Sunday, January 1, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AWAASA WAANDISHI WA HABARI WA MKOA HUO, KUWAANZISHIA TUZO YA MWANDISHI BORA WA MWAKA

Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Mhe. Eng. Stella Manyanya akizungumza na wadau wa habari wakati akifungua mkutano wa wadau hao ulioandaliwa na klabu ya waandishi wa habari wa mkoa wa Rukwa. Kushoto ni Mwenyekiti wa RKPC na Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Kanali John Mzurikwao. Picha na Mussa Mwangoka.

Mwandishi wa habari Bw. Sammy Kisika, akiwa na wadau wa habari wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa siku ya mkutano wa wadau hao.

Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya (MB) wa kwanza kushoto waliokaa, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Kanali John Mzurikwao katikati na waandishi pamoja na wadau wa habari wa Mkoa huo.

Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari ya Mkoa wa Rukwa, Felician Simwella akisoma taarifa ya klabu hiyo kwa mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya (MB) aliyekaa-kulia.

Mdau wa habari, Crepinus Rwegasira ambaye ni meneja wa TTCL mkoa wa Rukwa akitoa mchango wake katika kikao hicho cha wadau wa habari.

WAANDISHI wa habari mkoani Rukwa, wametakiwa kutumia taaluma yao  kutangaza fursa za kiuchumi za mkoa huo, ikiwa ni njia moja wapo ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya, wakati alipofungua mkutano wa wadau wa habari, ulioandaliwa na Klabu ya waandishi wa habari ya mkoa huo (RKPC) na kufanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa (RDC) uliopo katika Manispaa ya Sumbawanga.

Alisema kuwa mkoa wa Rukwa una fursa nyingi za uwekezaji, pamoja na kutangazwa katika Kongamano la Uwekezaji la Ukanda wa Ziwa Tanganyika lililofanyika mwezi Oktoba mwaka jana, bado wanahabari wanafursa ya kuendelea kutangaza fursa hizo lengo likiwa ni kuvutia wawekezaji ambao wakiwekeza itasaidia kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja, mkoa na taifa kwa ujumla.

Alisema kuwa Serikali inajitahidi kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuboresha miundombinu ya barabara ambapo zile zinazounganisha Mkoa huo na ile ya jirani zinajengwa kwa kiwango cha lami. Aidha viwanja vya ndege, bandari ya Kasanga na kipili navyo vinaendelea kujengwa, hivyo ni jukumu la waandishi kuandika juu ya fursa za uwekezaji zilizopo na uboreshaji wa miundombinu hiyo.

"Jicho la maendeleo mkoa Rukwa ni nyie waandishi wa habari...... sasa tangazeni mazuri yaliyopo, fursa za uwekezaji katika kilimo, madini, utalii na maeneo mengine  bila kusahau elimu ili wajitokeze wawekezaji wa ndani na nje hali hii itasaidia kupunguza umasikini wa kipato kwa mtu mmoja mmoja, Mkoa na taifa pia" alisema Mhandisi Manyanya.

Aliongeza kuwa uongozi wa Mkoa wa huo umepanga kuhakikisha kuwa katika bajeti ijayo kunakuwa na fungu la kuwawezesha waaandishi wa habari kiuchumi pale inapobidi, vitendea kazi ili waweze kutekeleza majukumu yao pasipo kipingamizi cha aina yoyote tofauti na sasa ambapo waandishi wengi hawana vitendea kazi hali inayowaathiri kiutendaji kwa namna moja au nyingine.

Hata hivyo, Manyanya aliongeza kuwa mkoa umeweka utaratibu ambao utaanza mwakani wa kutoa zawadi kwa mwandishi ambaye ameandika habari zenye kuleta tija na changamoto kwa Serikali ambapo mshindi atapatiwa zawadi ya Sh. milioni moja  huku mwandishi ambaye atabainika kukiuka miiko na kanuni za uandishi wa habari akipata adhabu ambayo hakuiweka bayana.

