Saturday, February 18, 2012

TAAARIFA YA MKOA WA RUKWA ILIYOSOMWA NA MKUU WA MKOA HUO KWA MAKAMU RAIS AMBAYE YUPO MKOANI HUMO KWA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU SABA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akisoma taarifa yake ya Mkoa kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Mohammed Gharib Billal katika ukumbi wa Ikulu Ndogo ya Mpanda mara baada ya kuwasili kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku saba Mkoani Rukwa.

Mhe. Makamu wa Rais akifuatilia hotuba hiyo mstari baada ya mstari.

TAARIFA YA MKUU WA MKOA WA RUKWA KWA MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MHE. DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL
KATIKA ZIARA YAKE MKOANI RUKWA
TAREHE 18 - 24 FEBRUARI, 2012.

Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
1.0.    UTANGULIZI.

Mheshimiwa Makamu wa Rais, Awali ya yote napenda kuchukuwa fursa hii kukukaribisha wewe na ujumbe wako hapa Mkoani Rukwa. Sisi wananchi wa Mkoa wa Rukwa tunafarijika sana pindi tunapotembelewa na viongozi wa Kitaifa kwani tunajua wazi tutapata ushauri, maelekezo na maagizo kwa ajili ya kuboresha utendaji wetu wa kazi.

Mheshimiwa Makamu wa Rais, Taarifa hii inazungumzia habari za Mkoa wa Rukwa ambao ni pamoja na Mkoa mpya wa Katavi. Inaonyesha ulipo mkoa na umbile lake . Aidha, tunaelezea mafanikio na changamoto zilizomo katika sekta mbalimbali  ikiwemo Elimu, Afya, maji, Kilimo, Ushirika, Uvuvi, Ardhi, Maendeleo ya jamii, Biashara, Viwanda, Miundombinu, Mawasiliano na Masuala mtambuka. Pia  hatukusahau  masuala ya Haki za Binadamu na Utawala bora.

2.0.    HALI YA ULINZI NA USALAMA.

Mheshimiwa Makamu wa Rais,
Kwa ujumla hali ya Ulinzi na Usalama katika Mkoa ni shwari na ya kuridhisha kwa kiasi kikubwa.  Matukio machache ya uhalifu yanayojitokeza yameendelea kushughulikiwa na kudhibitiwa na Kamati za Ulinzi na Usalama za kila Wilaya kwa kushirikiana na kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa.

Kwa upande wa Kisiasa viko vyama tisa (9) vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, Chama Cha Mapinduzi - Chama Tawala ndiyo chama chenye nguvu katika Mkoa wa Rukwa. Kati ya Waheshimiwa Wabunge 12, 10 wanatoka Chama Cha Mapinduzi na wawili wanatoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA. Kati ya Wahe. Madiwani 106 wa kuchaguliwa, 92 wanatoka Chama Cha Mapinduzi, 12 kutoka CHADEMA, mmoja kutoka DP na mmoja kutoka TLP.

3.0. MAANDALIZI YA MAENEO MAPYA.
Mheshimiwa Makamu wa Rais,
Mkoa umejiandaa kupokea maeneo mapya ya Utawala ambayo ni Mkoa mpya wa Katavi na Wilaya mpya za Mlele na Kalambo.

Mkoa ulishatambua Ofisi utakapoanzia Mkoa mpya wa Katavi na makazi ya Viongozi wa ngazi ya Mkoa. Pia tumeainisha Watumishi watakao kwenda kuanzisha maeneo hayo mapya ya kiutawala.

Changamoto
Tuna changamoto ya upungufu wa vitendea kazi, magari na samani za ofisi. Hatuna magari ya kwenda kuanzishia maeneo hayo. Nyumba na Ofisi zitakapoanzia Wilaya zetu mpya pia zinahitaji ukarabati.

4.0.    ELIMU
4.1.  ELIMU YA AWALI
Mhe. Makamu wa Rais,
Mkoa wa Rukwa kwa mwaka huu 2012 ulilenga kuandikisha wanafunzi 46,707 hadi sasa wanafunzi 27,385 wameandikishwa wakiwemo wavulana 14,675 na wasichana 12,710. wenye umri wa miaka 5 na 6

4.2  ELIMU YA MSINGI
Mhe. Makamu wa Rais,
Mkoa wa Rukwa umeweza kuandikisha wanafunzi 35,108 sawa na asilimia 73.93  kuanza darasa la kwanza 2012 wakiwemo wavulana 17,716 na wasichana 17,392 kutoka katika lengo la kuandikisha wanafunzi 47,482 hata hivyo zoezi la uandikishaji linaendelea.

4.2.1 MTIHANI WA KUMALIZA ELIMU YA MSINGI 2011
Jumla ya watahiniwa 28,551 kati yao wavulana 13781 na wasichana 14770 walifanya mtihani kati ya watahiniwa 30,070 waliosajiliwa ikiwa ni asilimia 94.69. Kati ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi mwaka 2011, vijana 14,612 walifaulu kuingia kidato cha kwanza mwaka 2012 kati yao 8,221 ni wavulana na 6,391 ni wasichana. Ufaulu huu ni sawa na asilimia 51.07 ya watoto waliofanya mtihani.

4.3.  ELIMU YA SEKONDARI.
Mhe. Makamu wa Rais,
Mkoa una jumla ya shule za Sekondari 114 zikiwemo 99 za Serikali na 15 zikiwa ni za watu binafsi na mashirika ya dini. Shule zenye kidato cha V-VI zipo 12 ambapo nane (8) za Serikali na nne (4) zisizo za Serikali.
   
Mwaka 2011 jumla ya wanafunzi 7,467 wakiwemo wavulana 4,624 na  wasichana 2,843 wamefanya mtihani wa  kuhitimu kidato cha nne. Aidha, jumla ya wanafunzi 8,649 wa kidato cha pili wakiwemo wavulana 5,057 na wasichana 3,592 walifanya mtihani mwaka 2011.

