Thursday, January 19, 2012

FAHAMU ENEO LILILOTENGWA TANGU MWAKA 1984 KWA AJILI YA KUJENGWA UWANJA WA NDEGE KATIKA MJI WA SUMBAWANGA, KUNA HAJA YA ENEO HILI SASA KUENDELEZWA?

Hili ni eneo la Kisumba takribani Kilomita 23 nje kidogo ya Mji wa Sumbawanga. Eneo hili lipo ndani ya Manispaa ya Sumbawanga. Eneo hili lilitengwa tangu mwaka 1984 enzi za Utawala wa Mhe. Maj. Gen. T. Kiwelu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa wa awamu ya tatu tangu Mkoa huo uanzishwe mwaka 1974.

Kutokana na kuwepo kwa fedha kwa ajili ya kuboresha uwanja mdogo wa ndege wa sasa ambao upo katikati ya Mji wa Sumbawanga, Uongozi wa Mkoa wa Rukwa ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Injinia Stella Martin Manyanya umeona kuna haja kubwa ya fedha hizo kuhamishiwa katika eneo hili la kudumu ambalo ni kubwa kutosha kujenga uwanja mkubwa wa kimataifa.

Haja hiyo imekuja kutokana na sababu kuu mbalimbali moja ikiwa ni udogo wa eneo la uwanja wa sasa hali itakayopelekea Mkoa kuwa na uwanja mdogo usiokidhi mahitaji yote ya usafiri wa anga. Hata hivyo kutakuwepo na haja ya kupanua uwanja huo kama ukifanyiwa maboresho jambo litakalosababisha migogoro na wananchi litakapokuja suala la kuhamishwa wananchi hao.

Tatu kutakuwepo na ulazima wa kuwafidia wananchi watakaohamishwa jambo litakaloigharimu Serikali wakati kuna eneo hilo kubwa ambalo lipo wazi kuweza kujengwa uwanja mkubwa zaidi hata kama ujenzi wake utachukua muda mrefu. "Ni bora nguvu ya kuboresha uwanja huo mdogo ipelekwe kujenga uwanja mkubwa ambao utakuwa ni wa kudumu katika eneo la Kisumba ambalo lilishatengwa kwa ajili hiyo hata kama ujenzi huo utachukua miaka mitatu, faida yake itakuwa kubwa" alisema Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya.

Sababu nyingine ni kuwa, baadhi ya marobani wamekuwa wakisikika wakisema uwanja wa ndege wa Sumbawanga ni kipimo tosha kwa robani mzuri kutokana na ugumu wake wakati wa kutua na kupaa. Aidha wataalam nao wanasema kuwa uwanja wa ndege ukiwa katikati ya Mji ni tatizo kwani barabara za magari humchanganya robani na barabara za mapitio ya ndege jambo linaloweza kusababisha ajali mda wowote.

Uwanja mdogo wa ndege wa Sumbawanga umezungukwa na makazi ya wananchi jambo ambalo sio salama kwa wananchi husika pamoja na uwanja pia. Hivyo kuna haja kubwa ya nguvu hiyo ya kukarabati uwanja huu kupelekwa katika eneo lililotengwa kuepusha migogoro na wananchi.

Eneo hili la Kisumba lipo katika barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami inayoelekea Matai- Kasanga. Uwepo wa barabara hii itakuwa ni kiunganishi kizuri cha uwanja huo utakaojengwa na Mji wa Sumbawanga na Wilaya mpya ya Kalambo ambapo uwanja huo utakuwa katikati ya Wilaya hizo mbili.

Hata hivyo katika ziara ya hivi karibuni ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alikuta sehemu kubwa ya eneo hilo ikiwa wazi na sehemu ndogo ikiwa imevamiwa na wananchi ambao wamelima na baadhi yao kujenga vijumba vya muda. Mkuu huyo wa Mkoa alitumia fursa hiyo kumuagiza Mkuu wa Kitengo cha Miundombinu Mkoa kupima eneo hilo. Aidha alimuagiza Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisumba Ndugu Nestori Kakwaya ashirikiane na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga katika kuzungumza na wananchi wa eneo hilo wafaham dhima ya Serikali juu ya eneo hilo na kwa wale ambao wameshahodhi maeneo waweze kuayaachia mara moja. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (wa pili kulia) akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Kanali John Antonyo Mzurikwao (wa pili kushoto) na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisumba Bw. Nestori Kakwaya kuhusu uwanja huo.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Meneja wa Tanroad Mkoa wa Rukwa, Katibu Tawala Msaidizi Kitengo cha Miundombinu, Naibu Meya Manispaa ya Sumbawanga na Afisa Habari Mkoa wa Rukwa walipotembelea eneo hili la Kisumba.

Uwanja Mdogo wa Ndege wa Sumbawanga. Hapo akionekana Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Joyce Mgana akimkaribisha Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Lazaro Nyarandu alipokuja kufungua maonesho ya Sido Kanda ya Nyanda za Juu Kusini katika uwanja wa Nelson Mandela mwishoni mwa mwaka jana.

4 comments:

 1. It makes sense to have a new airport in Kisumba. The existing airport is small and it is dangerous for the pedestrians who cross the airport.
  Mdau wa Edeni A

  ReplyDelete
 2. Ukijengwa uwanja mpya wa ndege, huo wa sasa utengenezwe kama bustani na eneo la mapumziko. We need open spaces to relax!
  Nawakilisha.

  ReplyDelete
 3. This RC is doing terrific job. She is great lady and I am impressed with her dedication and hard-work. She makes me remember General T. Kiwelu.

  ReplyDelete
 4. Nampongeza sana sana Mkuu Wa Mkoa Inj.Manyanya kwa uamuzi aliotoa kuhusu uwanja wa ndege wa Kisumba kujengwa badala ya kuendeleza Uwanja uliopo katikati ya mji. napendekeza uwanja wa sasa upimwe viwanja na kupewa Shirika La Nyumba ili zijengwe nyumba za kukopesha na kuuza kwa wananchi kwani shirika la nyumba litajenga nyumba bora nzuri na kuleta sura nzuri ya mji....Tamim Said

  ReplyDelete