto ni Kaimu Mkurugenza wa Manispaa ya Sumbawanaga, Bw. Maulid.

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya wakisikiliza swali kutoka kwa waandishi wa habari.

PRESS CONFERENCE
24/12/2011
Viongozi wote wa serikali,
Watumishi wote wa serikali,
Vyama vya siasa,
Taasisi za Dini, wazee wetu wa mkoa wa Rukwa,
Akina mama na vijana bila kuwasahau kwa namna ya pekee waandishi wetu wa Habari

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana wanajamii wa Mkoa wa Rukwa na Mkoa tarajiwa wa Katavi kwa jinsi ambavyo mmenipa ushirikiano wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania toka kuteuliwa kwangu kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
1.   Salam za Krismas na Mwaka Mpya

v Kesho tarehe 25/12/2011 ni Sikukuu ya Krismas ambapo Wakristu Duniani kote watasherehekea kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristu. Sikukuu hiyo inakuja sambamba na Sherehe za Mwaka mpya 2012.

v Napenda kuchukua fursa hii kuwatakia wakazi na wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa heri ya Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya wenye mafanikio (2012).

v Nawaomba wananchi wote pamoja na wageni wa Mkoa wa Rukwa kusherehekea msimu huu wa  Sikukuu kwa amani na utulivu kwa kujiepusha na vitendo vyote vya uvunjifu wa amani.

v Nawahakikishia wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama katika mkoa wetu vimejipanga vizuri katika kuhakikisha kunakuwepo na usalama wa Mali na Raia wakati wote huu wa Sikukuu.

v Aidha nitoe tahadhari kwa wale wote watakaohusika na vitendo vya uvunjifu wa amani kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria, na hivyo tunaomba ushirikiano kutoka kwa wananchi katika utoaji wa taarifa za matukio mbalimbali yanayoashiria uvunjifu wa amani.

v Natoa wito kwa madhehebu yote ya dini katika Mkoa wa Rukwa kuendeleza ushirikiano na Serikali katika kuleta maendeleo ya Mkoa wetu wa Rukwa.
2.   Hali ya Mvua zinazoendelea kunyesha Mkoani Rukwa

*     Nichukue fursa hii Kuungana na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwapa pole wananchi wote wa Jiji la Dar es Salaam waliopatwa na maafa au kuathirika kwa namna moja ama nyingine na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha kwa muda wa siku tatu mfululizo.

*     Kwa taarifa iliyotolewa tarehe 22-23/12/2012 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini Dkt. Agnes Kijazi inaonyesha kuwa maeneo ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi (Mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa) yanatarajiwa kuendelea kuwa na mvua katika kiwango cha juu ya wastani pamoja na vipindi vya mvua kubwa.

*     Hali ya mvua katika Mkoa wetu wa Rukwa inaendelea kunyesha kwa kiwango cha kuridhisha. Mpaka sasa hakuna taarifa zozote za maafa ya mvua hizo katika mkoa wetu.

*     Kufuatia agizo la hivi karibuni la Mheshimiwa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwataka wananchi wote wanaoishi katika maeneo hatarishi kwa mvua zinazoendelea kunyesha hasa mabondeni waondoke, Napenda kuwaagiza wale wote wanaoishi kwenye maeneo hayo katika Mkoa wetu waondoke mara moja ili kuepusha madhara yanayoweza kuletwa na mvua zinazoendelea kunyesha. Aidha Idara ya Ardhi ihakikishe inawapimia viwanja salama wale wote watakaobainika kuwa na ulazima wa kuhama katika maeneo hayo hatarishi.

3.   Hali ya Barabara

Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wetu baadhi ya maeneo korofi ya barabara ni mbaya hasa barabara ya Tunduma-Ikana, Majimoto-Inyonga, Mpanda-Inyonga, Mpanda-Karema na Mpanda-Kigoma, Hivyo basi nawaagiza Tanroads kuhakikisha maeneo hayo yanarekebishwa ili yaweze kupitika bila usumbufu wowote.

Aidha ni marufuku kwa magari ya mizigo kuzidisha uzito uliopangwa kisheria. Kwa ufahamu wangu uzito huo usizidi tani 30.
4.   Usafi wa Mazingira

·        Hali ya usafi wa mazingira katika miji yetu siyo ya kuridhisha sana. Napenda kutoa agizo kwa wananchi na wakazi wote wa mkoa wa Rukwa kushiriki katika usafi wa mazingira ili kuepukana na Magonjwa ya Mlipuko hususan Kipindupindu.

·        Usafi ni jukumu la kila mwananchi hivyo kila kaya ihakikishe inafanya usafi katika eneo lake kuweka mazingira safi na ya kuvutia kuweza kuuletea mkoa wetu sifa na heshima.

·        Viongozi wote wa serikali katika mkoa kuanzia ngazi ya wakuu wa wilaya hadi wenyeviti wa vijiji na mitaa wawe ni mfano katika usafi wa mazingira na wasimamie  zoezi la usafi wa mazingira kikamilifu katika maeneo yao.

·        Natoa agizo kwa Viongozi wa Manispaa ya Sumbawanga kuhakikisha barabara zote za lami katika Manispaa  zinakuwa safi kwa kufagia mara kwa mara mchanga ambao unatuama kwenye barabara hizo.

·        Wahakikishe pia miundombinu ya maji safi na maji taka katika Manispaa hususan mitaro ya maji taka inazibuliwa na kusafishwa mara kwa mara.

·        Natoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa kutumia fursa hii ya mvua zinazoendelea kunyesha kupanda miti kuhifadhi mazingira na vyanzo vya Maji. 

5.   Bei ya bidhaa:

Nimesikitishwa kuona bei ya petrol kufikia Tshs. 8,000/= na cement kufikia mfuko Tshs,22,000/= wakati inatoka hapa jirani Mkoa wa Mbeya. Hali ya mafuta naamini itaboreka hivi karibuni kwani tayari malori yapo njiani kuleta bidhaa hiyo. Kuhusu cement nawataka wafanya biashara washushe mara moja, bei ya cement isizidi elfu 18,000/=. Zaidi ya hapo TRA wafuatilie mahesabu yao na kuona kama kweli wanapata hasara.
Napenda kuwaambia wananchi wangu wa Mkoa wa Rukwa kuwa; nawapenda sana, na ombi langu kwao ni ushirikiano wa hali na mali katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya mkoa huu. Naahidi kutoa ushirikiano wangu wote kwao bila kubagua dini, rangi, kabila, maskini au matajiri.

Nashkuru kwa kunisikiliza.
 Eng. Stella Martin Manyanya
MKUU WA MKOA
RUKWA

No comments:

Post a Comment