Thursday, February 2, 2012

JE WAYAJUA HAYA?

Hapa ni Kijiji cha Msisi tarafa ya Mtowisa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga barabara itokayo Mwese kwenda Milepa. (Kwa taarifa zaidi soma hapo chini) 

Katika kabila la wasukuma ambao pia wanapatikana kwa wingi Mkoani Rukwa kutokana na tabia yao ya kuhamahama kutafuta malisho ya mifugo yao, kuna Utamaduni wa kipekee katika kabila hilo kwa yule mtu ambaye amefankiwa kuuwa Simba kulinda mifugo yao. Mtu huyo huitwa "Nchimio Shimba" kwa Kisukuma au Mchoma Simba kwa Kiswahili.

 Jambo la kushangaza ni kwamba Mtu huyo hupewa mavazi maalum kama inavyoonekana pichani na Mganga ambaye pia humfanyia dawa za kienyeji kwa imani ya kumlinda kutokana na damu ya Simba iliyomwagika inayoaminika kuwa na madhara katika kabila lao, usipofanyiwa hivyo inaaminika kuwa unaweza hata kuchanganyikiwa. 

Akishakamilsha zoezi la kufanyiwa dawa na kuveshwa mavazi hayo Mtu huyo kazi yake kubwa huwa ni kutembelea ndugu jamaa na marafiki au mtu yeyote wa kabila hilo na kazi kubwa huwa ni kuimba na baadae kupewa Ng'ombe, Mbuzi au Fedha. Kazi hiyo huweza kuifanya kwa muda mrefu usiopungua miaka miwili na kuendelea. 

Huweza pia kusafiri Mkoa mmoja hadi mwingine, na kwa wasukuma hicho ni kitendo cha kishujaa na chenye sifa ya kipekee. Katika safari zake zote hizo hupewa tunzo kwa kufanikiwa kuua Simba na watu wa kabila lake.

 Chanzo cha habari hii kiliendelea kusema kuwa Mtu huyo akichoka kuvaa mavazi hayo na kutembea hurudi kwa Mganga wake aliyemfanyia dawa na kisha kumfanyia dawa nyingine na kumnyoa nywele zake zote kisha kuvuliwa mavazi hayo na kurudi kuishi maisha yake ya kawaida. 

Ikumbukwe kuwa wakati akiwa kwenye mavazi hayo mtu huyo huwa hafanyi kazi nyingine yeyote zaidi ya kuzunguka kuimba nyimbo na kupewa zawadi mbalimbali na watu wa kabila hilo.    

Mchoma Simba huvaa mavazi maalum huku akibeba Mkuki na Fimbo begani , Mwanvuli kujikinga na mvua, pamoja na Ngao maalum kama inavyoonekana pichani.

Viatu anavyovaa Mchoma Simba

Huyu ni bwana Mayyeka Rubinza Mkazi wa Kijiji cha Msisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa. Bwana Rubinza ni Msukuma na maelezo hayo aliyatoa yeye mwenyewe baada ya kujaribu kuongea na Mchoma Simba akagoma kuzungumza chochote kutokana na masharti ya Kabila hilo.

No comments:

Post a Comment