Mkuu huyo wa mkoa ambaye anaamini kufanya kazi na waandishi wa habari ni miongoni mwa chachu ya mabadiliko yenye tija kwa jamii, aliwashauri viongozi wa Klabu hiyo kuhamasisha wananchama wao na wao wenyewe kufanya kazi ya uandishi wa habari tofauti na ilivyo sasa kwani waandishi ni wachache ukilinganisha na idadi ya wanachama wa klabu hiyo.

Alisema " hapa nimewaona mko wengi sana wanachama wa klabu hii lakini waandishi wa habari ni sita tu sasa hii sio nzuri sana....... viongozi wahamasisheni wanachama wenu waandike kwenye vyombo vya habari vya hapa mkoani na nje ya mkoa lengo tuutangaze mkoa wetu'. 

Katika mkutano huo, changamoto nyingi zilijitokeza kutoka wadau, ambapo Mwl. Lusungu Kihahi alisema kuwa ipo haja kwa waandishi wa habari kuacha kukaa ofisi kusubiri kuletewa habari lakini wanapaswa wazitafute hasa kwa kufika vijijini ambako ndiko kuna matatizo na kero nyingi zinazohitaji ufumbuzi.

Alisema kuwa kero za maji, afya, elimu, ukosefu wa watumishi wa kada mbalimbali, pembejeo za kilimo kutofika kwa wakati, ushuru kwa wakulima ni nyingi kwenye maeneo hayo, sasa ni fursa nzuri kwa wanahabari kuyafikia maeneo hayo na kutangaza habari hizo ili serikali ifahamu na kuzitafutia ufumbuzi kwa haraka.

Naye,Bw. Osemu Chapita ambaye ni Katibu wa Chadema mkoa wa Rukwa, alisema kuwa waandishi wa habari wa mkoa wa Rukwa waache ubaguzi katika kuandika habari za kisiasa, kwa kukipendelea chama kimoja cha siasa ambacho hakukitaja jina chama hicho.

Aliongeza kuwa waandishi wanapaswa kuandika habari za mazingira na kukemea mauaji ya kujichukulia sheria mkononi ambayo yanakithiri kila kukicha katika mkoa huo.
"waandishi inalazima ifike wakati mjitolee kwaajili ya mkoa wa Rukwa, andikeni kuhusu uharibifu wa mazingira kwa sababu hili tatizo ni kubwa...... uhabirifu umekithiri mno, watu wanachoma moto misitu, ukataji wa miti hovyo, ujenzi holela, utiririshaji wa maji taka mjini lakini hamsemi nani atakaye tusemea sisi" alihoji Chapita.

Naye Padri Ponsiano Chomba ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Redio Chemchem cha Mjini Sumbawanga, alisema kuwa Serikali kwa ushirikiano na klabu hiyo wanapaswa kuangalia uwezekano wa kuanzisha gazeti la mkoa ambalo litakuwa na habari nyingi za mkoa huo kuliko ilivyo sasa ambapo waandishi wamekuwa wakitegemea zaidi vyombo vya habari za kitaifa ambako kuna wakati habari za Rukwa zimekuwa zikikosa nafasi.

"siku za nyuma tulikuwa na gazeti hapa likiitwa Rukwa leo kwanini lisifufuliwe..... tuweze kuwa na habari nyingi na sisi tuliobahatika kusoma kidogo taaluma hii tuweze kulitumia kwa kuandika mambo yanayohusu mkoa huu" Alisema Padri huyo .

Katika mkutano huo, mada tatu ziliwasilishwa ambazo ni Umuhimu wa vyombo vya habari katika mikoa ya pembezoni, Hali halisi ya vyombo vya habari katika mkoa wa Rukwa, Polisi jamii na ulinzi Shirikishi ambazo ziliwasilishwa na Bw.Sammy Kisika, Bw. Gurian Adolf (waandishi wa habari) na Bw. Sixmound Kibasa wa jeshi la polisi.

Mada hizo lizikonga nyoyo za wadau ambao wengi wao walisikika wakisema kwamba sasa tuna fursa nzuri ya kuwatumia waandishi wa habari baada ya kufahamu umuhimu wao na vyombo vya habari pia.

No comments:

Post a Comment