Monday, February 6, 2012

SALAM ZA MKUU WA MKOA WA RUKWA SIKU YA SHERIA NCHINI ILIYOFANYIKA TAREHE 03 FEBRUARI 2012

Mheshimiwa Jaji Mfawidhi,
Mheshimiwa Jaji Pellagia B. Khaday,
Mheshimiwa Wakili Mfawidhi wa Mkoa,
Waheshimiwa Mahakimu wa ngazi zote,
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya,
Waheshimiwa Wabunge,
Waheshimiwa viongozi wa dini,
Waheshimiwa viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa,
Mabibi na Mabwana,
Itifaki imezingatiwa.
Mheshimiwa Jaji Mfawidhi,
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuweza kutulinda, kutupa afya na kufikia siku hii ya leo.
Pia napenda kuchukua nafasi hii ya kuwashukuru Mheshimiwa jaji Mfawidhi pamoja na Mahakama zako kwa kunipa nafasi hii ya kuwa mgeni rasmi katika sherehe hii muhimu ya Siku ya Sheria duniani leo tarehe 03/02/2012.
Mheshimiwa Jaji Mfawidhi,
Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaundwa na mihimili mitatu yaani Serikali, Bunge na Mahakama.  Mahakama ndio mhimili mkuu wenye jukumu kubwa la kutoa haki na wananchi wanalitambua hilo.  Mategemeo makubwa ya wananchi ni kuona kwamba suala hili la utoaji wa haki linatekelezwa vizuri na kwa usawa.
Mheshimiwa Jaji Mfawidhi,
Kama ulivyonifahamisha, maudhui ya maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini mwaka huu ni “ADHABU MBADALA KATIKA KESI ZA JINAI – FAIDA ZAKE KATIKA JAMII”.  Nami naungana na maudhui hii kusema kuwa endapo adhabu mbadala zitakazokuwa zinatolewa zitatekelezwa kikamilifu kwa kuzingatia uhalisia na matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii zetu basi hiyo inaweza ikawa na tija kuliko hata kutoa adhabu zilizozoeleka za kifungo jela.  Ni kweli jamii kubwa ya Watanzania haijawa na uelewa wa kutosha kuhusu adhabu mbadala katika kesi za jinai.  Hivyo ni wajibu wa Mahakama kwa kushirikiana na wadau wengine kama Serikali pamoja na Bunge kuendelea kuelimisha jamii zetu juu ya aina hii ya adhabu.
Mheshimiwa Jaji Mfawidhi,
Katika Miji yetu kuna kero mbalimbali ambazo zinahitaji nguvu kazi katika kuzirekebisha mfano; kufukua mitaro ya maji machafu, kupanda miti maeneo yenye upungufu wa miti, kufanya usafi, kusafisha masoko, n.k.  endapo wahalifu watatumika katika kurekebisha hali hiyo ikiwa ni sehemu ya kutumikia adhabu zao itakuwa na tija kwa Taifa kwani badala ya kutafuta pesa taslimu kwa ajili ya kulipia kazi hizo basi nguvu kazi ya wahalifu itaweza kuziba pengo hilo kwa muda ule wanaotakiwa kutumikia adhabu.  Hali kadhalika, adhabu ya aina hii inamuwezesha muhalifu kuendelea kuwajibika katika familia yake kama ambavyo mmeeleza wakati anapokuwa katika muda wake wa ziada.
Mheshimiwa Jaji Mfawidhi,
Kutumikia adhabu mbadala ni fursa kubwa kwa mhalifu huyo kwani anapata nafasi ya kuendelea na maisha yake mengine.  Lakini hiyo haimaanishi kuwa amesamehewa kabisa adhabu na ni vema kutambua kuwa adhabu iko kwa ajili ya mkosaji na hivyo sio sifa njema.  Kwa hiyo basi nashauri pale inapotokea mhalifu aliyepata adhabu ya aina hiyo kutotimiza wajibu wake ipasavyo endapo Mahakama itaona inafaa ni vema apewe adhabu nyingine kali ili kuwa fundisho kwake na kwa wenzake wanaotaka kudharau adhabu hiyo.
Mheshimiwa Jaji Mfawidhi,
Kwa kuwa pia sio rahisi kwa Mahakama kuotea kila wakati mahitaji ya nguvu kazi katika huduma za jamii zinazohitajika ni vema basi Halmashauri pamoja na Manispaa kutoa ushirikiano kwa kupeleka mahitaji mbalimbali ya kazi za kijamii katika  Mahakama husika, ili kuwezesha Mahakama kupata maeneo ya kutoa adhabu mbadala.
Mheshimiwa Jaji Mfawidhi,