4.4.  ELIMU YA UALIMU.
Mhe. Makamu wa Rais, Mkoa una chuo kimoja cha Ualimu cha Serikali kiitwacho Sumbawanga kinachotoa mafunzo ya ualimu ngazi ya cheti daraja la IIIA na mafunzo ya cheti cha Sayansi Kimu.  Pia Mkoa una vyuo viwili binafsi vya Ualimu vinavyotoa mafunzo ya ualimu daraja la IIIA vyote vikiwa vimepata  usajili na hivyo Mkoa kuwa na vyuo vitatu vya mafunzo ya ualimu,  vyuo hivi vimesajiliwa kwa jina la Rukwa Chuo cha Ualimu na St. Aggrey Chanji.

4.5.  ELIMU YA UFUNDI
Mhe. Makamu wa Rais, Mkoa una Chuo kimoja cha VETA kilichoko wilayani Mpanda na vituo vya ufundi stadi sita (6) katika fani za Useremala, Uashi na Sayansi Kimu. Aidha, vipo vyuo vya ufundi vitatu (3) katika fani za Ufundi Magari, Uchomeleaji na Kompyuta.

4.6.  ELIMU YA WATU WAZIMA (EWW)
Mhe. Makamu wa Rais, Mkoa una madarasa ya KCK yapatayo 357 na wanakisomo wapo hatua mbalimbali.

4.7.  UKAGUZI WA SHULE
Mhe. Makamu wa Rais,
Halmashauri za Wilaya zimekuwa zikisaidia ili Wakaguzi wa shule waweze kukagua shule. Katika kipindi cha Januari - Desemba 2011 shule za msingi 103 zilikaguliwa.

4.8.  ELIMU YA JUU
Mhe. Makamu wa Rais, Mkoa unacho Kituo cha Chuo Kikuu Huria chenye jumla ya wanachuo 150 katika kozi mbalimbali.  Katika kipindi cha mwaka 2009 hadi 2011 jumla ya wanachuo 57 wamefuzu na kutunukiwa vyeti katika fani mbalimbali.

4.9   CHANGAMOTO
Mhe. Makamu wa Rais, Zipo changamoto ambazo zinaikabili sekta ya Elimu mkoani Rukwa ni:-
·              Upungufu wa hosteli/daharia katika shule za sekondari
·              Mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari
·              Ushiriki hafifu wa wananchi katika kuchangia utekelezaji wa MMEM na MMES

4.10 MATARAJIO YA BAADAYE:
·              Kuboresha taaluma kuanzia shule za awali, msingi, sekondari na vyuo ili kukidhi ushindani wa kielimu katika soko la kimataifa

5.0   SEKTA YA AFYA
Mheshimiwa Makamu wa Rais,
Sekta ya Afya Mkoani ina umuhimu mkubwa katika kuhakikisha utengano wa Afya na maisha ya wana Rukwa.

5.1. CHANGAMOTO

Sekta ya Afya mkoani inakabiliwa na changamoto zifuatazo:
-          Uhaba wa watumishi kutokana na watumishi wanaopangiwa kuja mkoa wa Rukwa kutoripoti katika vituo vyao vya kazi
-          Upatikanaji wa madawa na vifaa kwa wakati kutoka bohari kuu ya madawa (MSD)
-          Bado kuna maeneo magumu kufikika hasa mwambao wa ziwa Tanganyika

6.0. SEKTA YA MAJI
Mheshimiwa Makamu wa Rais
Kiwango cha usambazaji maji safi na salama katika Mkoa wa Rukwa ni asilimia 50 tu.  Jitihada zinafanyika kuhakikisha kuwa usambazaji unakidhi mahitaji ya watumiaji ifikapo 2025 kulingana na dira ya maendeleo.

6.1. MAJI VIJIJINI
Mipango ya Maendeleo ya Uboreshaji wa upatikanaji na usambazaji wa majisafi na salama ili kuhakikisha kiwango cha huduma ya maji kinapanda kwa kila Halmashauri inafanywa kupitia program ndogo ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kupitia mradi unaojulikana kama Mradi wa Vijiji Kumi. Jumla ya Visima 22 vimechimbwa katika maeneo mbalimbali yaliyotambuliwa kwa mradi huo.

6.2. MAJI MJINI
Mji wa Sumbawanga kwa kutekeleza Miradi miwili yenye kuleta mafanikio ya haraka. Hadi sasa visima 13 vimechimbwa ambapo visima 8 vina maji na vinaweza kutoa jumla ya lita 4,000,000 kwa siku.

6.3. CHANGAMOTO
Sekta ya maji inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kudumisha Huduma ya Maji katika Mkoa wetu. Changamoto hizi ni:
Ø  Uharibifu wa mazingira hasa kuchoma moto misitu kunakosababisha kukauka kwa vyanzo vya maji,
Ø  Wizi wa miundombinu ya maji, bomba na mifuniko ya chemba za maji,

7.0.  UWEZESHAJI WA KIUCHUMI.
Mheshimiwa Makamu wa Rais,
Mkoa unawezesha jamii kiuchumi  katika juhudi za kuondokana na umaskini wa kipato kwa  kutoa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali kwa vijana na wanawake kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF). Mafunzo ya ujasiriamali yametolewa kwa vikundi 797 na jumla ya vikundi vya Akinamama vipatavyo 806 ambavyo vimepatiwa mikopo yenye thamani ya Sh. 255,750,000/= kati ya hizo fedha zilizorudishwa na Sh. 78,191,250/= na ufatiliaji unaendelea.

7.1.  UANZISHAJI WA VICOBA
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Vikundi vya VICOBA vya vijana na akinamama, vimeundwa, mafunzo ya ujasiriamali wa biashara ndogo ndogo, ufundi na usindikaji wa mazao yametolewa kwa wajasiriamali 195 .

7.2.  UWEZESHAJI WA MAKUNDI YA KIJAMII
Idadi ya wanawake wanaojiendeleza kielimu kuanzia Elimu ya awali hadi Vyuo Vikuu imeongezeka na kufikia wanawake 169,088  mwaka 2011.

