Tuesday, January 31, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AMUWAKILISHA WAZIRI MKUU KWENYE MAHAFALI YA KIDATO CHA SITA SHULE YA SEKONDARI USEVYA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injnia Stella Manyanya akisalimiana na baadhi ya viongozi na maafisa elimu wa Wilaya ya Mpanda na Mkoa wa Rukwa mara baada ya kuwasili katika mazingira ya shule ya Sekondari ya Usevya tayari kushiriki mahafali ya Kidato cha Sita kwa niaba ya Waziri Mkuu ambaye hakuweza kuhudhuria kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine muhimu ya kiserikali. Shule ya Sekondari Usevya ipo Wilayani Mpanda Jirani na Kijiji cha Kibaoni ambacho ni Nyumbai kwa Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda. 

Mkuu wa Mkoa akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Shule hiyo. Anayeshuhudia ni Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Naomi Nko.

Mkuu wa Mkoa alianza shughuli za mahafali hayo kwa kukagua Kikosi cha Gwaride la shule hiyo ambacho kilikuwa kimejipanga kikakamavu bila ya kutikisa hata kidole.

Vijana wa Shule ya Sekondari Usevya walionekana kuwa na vipaji mbalimbali, hapa ikiwa ni baadhi ya wanafunzi wanaohitimu wakijiandaa kwa namna yake kwa ajili ya kusoma Shairi kwa Mgeni Rasmi.

Risala ya Wanafunzi wanaohitimu ikisomwa kwa Mgeni Rasmi, Kushoto ni Gatus Mgasira na Mussa Hussein.

Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Naomi Nko alishindwa kuvumilia na kuamua kuinuka kusakata rumba na wanafunzi wanaohitimu.

Risala ya wanafunzi wanaobaki ikisomwa na Mwanafunzi Revocatus Pigangozi.

Baadhi ya wanafunzi waliandaliwa kuonyesha gwaride maalum lililopita mbele ya Mgeni Rasmi, Wanafunzi hawa walioneka kupikwa vizuri kwani walionyesha ukakamavu wa hali ya juu.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Usevya Mwl. Makanganya Makalanga akisoma taarifa ya shule yake kwa Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Manyanya.
Alisema kuwa Shule yake ilianzishwa mwaka 2006 ikiwa na wanafunzi 80, lakini mwaka 2010 walihitimu wanafunzi 18. Mwaka jana 2011 Shule hiyo ilikuwa ya kwanza kimkoa na ikashika nafasi ya 26 kitaifa hali iliyompa moyo Waziri Mkuu na kutoa zawadi ya 100, 00/= kwa kila mwalimu na 50, 000/= kwa kila mjumbe wa bodi ya shule hiyo.
Mkuu huyo wa shule akikabidhi taarifa yake hiyo kwa Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Lilifuata zoezi la ugawaji wa vyeti kwa wanafunzi wanaohitimu. Hapo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akimkabidhi cheti mmoja ya wahitimu katika Shule hiyo.

Burudani ya Muziki kutoka kwa wanafunzi wanaohitimu ilichukua nafasi yake kuweka mazingira sawiyya.

Ilifika wakati Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kutoa nasaha zake kwa wanafunzi wanaohitimu. Kwanza kabisa aliwaambia wanafunzi hao kuwa alikuwepo mahala hapo kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda ambaye hakuweza kuhudhuria mahafali hayo kutokana na kukabiliwa na shughuli nyingine muhimu za kiserikali.
Katika nasaha zake hizo aliwataka Wanafunzi hao kujijengea fikra za kujiajiri pindi wamalizapo masomo yao na sio kubaki kuitegemea Serikali ambayo ina mambo mengi ya kufanya. "Jitahidini muokoe maisha yenu wenyewe, mnahitaji kulea maisha yenu...Askari namba moja ni wewe kuikoa familia yako" Alisema Injinia Manyanya.
Alizungumzia pia suala la mimba za mashuleni na kusema kuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya elimu mashuleni. Aliwaasa wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuwaahidi wale wote watakaopata Division One na Two atahakikisha anawasaidia kupata Shule za kujiendeleza.
Katika nasaha zake hizo aliwataka wanafunzi hao kutopumbazika na kauli za baadhi ya viongozi na wananchi kuwa eti Watanzania ni masikini. Aliwataka kutumia fursa waliyonayo katika kuhakikisha jamii inaondokana na fikra hizo na kujiendeleza zaidi kielimu waweze kuikomboa jamii ya wanarukwa.
Kwa upande mwingine aliwataka wazazi wote Mkoani Rukwa kuwasaidia watoto wao kufikia malengo ya kuwa na elimu bora. Aliomba ushirikiano kutoka kwa wazazi pamoja na waalimu ili kuiweka Rukwa katika hatua nyingine kielimu. Aliwaasa wazazi kuchangia huduma za elimu ikiwepo chakula mashuleni.
Alisema kuwa Rukwa kama Mikoa mingine inakabiliwa na tatizo la uhaba wa waalimu na kuwataka waalimu wanaopangiwa Rukwa kuondokana na fikra potofu za imani za kishirikina na kwamba Rukwa ni Mkoa salama ambao mambo hayo sasa yamebaki kuwa ni historia.
Kuna wakati aliamua kuinuka na kuiacha meza kuzungumza na wanafunzi kwa ukaribu huku akitumia mifano halisia. Aliwaita baadhi ya watumishi kutoka Ofisi yake akiwepo Katibu wake na Afisa Habari wake pamoja na Afisa Tawala Wilaya ya Mpanda na Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda. Aliwatumia watumishi hao kama mfano wa  mafanikio ya elimu kwa wanafunzi wanaohitimu na kuwaeleza kuwa wana fursa kubwa ya kufikia mafanikio watumishi hao waliyofikia cha msingi ni kujitambua, kujiwekea malengo na kusoma kwa bidii.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ndiye aliyefungua Muziki ikiwa ni ratiba ya mwisho kwenye mahafli hayo. Hapo akionekana na baadhi ya wanafunzi wakivunja mifupa.

Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na wanafunzi wanaohitimu kidato cha sita 2012 shule ya Sekondari Usevya.

No comments:

Post a Comment