Pamoja na umuhimu wa adhabu hii mbadala bado tunawaomba kuangalia kwa uzito mkubwa aina ya makosa.  Baadhi ya jamii kosa kama kumpiga au kumnyanyasa mke au mume haichukuliwi kama ni kosa kubwa bali ni mtindo wa maisha.  Hiyo imesababisha vitendo hivyo kuota mizizi na matokeo yake kufikia kusababisha hata vifo na kuongezeka kwa watoto wa mitaani au wanaoishi katika mazingira magumu.  Hivyo basi ili kukomesha vitendo hivyo ni vema watu ambao wanafanya unyanyasaji katika familia wapewe adhabu kali.
Mheshimiwa Jaji Mfawidhi,
Naomba niongelee kwa kifupi mambo makuu matatu ambayo ni vema pia mkayaongezea kasi:-
1.  Kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Magereza.
2.  Baadhi ya walalamikaji kutumia Mahakama kama fimbo ya kunyanyasa wenzao
3.  Kusogeza huduma karibu na wananchi.
1.  Kupunguza msongamano wa wafungwa na Mahabusu katika Magereza.
Kama mlivyonieleza, pamoja na jitihada mnazozifanya katika kushughulikia kesi, hali halisi inaonyesha kuwa bado kuna msongamano mkubwa katika magereza yetu. Mbaya zaidi watuhumiwa wanapokuwa katika magereza hayo hawaruhusiwi kufanya kazi badala yake Serikali inatumia gharama kubwa katika kuwahudumia. Hali hiyo inasababishwa na kesi kutosikilizwa na kutolewa maamuzi mapema hata kwa kesi ambazo pengine hazikuwa na ulazima wa kuchukua muda mrefu.  Hivyo basi nashauri kuongeza kasi ya kumaliza kesi hizo. Kwani kuna msemo ambao nausikia mara kwa mara hasa nikiwa Bungeni kwamba “haki inayocheleweshwa ni sawa na haki isiyokuwepo”.
2.  Baadhi ya walalamikaji kutumia Mahakama kama fimbo ya kunyanyasa wenzao
Katika ziara zangu nilizofanya vijijini wananchi wamenilalamikia kuwa baadhi yao huamua kufungua kesi zinazostahili kushughulikiwa katika mahakama za Mwanzo katika Mahakama za Manispaa ya Sumbawanga.  Hali hiyo hulazimisha watuhumiwa wasiokuwa na kipato cha kutosha kulazimika kusafiri kuja kusikiliza kesi zao Sumbawanga Mjini, wakati katika maeneo yao kuna Mahakama hizo.  Nashauri watu hao wasipewe mwanya wa kuleta usumbufu kwa wenzao usio wa lazima.  
3.  Kusogeza huduma karibu na wananchi
Ni dhamira ya Serikali kusogeza huduma karibu na wananchi. Sisi sote hapa ni mashaidi kwamba Wilaya ya Nkasi haina Mahakama ya Wilaya, hii inasababisha kesi zote za ngazi hiyo kushughulikiwa Sumbawanga jambo ambalo linaongeza msongamano katika Gereza la Sumbawanga, gharama kubwa za kusafirisha watuhumiwa hao kwani mara nyingi walalamikaji hugharimia wakati ule mtuhumiwa anapofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza baada ya hapo jukumu hilo linaachwa mikononi mwa Serikali.  Jambo ambalo ni kero kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Nkasi.  Ni vema Mahakama ikaliangalia hili kwa kina ili kuweza kusogeza huduma hii kwa wananchi.
Mheshimiwa Jaji Mfawidhi,
Hata hivyo ni jambo lisilopingika kwamba wakati mwingine Mahakama imekuwa na changamoto kubwa katika kutekeleza majukumu yake kama ilivyopanga kutokana na upungufu wa fedha, hiyo imetokana na Serikali kuwa na majukumu mengi ya kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi wake kama vile afya, maji na miundombinu. 
Pamoja na changamoto hizo Mahakama imejitahidi kwa kiwango kikubwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu, hivyo nawapongezeni sana.  Kwa kutambua hilo hivi karibuni Serikali imetunga sheria ya  mfuko maalum kwa ajili ya Mahakama.  Ni rai yangu kuona kuwa Mahakama inatengewa fedha za kutosha hususan katika Mkoa wangu wa Rukwa ili kuondoa kero mbalimbali zinazokwamisha kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwemo ujenzi wa nyumba za Majaji, Mahakimu na Wanasheria pamoja na majengo mengine ya Mahakama. 
Mheshimiwa Jaji Mfawidhi,
Ni imani yangu kwamba Sumbawanga itakuwa tulivu endapo mihimili yote mitatu itashirikiana katika kutimiza wajibu wake kwa wananchi ipasavyo.  Nami nipo tayari kutoa ushirikiano wangu kwenu wakati wowote.

Asanteni kwa kunisikiliza.
Mhandisi Stella Martin Manyanya (Mb)
MKUU WA MKOA WA RUKWA

No comments:

Post a Comment