Tuesday, February 21, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AIOMBA SERIKALI KUSAIDIA KUHAKIKISHA BARABARA ZA LAMI ZINAZOJENGWA MKOANI HUMO ZINAKAMILIKA KWA WAKATI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Manyanya akizungumza Wilayani Mpanda. Kushoto ni Mhe. Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Billal na Mke wake Mama Asha Billal.
Mkuuwa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya ameiomba Serikali kupitia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Billal kusaidia kuhakikisha ujenzi wa barabara za lami zinazoendelea kujengwa Mkoani Rukwa zinakamilika kwa wakati.
Mkuu huyo wa Mkoa alitoa ombi hilo jana mara baada ya kusomwa taarifa ya ujenzi wa barabara za lami zinazoendela kujengwa Mkoani humo kwa Mhe. Makamu wa Rais ambapo taarifa hiyo ilielezea changamoto zinazokabili ujenzi huo ambazo zinatishia kukamilika kwa ujenzi huo katika muda uliopangwa.
Taarifa hiyo iliyowasilishwa na Meneja wa Tanroads Mkoa wa Rukwa Ndugu Florian Kabaka jana iliweza kuainisha changamoto mbalimbali zinazoukabili ujenzi huo ikiwemo ucheleweshwaji wa malipo ya fedha kwa ile miradi inayotemea fedha za ndani hususani barabara za Sumbawanga-Kasanga na Sumbawanga-Mpanda.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo changamoto nyingine ni baadhi ya wakandarasi wanaojenga barabara hizo kukimbiwa na wafanyakazi wao kutokana na ukosefu wa fedha za kuwalipa hali inayopelekea kuzorota kwa ujenzi huo.
Mbali na changamoto hizo, nyingine ni kuchelewa kulipwa fidia wananchi waliothibitika kustahili malipo hayo ili kuepusha shughuli za ujenzi katika maeneo wanayotakiwa kuhama.
Pamoja na changamoto hizo nyingine ni wizi wa vifaa vya ujenzi wa barabara hizo zikiwepo nondo, mafuta, simenti, vyuma na hata mabati. Kwa mujibu wa Meneja huyo wa Tanroads ujenzi huo unatakiwa kukamilika mwakani 2013 lakini kama hali itaendelea kuwa hivyo basi huenda ukamilishaji wa miradi hiyo ukachelewa.
Baada ya kusomwa taarifa hiyo ilifika wakati kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kumkaribisha na kumtambulisha Mhe. Makamu wa Rais kwa wananchi wa Wilaya ya Nkasi ambapo amenza ziara akitokea Wilayani Mpanda. Kabla ya kufanya hivyo alilazimika kutumia fursa hiyo kutoa ombi lake rasmi kwa Makamu wa Rais kuhusu ujenzi unaondelea na kuhakikisha kuwa changamoto zinzozikabili barabara hizo zinapatiwa ufumbuzi.
"Wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa wanaishukuru sana Serikali yao kwa hatua yake kubwa ya kuleta miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara za lami Mkoani hapa kitu ambacho ni cha kujivunia kwa wanarukwa wote, Nitumie fursa hii kuiomba Serikali itusaidie kuondokana na changamoto zinazoikabili miradi hii ili iweze kuakamilika kwa wakati" Alisema Injinia Manyanya.
Serikali imesaini mikataba ya ujenzi wa barabara za lami Mkoani Rukwa kwa barabara za Tunduma-Ikana-Laela, laela-Sumbawanga, Sumbawanga-Kasanga na Sumbawanga-Mpanda. Hadi hivi sasa ujenzi wa barabara kwa baadhi ya maeneo hayo unaendelea na maeneo mengine yamesimama kwa muda kutokana na uhaba wa fedha.
Mhe. Makamu wa Rais yupo Mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi ya siku saba ambapo, ameshatembelea Wilaya ya Mpanda, Sasa yupo Wilayani Nkasi na baadae atamalizia ziara yake Wilayani Sumbawanga amabap atatembelea miradi mbalimbali ya maendeleo, kuizindua na kuweka mawe ya msingi. Ziara yake hiyo itakamilika tarehe 24 Februari 2012 ambapo ataenda Mkoa jirani wa Mbeya kwa ziara kama hiyo ya kikazi.

No comments:

Post a Comment