Sunday, January 22, 2012

HABARI KUTOKA MKOA JIRANI WA RUVUMA: RC RUVUMA AWAASA VIJANA WA JKT KUWA WAZALENDO NA NCHI YAO

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu akihutubia wakati wa kufunga mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana 822 katika kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa Mlale wilaya ya Songea mkoani Ruvuma

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said  Mwambungu akikagua gwaride lililoandaliwa na wahitimu wa mafunzo ya awali ya kiejshi katika kikosi cha 842 Mlale JKT ambapo alikuwa mgeni rasmi.Jumla ya vijana wapatao 822 wamehitimu mafunzo hayo juzi. Anayemuongoza Mkuu huyo wa Mkoa ni kiongozi wa gwaride hilo Meja Ramadhan.

Wahitimu wakipita mbele ya jukwaa na kutoa heshima kwa mgeni rasmi wakati wa gwaride la kuhitimu mafunzo ya awali ya kijeshi yaliyofanyika juzi katika kikosi cha 842 KJ Mlale JKT.Jumla ya vijana 822 walihitimu mafunzo hayo yaliyofungwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu

Na Revocatus Kassimba- Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa RUVUMA.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu  amewaasa vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kuwa wazalendo na wenye kuipenda nchi yao ili waweze kuitumikia iweze kuwa na Maendeleo  endelevu.
Ametoa wito huo juzi wakati akifunga mafunzo awali ya kijeshi  yaliyojulikana kama Oparesheni  Miaka 50 ya Uhuru yalitolewa katika kikosi cha jeshi 842 Mlale JKT  kilichopo Wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma.
Mwambungu amewapongeza Vijana hao kwa kuonyesha moyo wa kizalendo tangu wajiunge na mafunzo hayo mwaka jana Julai ambapo wamejifunza mambo mengi yakiwepo stadi za kazi na mafunzo ya awali ya kijeshi.
Aliongeza kusema  kuwa mafunzo haya yatasaidia kujenga moyo wa kuipenda nchi hususani katika kipindi hiki ambacho maadili miongoni mwa Vijana yanaporomoka hivyo kwa kujiunga na jeshi la kujenga Taifa Vijana hupata Elimu na maarifa ya kujitegemea na hatimaye kuwa Vijana mahiri katika Utendaji kazi.
Alitumia pia fursa hiyo kuwapongeza Vijana wote walioshiriki katika operesheni ya kusomba mahindi kutoka kwa wakulima kipindi cha mwisho wa mwaka uliopita ili kunusuru mazao ya wakulima kuharibika
“Nawapongeza kwa umahiri wenu katika kipindi cha oparesheni ya kusomba mahindi kutoka kwa wakulima kwani agizo nililotoa kwa makamanda wenu lilitekelezwa vyema” sasa wakulima wana nufaika na kazi mliyoifanya huo ndio uzalendo alisisitiza mkuu wa Mkoa huo.
Awali akitoa taarifa ya mafunzo kwa Mkuu wa Mkoa, Kaimu kamanda kikosi cha 842 KJ Mlale Meja T. S. Mpupu  alisema mafunzo hayo ya awali ya kijeshi  yalianza tarehe 26 Julai 2011 na kuhitimishwa tarehe 20 Januari 2012 lakini yatendelea hadi kipindi cha mkataba wa miaka miwili kitakapoisha.
Aliongeza kusema wakati wanaanza kulikuwa na Vijana wapatao 827 kutoka katika mikoa yote ya Tanzania na hadi wanahitimu ni Vijana 822 kati yao wavulana ni 671 na wasichana 152.
Aliendelea kueleza kuwa Vijana watano hawakuhitimu mafunzo kutokana na watatu wao kufariki dunia kwa matatizo ya ugonjwa na wawili kutoroka mafunzo hayo.
Aidha kwa upande wake mwakililishi wa Mkuu wa Jeshi la kujenga Taifa Luteni Kanali Malembo aliwakumbusha wahitimu hao juu ya kiapo walichoapa mbele ya mgeni rasmi kuwa wataeendeleza utii  na kuitumikia nchi ya Tanzania kwa  uaminifu,utii na uhodari siku zote.
Alisema kuwa watakapotoka hapo (Mlale) watasambazwa katika makambi mengine nchini ili wakaendelee na mafunzo ya stadi za uzalishaji hadi kipindi cha miaka miwili kitakapoisha hivyo aliwasihi kuwa na nidhamu.
“Nidhamu ni kitu cha msingi unapokuwa Ndani ya Jeshi la Kujenga Taifa” alisema Luteni Kanali Malembo.
Kikosi cha jeshi Mlale JKT kilianzishwa mwaka 1970 kikiwa na Malengo ya kuwalea Vijana  kwa kuwapatia mafunzo na stadi za uzalishaji mali ili wakihitimu waweze kuajiriwa na serikali au wajitegemee katika kuendeleza Uchumi wao na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment