Thursday, December 22, 2011

YALIYOJIRI KATIKA ZIARA YA MKUU WA MKOA WA RUKWA WILAYANI MPANDA HIVI KARIBUNI

Njiani kuelekea Mpanda Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya alikutana na wajasiriamali wadogowadogo wakifanya biashara ya matunda kandokando ya barabara itokayo Sumbawanga kuelekea Mpanda. Aliwaunga mkono wajasiriamali hao kwa kununua bidhaa zao na kuwapa kinamama waliokuwa na watoto zawadi kidogo ya fedha ambazo waligawana na watoto zao.

Hili eneo linaitwa Magamba ambalo lipo wilayani Mpanda ambapo katika msimu huu wa masika maembe mengi yanapatina katika eneo hili, Ndoo moja ya maembe inayoonekana inauzwa shilingi alfu mbili. Ni fursa kubwa kwa wawekezaji kujenga miundombinu katika maeneo haya kwa ajili ya viwanda vya kusindika matunda na kusafirisha bidhaa hiyo.

Katika ziara yake hiyo alipata fursa ya kuzungumza na viongozi wa Halmashauri ya Mji Mpanda na kujadiliana nao baadhi ya mambo. Aliiagiza Halmashauri ya Mji Mpanda kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato mbali na ilivyokuwa navyo hivi sasa kuweza kuongeza wigo wa kodi za Halmashauri hiyo. Aidha alimuagiza Mkurugenzi wa Mji Mpanda kuzingatia usawa wa kijinsia kwenye kuajiri katika Halmashauri hiyo. Hiyo ilikuja kutokana na kuwepo kwa wanaume wengi zaidi ya asilimia 90 kwenye kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na wafanyakazi wa Halmashauri hiyo ya Mji Mpanda.

Alipata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari ambapo alizungumzia mambo ya kadha wa kadha likiwepo suala la nafasi za ajira zinazopatikana Mkoani Rukwa na kuwatoa hofu watanzania ambao hupata fursa ya kuja kufanya kazi Rukwa na kuacha kufika kwa visingizio kuwa hakufai kuishi na kwamba ni Mkoa wa pembezoni pamoja na kuuhusisha na mambo ya kishirikina. Alisema kuwa Rukwa ni pahala salama sana kwa makazi na hakuna matatizo yeyote, yote mabaya yanayozungumzwa kuhusu Rukwa hayana ukweli wowote. Alisema "mimi nimekaa Rukwa na nimeona ni jinsi gani wananchi wake walivyo wakarimu na wenye upendo wa hali ya juu"

Alifanya kikao cha kazi na viongozi wote wa Mkoa wakiwemo wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa idara za Serikali ikiwemo Jeshi la Polisi, Magereza, TAKUKURU, Usalama wa Taifa, Uhamiaji na wakuu wa idara katika Sekretarieti ya Mkoa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda. Aliwata viongozi hao kila mmoja kutimiza wajibu wake na kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ushirikiano wa karibu miongoni mwao kuleta ufanisi katika shughuli za Serikali kwenye ngazi ya Mkoa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na Msafara wake ambao ni Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima, Mkuu wa Wilaya ya MpandaMhe. Dkt. Rajab Rutengwe na wasaidizi wake wengine pamoja na viongozi wa Halmashauri walifanya ziara kwenye Kampuni ya Uyeyushaji na ununuaji wa Shaba kutoka Uturuki ya TPM Mining.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ofisi za TPM Mining. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe. Dkt. Rajab Rutengwe na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akiwa na mwenyeji wake kiwandani hapo ambae ni Kaimu Meneja wa Uzalishaji Kiwandani aliyejulikana kwa jina moja la Mermet ambae pia ni Raia wa Uturuki.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya (MB) alionyeshwa makaa ya mawe yenye jumla ya tani 300 yaliyoagizwa kutoka China kwa ajili ya kuzalishia umeme wa kuendesha mitambo na shughuli za Kampuni hiyo. Aliwapasha wawekezaji hao kuacha kununua makaa hayo nje na badala yake wanunue hapa nchini. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe. Dkt. Rajab Rutengwe. 

Alionyeshwa pia vyakula mbalimbali wanavyoagiza wawekezaji hao kutoka nchini kwao Uturuki. Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliwataka wanunue vyakula vinavyopatikana hapa nchini.

Baadhi ya vyakula hivyo na vinywaji mbalimbali

Store ya kuhifadhia vifaa na vyakula vya Kampuni hiyo

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akiangalia moja ya madini yanayonunuliwa na Kampuni hiyo ya Kituruki Wilayani Mpanda, Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Dkt. Rajab Rutengwe.

Mkuu wa Mkoa na Msafara wake wakiangalia vyakula vinavyoagizwa na Kampuni hiyo kutoka nje ya nchi (Uturuki)

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya alipewa zawadi ya mapambo na wawekezaji hao, Kampuni ya TPM Mining.

1 comment:

 1. Shukrani kwa taarifa hizi na zingine unazoweka katika blogu hii. Navutiwa kuona taarifa za mkoa ambao sijawahi kufika na taarifa zake hazikuwa zinapatikana kirahisi, hata mtandaoni. Sasa mambo ni mazuri kutosha.

  Napenda tu nigusie hili suala la hao waTuruki kuagiza vyakula kutoka nchini kwao. Ni kweli, ingekuwa bora wanunue vyakula hapa hapa Tanzania.

  Mimi ni mtafiti na mwandishi katika masuala ya tofauti za tamaduni hapa duniani. Suala la chakula linapambanua utamaduni moja na mwingine. Hata kwetu ni hivyo hivyo. Vyakula vya Mchagga, kwa mfano, kwa ujumla ni tofauti na vile vya Mpemba.

  Sasa hao wa-Turuki isije ikawa wanaagiza kutoka kwao kwa msingi huo. Ingefaa tupate taarifa zaidi. Mwarabu akiwa hapa Mpanda, sitashangaa akiagiza tende kutoka Arabuni.

  Pamoja na kuwa ingekuwa vema iwapo hao wa-Turuki wangenunua vyakula vya kwetu, kuna pia jambo ambalo tunaweza kujifunza kutoka kwao. Mimi ni m-Tanzania ambaye niko hapa ughaibuni, lakini huwa natafuta vyakula kwenye maduka ya wa-Afrika ambao wanauza vyakula vya kwetu. Natumia chai na kahawa ya Tanzania, kama nilivyoeleza hapa.

  Sisi wa-Tanzania tuna kasumba ya kutisha ya kushabikia vitu vya nje, vitu vya mamtoni. Mtu anafurahi avae nguo kutoka Paris au London, au raba mtoni, au atumie marashi na sabuni kutoka nje, wakati vingi vinatengezwa Tanzania. Kwa kufanya hivyo, tunaangamiza viwanda vyetu, tunajikosesha ajira, na tunajenga uchumi na ajira kwenye nchi za wenzetu.

  Nimeandika hayo kwenye kitabu kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Lakini tuna tatizo jingine kubwa Tanzania. Watu hawasomi vitabu.

  ReplyDelete