Wednesday, February 1, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AWAPASHA WAMILIKI WA VITUO VYA KULEA MAYATIMA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Manyanya (Mb) akikabidhi vyandarua arobaini na vifaa vingine kwa niaba ya Klabu ya Kimataifa ya Rotary (Rukwa) inayoshughulika na utoaji wa misaada mbalimbali katika jamii kwa watoto yatima wa kikundi cha Katandala Wilayani Sumbawanga Mkoani Rukwa. Anayepokea vyandarua hivyo ni Mlezi wa watoto hao Sister Helena Katebela na katikati ni Rais wa Klabu hiyo Mkoa wa Rukwa Ndugu Rainer Lukarah. Mkuu huyo wa Mkoa aliwaasa wamiliki wote wa vituo vya kulelea mayatima kufanya kazi zao kiuadilifu kwa kutotumia nafasi zao kujinufaisha wao wenyewe.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akimvesha gloves mtoto yatima Juma Kapera anayelelewa na kituo cha kulea mayatima cha Katandala Wilayani Sumbawanga. Gloves hizo pamoja na vifaa vingine ikiwemo vyandarua arobaini na vifaa vingine vya watoto vilitolewa na Klabu ya Kimatifa ya Rotary kupitia wanachama wake wa Rukwa. Siku za hivi karibuni Mtoto Juma alinusurika kuuwawa na watu wasiojulikana kwa imani za kishirikina baada ya kutekwa kwa muda wa wiki mbili na kupatikana akiwa ametelekezwa huku akiwa amechanjwachanjwa mwili mzima baada ya msako mkali wa Polisi.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa (katikati) akizungumza kwenye hafla ya kutoa msaada kwenye kituo cha kulea mayatima Katandala, kushoto ni Rais wa Rotary Club ya Sumbawanga Ndugu Rainer Lukarah na kulia ni Mwanachama wa Klabu hiyo ambaye pia ni Meneja Sido Mkoa wa Rukwa Ndugu Martin Augustino Chang'a.

Wanachama wa Klabu hiyo wakiwa wameshikilia zawadi walizotoa kwa kikundi hcho.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akiangalia watoto yatima waliozaliwa mapacha watatu ambao mama yao alikufa wiki moja baada ya kuwazaa kutokana na kuishiwa damu. Watoto hao wamezaliwa tarehe 13/01/2012 Wilayani Mpanda. Watoto hao wanajulikana kwa majina ya Isaak Bjukano, Leonard Bjukano, na Deborah Bjukano. Kutokana na hali hiyo Mkuu huyo wa Mkoa aliwaasa kinamama kutojifungulia majumbani kwani athari zake ni mbaya hivyo kuwashauri kinamama wote kujifungulia kwenye vituo vya afya au Zahanati

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Manyanya amewaasa wamiliki wote wa vituo vya kulelea mayatima wanaotumia nafasi zao kujinufaisha wenyewe kiuchumi kuacha tabia hiyo mara moja.
 Alisema hayo hivi karibuni wakati akikabidhi zawadi mbalimbali kwa niaba ya wanachama wa "Rotary Club International" Mkoa wa Rukwa kwa watoto yatima wa kituo cha Katandala Wilayani Sumbawanga.
Amesema kuwa sio vitendo vya kiuadilifu kutumia kivuli cha watoto yatima kufanya shughuli za kujinufaisha wao wenyewe. "Natoa wito kwa wale wote wanaofanya kazi hii kuwa na uadilifu na wasitumie nafasi hizo kujinufaisha wao wenyewe kimapato" Alsema Injinia Manyanya.
Katika salamu zake kwa walezi na watoto hao yatima aliwashukuru wanachama wenzake wa Rotary Club Sumbawanga kwa kuona umuhimu wa kuwatembelea watoto waliofiwa na wazazi wao pamoja na kuunga mkono juhudi za walezi hao.
Mkuu huyo wa Mkoa alitoa ahadi ya tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 5,000 ambalo thamani yake ni shilingi 1,800,000/= kwa kituo hicho cha Katandala. Zawadi nyingine zilizotolewa na Klabu hiyo ni pamoja na vyandarua 40 vya Mmbu, Mbuzi mmoja na Vifaa vingine kwa ajili ya watoto hao.
Klabu ya Rotary ni Klabu ya Kimataifa yenye wanachama duniani kote inayoshughulika na utoaji misaada kwa wanajamii waliopo katika mazingira magumu wakiwepo watoto mayatima na walemavu.   

No comments:

Post a Comment