7.3.  HUDUMA KWA MAKUNDI YENYE UHITAJI.
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mkoa umetoa misaada yenye thamani ya Sh.22,959,100/= kupiti NMSF Grant kwa makundi mbalimbali yenye uhitaji kama Watoto Yatima wajane, wazee na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wapatao 708. Mkoa umewatambua walemavu wa ngozi (Albino) wanawake 448 na wanaume 349, jumla 797. Vile vile, Mkoa una vituo vinne (4) vya kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi: Manispaa ya Sumbawanga vituo viwili (2), Halmashauri ya Wilaya Sumbawanga kituo kimoja (1) na Nkasi kituo kimoja (1):

7.4.  MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI:
Mkoa una vituo 85 vya ushauri nasaha na kupima kwa hiari (VCT). Jumla ya watu 240,000 wamejitokeza kupima VVU/UKIMWI kwa hiari. Pia Mkoa una vituo 91 vya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Mapambano dhidi ya UKIMWI mahali pa kazi yameimarishwa, mafunzo na misaada kwa wanaoshi na VVU/UKIMWI yametolewa yenye thamani ya Sh.23,588,150/=.

8.0.    KILIMO
8.1.    KILIMO CHA MAZAO
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Katika msimu wa kilimo wa Mwaka  2010/2011 Mkoa ulilima  jumla ya hekta 614,087 za mazao ya chakula na hekta 122, 627 za mazao ya biashara. Uzalishalishaji ulikuwa tani  2,136, 545 za mazao ya chakula na tani 161,637 za mazao ya biashara. Hii ni sawa na ongezeko la tani 166,672 (8.5%) za mazao ya chakula ukilinganisha na msimu uliopita.

Katika msimu huu wa kilimo wa 2011/2012 Mkoa umelenga kulima jumla ya hekta 679,300 za mazao ya chakula na matarajio yetu ni kuvuna jumla ya tani 2,518,270 mazao ya biashara tunalenga kulima jumla  ya hekta 133,282 na matarajio ya kuvuna ni tani 368,733.8. Katika kufanikisha adhima hiyo mwaka 2011/2012 Mkoa umepangiwa jumla ya Sh. bilioni 2.7 za miradi ya uwekezaji katika kilimo nje ya miradi ya umwagiliaji kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Sekta ya Kilimo katika Mkoa.
8.2      PEMBEJEO ZA KILIMO. 
Katika Msimu wa kilimo wa 2011/2012 Mkoa umepangiwa kuhudumia kaya 146,000 ambazo ni sawa na ekari 146,000 za mahindi. Mkoa umepokea jumla ya vocha  438,000 za pembejeo za kilimo toka  Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na  kuzisambaza katika Halmashauri zote za mkoa. Vocha hizo ni za ruzuku ya mbolea ya kupandia, kukuzia na mbegu chotara za mahindi. Vilevile, idadi hiyo ya vocha inajumuisha vocha za mbegu chotara za Mpunga kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. 

8.3. CHANGAMOTO.
Katika kutekeleza  mfumo wa ruzuku ya pembejeo za kilimo mkoa ulikabiliana  na changamoto zifuatazo:-
(i)        Bei za pembejeo kuwa juu tofauti na ilivyotegemewa na kufanya baadhi ya wakulima  walengwa kushindwa kuchangia tofauti ya bei.
Uwezo mdogo wa wakulima kuchangia gharama za seti nzima  zinazofikia  Sh. 125,500/= hadi 133,000/=, hivyo kuchagua aina  moja ya pembejeo mfano, mbegu tu au mbolea ya kukuzia. Hali hii itafanya malengo ya uzalishaji (tija) yasifikiwe.

8.4.  KILIMO CHA UMWAGILIAJI.
Mheshimiwa Makamu wa Rais,
Mkoa wa Rukwa una jumla ya Hekta 995,700 zenye uwezo wa kumwagiliwa. Kati ya eneo hilo hekta 27,000 zina uwezo wa juu, hekta 79,800 zina uwezo wa kati na hekta 888,900 uwezo wake ni wa chini. Kwa sasa eneo linalomwagiliwa ni  hekta 27,136 sawa na 25.4% ya eneo lenye uwezo wa juu na kati wa kumwagiliwa.

8.4.1. CHANGAMOTO ZA KILIMO CHA UMWAGILIAJI:
Katika utekelezaji wa shughuli za Umwagiliaji mkoa unakabiliwa na changamoto zifuatazo;
 1. Upungufu wa wataalamu na vitendea kazi, katika ngazi ya Halmashauri za Wilaya.
 2. Elimu ndogo kwa wakulima juu ya  kuzingatia matumizi bora ya maji, utunzaji bora wa mimea na matumizi bora ya zana za kilimo katika skimu za umwagiliaji.

8.4.2.      MKOA UMEJIPANGA KUTATUA CHANGAMOTO HIZO KWA:
Kuzielekeza Halmashauri zote za Mkoa kuajiri wataalam wa umwagiliaji, Mhandisi umwagiliaji, na Mpimaji, pia Mkoa unaendelea kutoa elimu kwa wakandarasi waliopo mkoani  wenye uwezo wa kujenga miundombinu ya umwagiliaji wafanye kazi hizo.

8.5.  MATUMIZI  YA ZANA ZA  KILIMO:
Matumizi ya wanyamakazi (maksai) kwa mwaka 2010/2011 ni asilimia 70%.Mkoa wa Rukwa Una jumla ya trekta kubwa 102 na matrekta madogo 225 .Mwaka 2010/2011 hekta 75,260.8 zimelimwa kwa kutumia trekta kubwa na hekta 45,810.4 kwa kutumia matrekta madogo.

