Wednesday, February 15, 2012

MAKAMU WA RAIS KUFANYA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU 7 MKOANI RUKWA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mohammed Gharib Billal.

Makamuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mohammed Gharib Billal atafanya ziara ya siku saba Mkoani Rukwa ambapo itajumuisha pia Mkoa mpya wa Katavi. Ziara yake hiyo itaanza tarehe 18 na kumalizika tarehe 24 Februari 2012 akitokea mkoani Ruvuma.
Awapo Mkoani Rukwa atatembelea Wilaya zote tatu za Mpanda, Nkasi na Sumbawanga. Mpanda atakuwepo kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 20 ambapo atapokea taarifa ya Serikali pamoja na Chama cha Mapinduzi. Aidha atafanya mkutano wa ndani katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Mpanda na mikutano wa nje katika uwanja wa Kashaulili na Ofisi ya Tarafa Inyonga.
Pamoja na hayo atapata fursa ya kuweka jiwe la msingi katika kituo cha afya katika tarafa ya Inyonga na kufanya Mkutano wa hadhara. Akiwa njiani kuelekea tarafa ya Mpimbwe ataona Mbuga ya Wanyama ya Katavi ambapo ataweka jiwe la msingi katika Ghala la Stakabadhi Mazao na kukabidhi hati za kimila za umiliki wa ardhi 300 katika kijiji cha Mwamapuli.
Akiwa wilayani Nkasi kuanzia tarehe 20 Februari 2012 Makamu wa Rais atapokea taarifa ya ujenzi wa barabara za Mkoa wa Rukwa na taarifa ya Wilaya ya Nkasi. Atafungua miradi ya maendeleo ikiwepo nyumba ya watumishi wa Halmashauri, Jengo la Utawala Shule ya Sekondari Nkomolo, na Daharia Shule ya Sekondari Korongwe. Atafanya pia Mkutano wa hadhara katika kiwanja cha shule ya Sekondari Korongwe.
Akimaliza ufunguzi wa miradi hiyo, ziara yake itahamia katika Wilaya ya Sumbawanga ambapo atamalizia ziara yake na kuelekea Mbeya kwa ajili kuendelea na zoezi kama hilo ambalo linategemewa kufanyika katika nchi nzima.
Mhe. Makamu wa Rais atawasili Sumbawanga tarehe 22 Februari 2012 akitokea Nkasi ambapo atapokelewa na viongozi wa Chama na Serikali ngazi ya Mkoa na Wilaya. Baada ya kupokelewa atapewa taarifa fupi ya Chama na Serikali.
Awapo Sumbawanga atapata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo ataweka jiwe la Msingi Jengo la ofisi ya Mkaguzi Mkazi Mkoa wa Rukwa na Jengo la benki ya CRDB. Atazindua Maghala ya kuhifadhi bidhaa bandarini yaliyopo Kasanga, Soko Jipya la Samaki Kasanga, na kampeni ya usafi katika Mji wa Sumbawanga “SUMBAWANGA NG’ARA” kwa kugawa vitendea kazi vya usafi.
Atapata pia fursa ya kusalimiana na wananchi katika maeneo yote ya miradi atakayotembelea ambapo atatembelea pia ngome ya “FORT BISMARK” iliyopo Kasanga na Kiwanda cha nyama cha SAAFI kinachomilikiwa na Mbunge Msataafu na mjasiriamali Ndugu Chrissant Mzindakaya.
Makamu wa Rais pia atafanya Mikutano wa hadhara katika viwanja vya Rukwa High School na Uwanja wa Mpira wa Laela. Atazungumza na wazee maarufu wa Wilaya ya Sumbawanga katika uwanja wa Ikulu Ndogo ya Sumbawanga.
Mhe. Makamu wa Rais atakamilisha ziara yake tarehe 24/02/2012 na kuondoka Sumbawanga kuelekea Mkoa jirani wa Mbeya ambapo atakuwa na ratiba ya ziara ya kikazi Mkoani humo.

No comments:

Post a Comment