Saturday, January 14, 2012

KAMPENI YA "SUMBWANGA NG'ARA" YAZIDI KUPAMBA MOTO, MKUU WA MKOA WA RUKWA ASHIRIKI NA WATUMISHI KUFANYA USAFI KATIKA JENGO LA OFISI YAKE

Mara baada ya kuzindua Kampeni ya kudumu ya usafi wa Mji wa Sumbawanga ya "SUMBAWANGA NG'ARA" Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (Pichani Kulia) ameendeleza kampeni hiyo kwa kushiriki na watumishi wa ofisi yake jana katika usafi wa mazingira ya Ofisi hiyo. Usafi uliofanyika ni pamoja na kufagia, kufyeka na kusafisha baadhi ya mitaro ya maji nje ya jengo hilo.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, usafi kama huo utakuwa unafanyika mara moja kila mwezi na aliwaasa watumishi hao kuendeleza kampeni hiyo hadi majumbani kwao pamoja na kuhamasisha wananchi wote wa Mji wa Sumbawanga. "Lengo letu ni kuona Mji wa Sumbawanga unabadilika na kuwa Msafi na wa kuvutia ikiwezekana uwe mfano kwa miji mingine nchini" alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Alisema kuwa usafi huo utakuwa ni wa kudumu kwa kushirikisha taasisi zote hapa Mkoani ambapo taasisi hizo zitashindanishwa ambapo washindi wawili wa mwanzo na wawili wa mwisho watatangazwa kupitia vyombo vya habari vya hapa mkoani Rukwa. Usafi huo pia utajumuisha maeneo yote ya Mji ikiwepo mitaa na barabara kuu katika mji wa Sumbawanga. Kampeni hiyo itaenea hadi kufikia katika kila kaya katika Mji wa Sumbawanga.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa anaomba Kampeni hii ya usafi isiwe kama adhabu au ya kulazimishana bali kila mtu kwa nafasi yake aichukulie kama sehemu ya maisha yake na jukumu lake la msingi kwani mwisho wa siku kampeni hii ikifanikiwa sifa itakuwa ni kwa kila mmoja aliyeshiriki kwa namna moja ama nyingine.

USAFI KATIKA MJI WA SUMBAWANGA UNAWEZEKANA KILA MMOJA WETU AKISHIRIKI KWA NAFASI YAKE.

No comments:

Post a Comment