8.5.    UNUNUZI WA MAHINDI MSIMU WA 2011/2012
         KUPITIA  NFRA:
Uzalishaji wa zao la mahindi umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka. Katika msimu wa 2010/2011 tulizalisha jumla ya tani 830,591 za mahindi. Mahitaji ya Mkoa ya mahindi ni tani 336,572 hivyo tulikuwa na ziada ya tani 494,019  za mahindi.
Mnunuzi mkuu wa zao la mahindi katika Mkoa wetu ni Wakala wa Taifa  wa Hifadhi ya Chakula-NFRA alinunua mahindi kwa  bei ya Sh. 350 kwa kilo.Hadi ununuzi ulipositishwa Mkoa kupitia NFRA ulikuwa umenunua  jumla ya tani 50,626.923 katika vituo vyote 15 vilivyofunguliwa kuanzia tarehe 2/08/2011 yenye thamani ya Sh. 17,719,423,050. Fedha hizo zimelipwa kwa wakulima wa mkoa wa Rukwa.

8.6.1.  CHANGAMOTO.
i.        Uhaba wa maghala.
Mpaka sasa NFRA wana akiba ya tani 55,000. katika maghala yake. Ili kupunguza tatizo hili NFRA watajenga Vituo vya  kuhifadhi mahindi  katika Mji wa Mpanda  na katika baadhi ya vijiji mkoani ikiwemo bonde la ziwa Rukwa.

8.6.2. UUZAJI WA MAZAO NJE YA MKOA/NCHI:
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mkoa umepokea maombi ya kupeleka mazao nchi za Burundi, Rwanda, Kenya na Mkoa wa Kigoma yenye jumla ya tani 7,070. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imetoa vibali viwili vyenye jumla ya tani 1,750 kwa ajili ya usafirishaji wa mahindi kwenda Burundi.

9.0    MIFUGO
9.1 RASILIMALI ZA UFUGAJI
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Kulingana na Sensa ya Kilimo ya 2003, asilimia 34 ya wananchi wa vijijini wa Mkoa wa Rukwa hujishughulisha na ufugaji. Hivyo ufugaji ni shughuli ya pili kwa umuhimu kiuchumi baada ya kilimo cha mazao.
Na.
Mfugo
Idadi
1
Ng’ombe
733,557
2
Mbuzi
291,636
3
Kondoo
65,479
4
Nguruwe
65,240
5
Kuku
954,128
6
Punda
6,543


9.2.  MIKAKATI YA SEKTA
Mheshimiwa Makamu wa Rais,
Mwaka wa 2008 Mkoa wa Rukwa ulibuni na kupitisha Mkakati wa Maendeleo ya Kilimo Rukwa; MAKIRU (MAPINDUZI YA KILIMO RUKWA) kama nyenzo ya kutafsiri, kupanga, na kutekeleza mazingira na fursa zilizopo katika mkoa. Baadhi ya mikakati ya MAKIRU inayohitaji kupewa kipaumbele katika sekta ya mifugo ni ile inayohusu matumizi ya ardhi na maeneo ya kuwekeza raslimali za kitaifa ambayo ni pamoja na:
(i)           Kuandaa na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi ili shughuli za ufugaji ziweze kufanyika katika maeneo yanayofahamika na kulindwa kisheria.
(ii)        Kuendeleza mifugo inayomilikiwa na wananchi walio wengi: kuku wa asili na ng’ombe wa nyama wa asili.

9.3.  CHANGAMOTO ZA SEKTA       
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mkoa unakabiliana na changamoto mbalimbali katika kuendeleza sekta ya ufugaji. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na:-
i)             Migogoro ya matumizi ya ardhi.
ii)            Uhamiaji wa wafugaji na makundi ya mifugo usiofuata taratibu.
10.0.          USHIRIKA.
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Hadi kufikia mwezi Desemba, 2011 Mkoa una jumla ya Vyama vya Ushirika 132 zikiwemo SACCOS 107 zenye jumla ya Wanachama 13,978 na Hisa za jumla ya Sh.334,179,000 akiba za Sh.1,882,955,000 na amana zenye thamani ya  Sh.55,969,000 hivyo kufanya jumla ya mtaji wenye thamani ya Sh.2,273,103,000.

11.0 UVUVI.
Kutokana na sensa ya mwaka 1999 uzalishaji wa samaki toka Ziwa Rukwa unakadiriwa kuwa ni tani 7,000 na Ziwa Tanganyika linakadiriwa kuzalisha samaki kiasi cha tani 165,000 hadi tani 200,000 kwa mwaka wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 80 hadi milioni 100.

Kuna aina mbali mbali ya samaki wanaopatikana katika maziwa na mito iliyopo katika Mkoa wetu. Ziwa Tanganyika linatupatia samaki aina ya dagaa, migebuka, sangara, kuhe, kambale na samaki wa mapambo. Ziwa Rukwa linatupatia kambale, gege na mamba. Dagaa na migebuka wanaopatikana ziwa Tanganyina  na gege toka ziwa Rukwa mara nyingi hukaushwa na kupelekwa kuuzwa kweye masoko makubwa ndani na nje ya nchi mfano Zambia, Kongo na Burundi.

11.1. CHANGAMOTO.
 1. Ukosefu wa nishati ya umeme kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika .
 2. Ukosefu wa zana bora za uvuvi kwa wavuvi.
12.0 SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Katika sekta hii kuna viwanda vidogo na vya kati vinavyoendeshwa, Viwanda hivyo vinajihusisha na shughuli za  usindikaji wa nafaka, samaki, nyama utengenezaji wa sabuni. Hadi sasa Mkoa una Viwanda saba ambavyo ni:- SAAFI Co.LTD, Tropical grain Co.LTD, Fantashiru Milling, Ikuwo Enterprises, Energy Milling.Co.Ltd, Migebuka Premium (Premji), Njema Soap Co. LTD. MPADECO

12.1.  BIASHARA
i.         Mkoa unaendelea kuhakikisha kuwa unawakwamua wananchi wake kiuchumi. Katika jitihada hizo maafisa biashara wamekuwa wakitoa elimu na ushauri kwa wajasiriamali juu ya kuendesha biashara zao kwa mafanikio na uboreshaji wa vifungashio kwa wasindikaji ili kuwavutia wateja. Shirika la kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO) imekuwa mstari wa mbele katika kuiendeleza sekta ya biashara.

