Wednesday, January 11, 2012

HALMASHAURI YA WILAYA YA SUMBAWANGA YASHAURIWA KUONGEZA MAKUSANYO YA MAPATO

Mwenyekiti wa Halmshauri ya wilaya ya Sumbawanga Godfrey Sichona (Katikati) akiendesha kikao cha kamati ya Fedha, Utawala na Mipango ya wilaya Sumbawanga. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Christian Laizer.
 
Mbunge wa jimbo la Kalambo Mkoani Rukwa Josephat Kandege (wa kwanza kulia) na wajumbe wengine wakifuatilia kikao cha Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga jana.
 
Baadhi ya wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga wakifuatilia kikao hicho.

NA RAMADHANI JUMA,
AFISA HABARI- OFISI YA MKURUGENZI -SUMBAWANGA

KAMATI ya Fedha Utawala na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya Sumbawanga imeshauri uongozi wa Halmashauri hiyo kuongeza ufuatiliaji wa ukusanyaji wa ushuru wa mazao ya uvuvi katika ziwa Tanganyika ili kujiongezea mapato zaidi kupitia chanzo hicho.

Baadhi ya wajumbe walishauri ufuatiliaji wa kina ufanyike juu ya taarifa za ukusanyaji wa ushuru unaofanywa na mtumishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayekusanya ushuru wa samaki wanaosafirishwa nje ya nchi, na pia kuweza kujua kama Halmashauri inatakiwa kupatiwa kiasi cha fedha zinazotokana na makusanyo hayo.

Akizungumza wakati wa kikao cha kamati hiyo kilichoketi tarehe 9 Januari mwaka huu, Mbunge wa jimbo la Kalambo Mheshimiwa Josephat Kandege ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo alisema bado kuna mianya mingi ya ukwepaji kodi kwa watumiaji wa ziwa hilo hivyo Halmashauri ifanye juhudi katika kuziba mianya hiyo.

Mheshimiwa Kandege pia aliishauri Halmashauri kufuatilia na kujua kiasi cha fedha kinachokusanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika ukanda wa Ziwa hilo kama ushuru wa mazao ya ziwani na kuwasilisha taarifa hiyo mbele ya kamati hiyo, ikiwa ni pamoja na taarifa ya kiasi cha fedha ambazo Halmashauru inastahili kupatiwa kama sehemu ya makusanyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Christian Laizer aliahidi kulifanyia kazi shauri huo kama ulivyotolewa na kamati hiyo ambapo taarifa ya utekelezaji itatolewa.
Kamati hiyo inatarajiwa kukutana tena tarehe 18 Januari mwaka huu, katika ukumbi wa Halmashauri hiyo uliopo eneo la Bomani ambapo taarifa mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya Maendeleo zitawasilishwa na kujadiliwa.

No comments:

Post a Comment