Sunday, January 29, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AISHAURI HOSPITALI YA WILAYA YA MPANDA KUBUNI VYANZO VIPYA VYA MAPATO KUTATUA MATATIZO MADOGOMADOGO YANAYOIKABILI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda Dkt. Yahya Hussein alipomtembelea Ofsini kwake jana kufuatia malalamiko ya watumishi katika hospitali yake juu ya madai ya mapunjo ya stahili zao ikiwepo malipo ya muda wa ziada, malipo ya nyongeza ya mshahara na usafirishaji wa mizigo.

Ofisini hapo alipokea taarifa ya madeni yaliyokwishahakikiwa  ya watumishi hao ambayo jumla yake ni zaidi ya Milioni 100. Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo alimueleza Mkuu huyo wa Mkoa kuwa kikwazo kikubwa cha kushindwa kulipa madai hayo ni mtiririko mbovu wa OC ambayo inatolewa na Serkali kila mwezi. Alisema kuwa mtiririko wa fedha wanayopewa haiendani na bajeti yao, alisema kuwa kwa mwezi anatakiwa kupewa zaidi ya Milioni 20 ili kuendesha shughuli zao bila kikomo lakini cha kushangaza huweza kupata Milioni 9 na fedha nyingine huchelewa jambo linalokwamisha utendaji kazi hospitalini hapo.

Aliongeza kusema "unaweza kupitisha likizo ya mtumishi katikati ya mwezi kwa mategemeo ya kumlipa stahili zake za likizo ifikapo mwishoni mwa mwezi lakini OC inakuja kidogo na hivyo tunashindwa kutimiza majukumu hayo na mengineyo ya msingi".

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Naomi Nko alisema kuwa upande wa madai ya nyongeza ya mishahara ambayo madai yao ndio makubwa kwa wale watumishi waliopandishwa vyeo, tatizo kubwa lipo wizarani (Utumishi)ambapo kwani taarifa zao zimeshapelekwa na utaratibu wa kuwabadilishia mishahara yao bado halijafanyiwa kazi kikamilifu. Alisema kuwa "Mtumishi huwezi kulipwa malimbikizo kabla ya kupewa mshara mpya jambo ambalo lipo chini ya Wizara husika".

Kufuatia kupokea taarifa hiyo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya ameishauri Hospitali hiyo kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda kubuni vyanzo vipya vya mapato ikiwepo kutilia mkazo sera ya kitaifa ya wananchi kuchangia katika huduma ya afya. "Kuna madeni mengine madogomadogo mfano kuna watu wanadai 5000 kwenye taarifa yenu hii, ni wazi mkiwa na vyanzo vyenu wenyewe vya mapato mnaweza kulipa madeni madogomadogo kama haya" alisema Injinia Manyanya. 

Kufuatia migomo ya madaktari nchini Mkuu huyo wa Mkoa aliwaasa madaktari kuwa na moyo wa kizalendo na subira kwa kutoa muda kwa uongozi uliopo serikalini ili uweze kutatua matatizo yao. Kupitita Mganga Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo ya Wilaya aliwashauri Madaktari wote nchini kuona na jinsi gani wataunda timu ya majadiliano ya kitaifa juu ya hatma ya sekta ya afya nchini.

No comments:

Post a Comment