12.2.        BEI ZA VYAKULA NA BIDHAA MBALIMBALI
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Tokea tupate agizo la kuangalia mwenendo wa bei hapa Mkoani hadi kufikia tarehe 20.01.2012 bei zimekuwa kama ifuatavyo:-
Vyakula:
i.         Bei ya rejareja kwa kilo moja ya Sukari ni kati ya Sh.2,000 hadi 2300.
ii.       Mafuta ya kula lita 10 ni Sh.30,000  sawa na Sh.3,000 kwa lita
iii.      Unga wa Sembe kilo moja inauzwa kwa Sh.700/-
iv.    Mchele unauzwa Sh.1,400 hadi Sh.1,700 kwa kilo.

Bidhaa nyingine   bei  zake ni kama ifuatavyo:- Petrol   lita moja Sh.2,262 /=, Diesel  lita moja Sh.2,248/=, Mafuta ya taa, lita moja Sh.2,221/=, Gesi  kilo 15  ni Sh. 57,000/= na  Saruji mfuko wa kilo 50 unauzwa  kwa shilingi hadi 21,000/=.

12.3. CHANGAMOTO ZILIZOPO;
·         Ubovu wa miundombinu
·         Ukosefu wa nishati kwa baadhi ya maeneo
·         Upungufu wa malighafi kwa baadhi ya viwanda i.e SAAFI

13.0  MALIASILI NA MAZINGIRA
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mkoa wa Rukwa una fursa nyingi za maliasili (utalii, misitu na ardhi) ambazo bado hazijatumiwa kikamilifu kama Maporomoko ya mto Kalambo yenye mita 235, wanyama waliopo katika mapori tengefu na mbuga ya wanyama ya Katavi, mbega wekundu waliopo katika msitu wa hifadhi wa Mbizi. Uwepo wa makaa ya mawe, uwepo wa ziwa Tanganyika na Rukwa pamoja na mito midogo midogo mingi. Katika kutekeleza sera ya Taifa  na sheria ya Mazingira, Mkoa umeendelea kuhamasisha wananchi katika kuhifadhi Mazingira kwa njia mbalimbali zikiwemo za upandaji miti na utoaji elimu ya  mazingira.

13.1. HIFADHI YA MAZINGIRA
 (i)       UPANDAJI MITI;
Jumla ya miti 4,099,613 imeoteshwa maeneo mbalimbali katika Mkoa wetu wa Rukwa mwaka 2010/2011.
(ii)      MATUMIZI BORA ARDHI
Jumla ya vijiji 70, vimeshatekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi ( Land Use Plan) kati ya vijiji 387 vilivyopimwa.

(iii)     ELIMU YA MAZINGIRA;
Elimu hii inatolewa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wakiwemo Mradi wa Hifadhi ya Mazingira ya ziwa Tanganyika, mradi uliopo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais Divisheni ya Mazingira,  Taasisi ya kuhifadhi wanyama iliyopo Mbeya  (WCS- Wildlife Conservation Society), REYO - Rukwa Environment Youth Organization, KAESO, ADAP - Association for Development for Areas Protected,  REDESO, GMU n.k,

13.2.        MRADI WA HIFADHI YA ZIWA TANGANYIKA
Katika Mkoa wa Rukwa, Programu hii inatekeleza miradi miwili kama ifuatayo:-
i.         Mradi wa usimamizi wa Bonde (catchments management)
ii.       Mradi wa uendelezaji wa Uvuvi na Hifadhi ya Mazingira ya ziwa Tanganyika.
Mambo ambayo yanapelekea kuandaa mkakati wa kuhifadhi ziwa Tanganyika yanatokana na tatizo la;-
Uchafuzi wa ziwa (environmental pollusion)
 1. Kuongezeka kwa tabaka la udongo (sedmentation)
 2. Uharibifu wa makazi ya viumbe ( destruction of breeding site)
 3. Uvuvi usio endelevu ( unsustainable fisheries)

13.3.        MISITU NA NYUKI
§  Mkoa umekusanya Shs. 201,559,099/= kutokana na ushuru utokanao na mazao ya misitu na ukataji wa leseni za biashara ya mzao ya misitu.
§  Jumla ya vijiji sita (6) vimepewa elimu ya ufugaji bora wa nyuki

13.4.        WANYAMAPORI
§  Usimamizi na uwindaji wa kitalii katika vitalu vya Lwafi, Msima, Nkamba, Mto Rungwa, Shama na Mlele umefanyika na kupatikana US$ 723,010 ambapo Halmashauri inategemea kupata 25% ya pesa hizo.
§  Usimamiaji wa uanzishaji wa “Wildlife Management Area (WMA)” utaowanufaisha wakazi waishio maeneo ya kando kando ya hifadhi  za wanyama kwani watanufaika na mapato yatokanayo na uwindaji, ambapo vijiji 2 vinavyounda CBOs ya UBENDE ndivyo vinavyonufaika na mpango huu.
13.5.        CHANGAMOTO;
·         Uelewa mdogo wa wananchi dhidi ya hifadhi ya mazingira.
·         Ukataji wa miti holela kwa ajili ya nishati ya kuni, mkaa, ujenzi na upanuzi wa mashamba, Uchungaji holela wa mifugo na wa kuhamahama na uchomaji moto ovyo.
13.6. MIKAKATI;
·         Kuwashirikisha wananchi wakati wa kuibua miradi ya maendeleo inayohusisha masuala ya mazingira, mfano mradi wa utengenezaji wa sabuni.
·         Kuendelea kuzijengea uwezo kamati za mazingira za vijiji ( VNRC)

14.0. MIUNDOMBINU
14.1. SEKTA YA BARABARA

Mheshimiwa Makamu wa Rais,

14.2. MATENGENEZO YA BARABARA KUU
Hadi kufikia tarehe 30 Desemba 2011, kazi za matengenezo ya barabara kuu zilizopangwa kufanyika katika mwaka wa fedha wa 2010/2011 zilikuwa zimekamilika ambapo km 417.7,madaraja 27 yalijengwa kwa gharama ya sh. millioni 3,289.

14.3.MIRADI YA MAENDELEO YA BARABARA
       
14.4. UKARABATI NA MATENGENEZO KUPITIA MPANGO WA PMMR (Performance–Based Management and Maintenance of Roads)

Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mradi wa PMMR kwa sasa unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 ambayo mikataba iliyopo ni ya Miaka Mitano. Katika kipindi cha 2010/2011 kiasi cha Km 272.3 za barabra zimekarabatiwa ambapo zimeigharimu Serikali Sh. 8, 953, 336,569

14.4.1.  UKARABATI/UJENZI KWA KUTUMIA FEDHA ZA NDANI (BAJETI YA MAENDELEO)

Mheshimiwa Makamu wa Rais, Katika mwaka wa fedha wa 2010/2011 tulitarajia kutengeneza km 101, barabara hizi zimekamilika kwa kutumia Sh. millioni 3,014,797.

14.5. UJENZI WA BARABARA KWA KIWANGO CHA LAMI

14.6.1 BARABARA YA SUMBAWANGA -LAELA- TUNDUMA (223.21KM)

14.6.2. SEHEMU YA SUMBAWANGA - LAELA (95.31 KM)

Eneo hili linajegwa na Kampuni ya Aarsleff-BAM International Joint Venture V.O.F kutoka Denmark na Uholanzi kwa gharama ya USD 97 Milioni chini ya mhandisi mshauri Egis BCEOM International kutoka Ufaransa.

Maendeleo ya jumla ya mradi hadi kufikia tarehe 20 Januari, 2012 yalikuwa yamefikia 21.9% ya kazi zote zilizopangwa. Kwa ujumla mradi unaendelea vizuri.
         
14.6.3.  SEHEMU YA LAELA - IKANA (64.2 KM)
Eneo hili linajegwa na Kampuni ya China New Era International Engineering Corporation kutoka China kwa gharama ya Sh. bilioni 76.1 chini ya Mhandisi Mshauri Egis BCEOM International kutoka Ufaransa.

Maendeleo ya jumla ya mradi 20 Januari, 2012 yalikuwa yamefikia (27.7%)ya kazi zote zilizopangwa. Kwa ujumla mradi unaendelea vizuri.

14.6.4.  SEHEMU YA  IKANA - TUNDUMA (63.7 KM)
Eneo hili linajegwa na Kampuni ya Consolidated Contractors Group S.A (offshore) (CCC) kutoka Ugiriki chini ya Mhandisi Mshauri Egis BCEOM International kutoka Ufaransa kwa gharama ya Sh. billion 82.5. Maendeleo ya jumla ya mradi hadi sasa yamefikia (18.4%) ya kazi zote zilizopangwa. Kwa ujumla mradi unaendelea vizuri.

14.7.0.SUMBAWANGA-NAMANYERE-MPANDA/KIZI-KIBAONI
            (274 KM)
14.7.1.  SEHEMU YA SUMBAWANGA-KANAZI (75 KM)
Eneo hili linajegwa na Kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering (Group) Corporation kutoka China chini ya Mhandisi Mshauri Nicholas O’Dwyer and Company Limited kutoka Ireland akishirikana na Apex Engineering Ltd kutoka Tanzania kwa  gharama ya Sh. bilioni 78.8.
         
Maendeleo ya jumla ya mradi hadi kufikia tarehe 20 Januari, 2012 yalikuwa (17.1%) ya kazi zote zilizopangwa. Kuchelewa kwa malipo ya Mkandarasi kumeathiri kasi ya utekelezaji wa mradi, ambapo mradi huu unategemewa kukamilika tarehe 15 Desemba, 2012.

14.7.2.   SEHEMU YA KANAZI-KIZI-KIBAONI (76.6 KM)
Eneo hili linajegwa na Kampuni ya China Hunan Construction Engineering Group  Corporation kutoka China, chini ya Mhandisi Mshauri Nicholas O’Dwyer and Company Limited kutoka Ireland akishirikiana na Apex Engineering Ltd kutoka Tanzania, kwa gharama ya Sh.82.84 bilioni. 
        
Maendeleo ya jumla ya mradi hadi kufikia 20 Januari, 2012 yalikuwa 25% ya kazi zote zilizopangwa. Mkandarasi anaendelea vizuri ingawa kuchelewa kwa malipo ya Mkandarasi kumeathiri kasi ya utekelezaji wa mradi.Na mradi huu unategemewa kukamilika tarehe 15 Desemba,2012 Changamoto kubwa katika mradi huu ni ukosefu wa fedha za kumlipa Mkandarasi kwa wakati.

14.8.0.  SUMBAWANGA-MATAI-KASANGA PORT (112KM)
Eneo hili linajegwa na Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation (CR15G)/   Newcentry Company Ltd chini ya Mhandisi Mshauri Nicholas O’Dwyer and Company Limited kutoka Ireland akishirikiana na Apex Engineering Ltd kutoka Tanzania. Gharama  ya Mradi ni Sh.133.3 billion.

Maendeleo ya jumla ya mradi hadi kufikia tarehe 20 Januari 2012 yalikuwa  11% ya kazi zote zilizopangwa. Mradi huu unatekelezwa kwa mkataba wa Usanifu na Ujenzi (Design and Build Contract). Usanifu wa kina wa kilometa 70 za kwanza umekamilika na Mkandarasi ameruhusiwa kuanza kazi katika kilometa 60 za kwanza.  Usanifu wa kilometa 42 zilizobaki unaendelea.

14.9.0.  MIRADI YA UPEMBUZI YAKINIFU NA USANIFU WA KINA
Miradi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika Mkoa ni:-

i).       Barabara ya Sumbawanga-Namanyere-Mpanda: Sehemu 
          ya Kizi-Sitalike -Mpanda (123 km)
ii).      Barabara ya Mpanda-Uvinza (185 km)
iii).     Barabara ya Mpanda-Inyonga-Koga (193 km)
iv).     Barabara ya Matai-Kasesya (47 km)


14.9.0. CHANGAMOTO

Mheshimiwa Makamu wa Rais, Tunakabiliwa na changamoto mbalimbali  kama ifuatavyo:
(i)           Uhaba wa mitambo ya matengenezo na ujenzi wa barabara pamoja na Magari kwa Wakandarasi na hata Wakala (TANROAD)
(ii)          Ugumu wa makandarasi kupata dhamana (bonds/guarantees) kutoka katika vyombo vya fedha na hivyo kuchelewa kuanza kazi.

15.0.        VIWANJA VYA NDEGE

15.1. KIWANJA CHA NDEGE CHA MPANDA

Kiwanja hiki kinajengwa kwa pamoja kati ya  Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi (UNHCR) kwa jumla Sh. bilioni 30.  Serikali ya Tanzania itagharamia Sh. bilioni 28.3 na Shirika la Umoja wa Mataifa Sh. bilioni 1.7.

Mradi wa kiwanja  unajumuisha shughuli zifuatazo:-
·         Kukarabati na kurefusha barabara ya kutua na kuruka ndege kwa kiwango cha lami kutoka urefu wa mita 1,500 na upana wa mita 30 hadi urefu wa mita 1,820.
·         Kujenga eneo jipya la maegesho ya ndege kwa kiwango cha lami lenye ukubwa wa kubeba ndege mbili aina ya ATR 42.
15.2. MAFANIKIO:
Kazi zote za ujenzi wa matabaka ya lami , ujenzi wa mfumo wa maji ya mvua (drainage works) na ulipaji wa fidia wa mali kwa ajili ya kupisha  upanuzi wa kiwanja zimekamilika kwa asilimia 100%. Kwa hivi sasa Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa uzio, kupanda majani katika eneo la usalama (runway strip), kuchonga barabara ya kuzunguka kiwanja  (peripheral road) pamoja na kuweka alama (markings) kwenye barabara ya kutua na kuruka ndege.  Kwa ujumla kazi zote katika mradi huu zimekamilika kwa asilimia 98%.

15.3. CHANGAMOTO:
Changamoto kubwa zinazojitokeza kwenye mradi huu ni mwingiliano wa miundombinu ya reli na barabara kwenye kiwanja cha ndege.

 15.4. MAPENDEKEZO:
Ili kiwanja kiweze kuwa endelevu inapendekekezwa kuhamishwa kwa barabara ya Mpanda /Tabora iliyopo  katikati ya eneo la reli na kiwanja . Aidha njia ya reli inayokatisha mwisho wa barabara ya kuruka na kutua ndege upande wa mashariki (runway 27) ihamishwe ili kupisha upanuzi wa  baadaye wa kiwanja.  Upanuzi huu ukifanyika utakidhi mahitaji ya ndege kubwa aina ya Boeng B737.
                 
15.5. KIWANJA CHA NDEGE CHA SUMBAWANGA

Kiwanja kina barabara moja ya kutua na kuruka ndege yenye urefu wa kilomita 1.6 na upana wa mita 30 kwa kiwango cha changarawe. Kutokana na shughuli za kiuchumi za Mkoa wa Rukwa  kumekuwepo na ongezeko kubwa la safari za ndege kutoka safari 57 mwaka 2002 hadi kufikia  safari za ndege 129 mwaka 2010. Idadi ya abiria nayo imeongezeka kwa asilimia 198 kutoka  idadi ya abiria 122 hadi kufikia 364 mwaka 2010.


15.6. CHANGAMOTO:
Changamoto zilizopo katika uwanja huu ni pamoja na:-
·         Kiwanja kuwa kwenye daraja sifuri la viwango vya zima moto kutokana na kutokuwepo gari la kutoa huduma za zimamoto
·         Uwanja kuwa na eneo dogo na kuwa karibu na eneo la Mji wa Sumbawanga.
 15.7. MIPANGO YA BAADAYE:
Kujenga uwanja wa kisasa katika kijiji cha Kisumba kilichoko umbali wa Km.20 kutoka mjini Sumbawanga.  Tayari eneo lenye ukubwa wa ekari 100 limepatikana.  Kazi ya upimaji inaendelea sambamba na ulipaji fidia.

16.0  HUDUMA YA RELI:
Kituo cha reli Mpanda ni maarufu katika kutoa huduma za usafirishaji wa abiria pamoja na mazao ya chakula na biashara.

16.1. MAFANIKIO:
Tangu kuanza kwa msimu wa mazao mwezi April 2011 hadi Desemba 2011 kituo kimesafirisha jumla ya tani 16,926 za mazao ya chakula na biashara. Kituo kimesafirisha pia tani 33,680 za mahindi kati ya tani 55,000 zilizotakiwa kusafirishwa msimu huu kutoka kwenye ghala la serikali la kuhifadhia chakula Mpanda kwenda Shinyanga. Hii ni sawa na mabehewa 842.

16.2. CHANGAMOTO:
Shirika hili katika kituo hiki cha Mpanda linakabiliwa na:-

·         Uchakavu wa miundombinu ya reli, uchache na uchakavu wa injini na mabehewa
17.0. BANDARI YA KASANGA
Bandari ya Kasanga inasimamiwa katika shughuli za uendeshaji na kampuni ya Agro Truck Investment Ltd. Kampuni hii inakarabati ghati kwa kuongeza eneo la kuegesha meli pamoja na ujenzi wa ghala ili kukidhi mahitaji ya abiria na mizigo. Fedha za ukarabati zilipatikana kwa msaada wa Serikali ya Norway kupitia ushirikiano wa Rukwa Association of Non Governmental Organization (RANGO). Ujenzi utagharimu Dola za Marekani 200,000.


17.1. MAFANIKIO:
·         Bandari inatazamia kupanuliwa kwa kujenga Godowns na majengo mengine ili kukidhi mahitaji ya bandari. Kwa hivi sasa tayari godowns 2 zimejengwa na zinatumika kikamilifu. Godowns  zinahifadhi tani 3,000 kila moja. Godowns zote zimegharimu Sh. bilioni 1.1. kutoka Mamlaka ya Bandari.
17.2. CHANGAMOTO:
Bandari ya Kasanga inakabiliwa na changamoto nyingi katika uendeshaji wake.  Changamoto hizo ni pamoja na:-
·         Ukosefu wa fensi kuzunguka eneo la bandari
·         Ukosefu wa nyenzo za kufanyia kazi ikiwepo focal lifts, winchi na safari chache za meli zinazofanywa kwa mwezi, na ukosefu wa huduma ya umeme wa uhakika.
18.0. SEKTA YA ARDHI.

Mheshimiwa Makamu wa Rais,
Mkoa hutegemea ardhi kwa ajili Shughuli za Kilimo na kiuchumi katika kuleta maendeleo endelevu na kupunguza umaskini, mchango wa Sekta ya Ardhi katika maendeleo ya Mkoa ni pamoja na uhakika wa kupata chakula na kipato.

18.1. CHANGAMOTO:
Mkoa unakabiliwa na changamoto zifuatazo:-

(i)           Mipango ya matumizi bora ya ardhi; Halmashauri hazijafanya kazi ya kutosha kutokana na ufinyu wa bajeti. Kazi hii ikifanyika kikamilifu itasaidia  kuepusha migogoro ya Wakulima na wafungaji katika Mkoa wetu.

19.0 MKONGO WA TAIFA
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Shughuli za kutandaza Mkongo wa Taifa zinaendelea katika Mkoa wetu hadi sasa hakuna tukio lolote la hujuma dhidi ya Mkongo lililotokea Mkoani kwetu.

20.0 SEKTA YA NISHATI

20.1.        MITAMBO YA KUFUA UMEME
Mheshimiwa Makamu wa Rais
Mji wa Sumbawanga unategemea umeme kutoka nchi jirani ya Zambia.  Hivi karibuni Serikali ilinunua na kufunga Generator nne zenye uwezo wa  kuzalisha megawati tano (5) .

(i)               Kazi ya kusimika Mitambo ya kufua Umeme ilianza mwanzoni mwa mwezi April, 2011 na kumalizika mwanzoni mwa mwezi Juni, 2011.
(ii)              Mitambo ilianza kufua Umeme kuanzia tarehe 02.08.2011 japokuwa kwa vipindi tofauti tofauti umeme huu umekuwa haupatikani kwa sababu ya kukosekana kwa mafuta yakuendeshea mitambo.

20.2. MRADI WA UMEME NAMANYERE
Kazi ya Mradi huu ilitarajiwa kukamilika mnamo mwezi Disemba, 2011, lakini hadi sasa kazi ya kutandaza nyaya inaendelea, na utandazaji wa nyaya umefika Mji wa Namanyere Wilayani Nkasi. Ni matumaini ya mkoa kuwa umeme utawaka mjini Namanyere na vijiji 12 vya njiani muda mfupi ujao.

21.0. MFUKO WA KUBORESHA MAZINGIRA YA WATUMISHI MKOA WA RUKWA (RCSFF)
Mfuko wa kuboresha mazingira ya Watumishi Mkoa wa Rukwa (Zamani mfuko wa Mwalimu Nyerere) tangu kuzinduliwa, umeweza kuleta jumla ya Walimu wa Sekondari 380 pamoja na Watumishi wa Idara ya Afya 36 ( katika kada za Madaktari na Wauguzi)

21.1.        HALI YA KIFEDHA YA MFUKO
Hadi sasa mfuko una jumla ya Sh.7,115,437.53 tu. Kwenye akaunti zake mbili zilizo katika benki za CRDB na NMB.  Aidha, Mfuko umewekeza fedha sehemu mbili tofauti kama ifuatavyo:-
 1. UTT zimewekezwa Sh.200,000,000/= ambazo zimeishatoa faida ya Sh.19,057,911
 2. Benki ya CRDB zimewekezwa Sh.35,000,000/= ambazo zimetoa faida ya Sh.2,450,000/= Hata hivyo faida hii ilishatumika kuwahudumia Madaktari walioletwa kabla majina yao kuingizwa kwenye Pay roll.

21.2.        CHANGAMOTO NYINGINE ZINAZOUKABILI MFUKO
(i)        Halmashauri hazichangii Mfuko wa kuboresha Mazingira kwa Watumishi
(ii)      Mfuko umeendelea kubeba mzigo mzito wa kuwalipa mishahara Madaktari na Walimu ambao hawajaingizwa kwenye Pay roll
Wananchi wengi bado hawajafahamu umuhimu wa kuchangia mfuko huu kutokana na kutokuwa na taarifa sahihi za mfuko

22.0. KONGAMANO LA UWEKEZAJI.
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mkoa Umeweza kuandaa kwa mafanikio makubwa Kongamano la uwekezaji Kanda ya Ziwa Tanganyika lililofanyika Wilayani Mpanda kuanzia tarehe 15-18/10/2011 na kufunguliwa rasmi na Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 17/10/2011. Kongamano hilo lilikuwa na lengo la kuzinadi fursa za Uwekezaji zinazopatikana katika Ukanda huu. Jumla ya washiriki zaidi ya 300 walishiriki kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo mabalozi 34 kutoka nchi mbalimbali.
23.0. MAONESHO YA SIDO KANDA YA NYANDA ZA JUU
          KUSINI
Mkoa wa Rukwa ulikuwa mwenyeji wa maonesho ya SIDO kwa Kanda ya Nyanda za juu kusini ambayo yalifanyika tarehe 11/11/2011 katika Manispaa ya Sumbawanga. Mgeni rasmi katika maonesho hayo alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Lazaro S. Nyarandu (Mb).

24.0. TAMASHA LA UTAMADUNI WA MTANZANIA.
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Jamii ya Wana Rukwa na Katavi wameweza kuadhimisha tamasha la utamaduni wa Mtanzania Kijitonyama katika Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam tarehe 25 - 27/11/2011. Mkoa umeanza utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa kwenye hotuba wakati wa kufunga maadhimisho. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imetoa chumba maalumu kwa ajili ya kuanzia utunzaji wa vitu vya asili na shughuli za makumbusho kwa Mkoa.

25.0. MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA BARA
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mkoa umefanikiwa kutoa kitabu maalumu kinachoelezea wapi tulipokuwa wapi tulipo na wapi tuendako, kitabu hicho kinaitwa ