Saturday, January 14, 2012

WAALIMU RUKWA KULIPWA MALIMBIKIZO YAO

WALIMU wa shule mbalimbali mkoani Rukwa hivi karibuni wanatarajiwa kulipwa zaidi ya Sh bilioni 1 ikiwa ni malipo ya malimbikizo yao.

Malipo hayo ni malimbikizo ya stahiki mbalimbali za walimu hao zikiwemo mishahara, kupanda cheo na uhamisho.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya amebainisha hayo alipokuwa anafunga mafunzo elekezi ya programu ya Maji, Afya na Usafi wa Mazingira - SWASH yaliyofanyika mjini hapa.

Bila ya kutaja ni lini walimu hao wataanza kulipwa alisema kuwa kiasi hicho cha fedha
kimeshapokelewa baada ya madeni ya walimu hao kuhakikiwa kwanza na mamlaka husika.


Akifunga semina hiyo alisema: ”Napenda pia kugusia suala la rushwa na uharibifu wa mazingira kuwa yanaathari kubwa kwa wanajamii wote na hata kwa vizazi vijavyo kwa kuwa
daima vinarudisha nyuma maendeleo”.

Mafunzo hayo ya siku tatu yaliwajumuisha wataalamu kutoka kada mbalimbali ngazi ya Mkoa na kutoka halmashauri zote tano.

Washiriki 71 walipata fursa ya kujadili mada mbalimbali ikiwemo elimu ya maji, afya na usafi
wa mazingira kuanzia ngazi ya Kaya hadi shuleni.

Alibainisha kuwa mkoa umeanza mkakati wa kuwa na shule ya mfano ambayo itawekewa
mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia ndani na nje ambapo shule zingine wataiga.

Pia alieleza kuwa tayari mchakato unaendelea wa ujenzi wa choo cha mfano katika Shule ya Msingi Mbalika katika Manispaa ya Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Manyanya akinawa mikono kwa sabuni kwa kutumia kifaa kinachoitwa "Kibuyu Chirizi" kilichobuniwa na wakufunzi wa programu ya SWASH kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao Shule zao hazina miundombinu bora ya maji. Kifaa hicho kinaambatana na kauli mbiu ya programu hiyo kuwa "Nawa mikono kwa sabuni kuepuka kula Kinyesi". Programu ya SWASH inahusikana elimu ya maji, afya na usafi wa mazingira kuanzia ngazi ya Kaya hadi shuleni. 

No comments:

Post a Comment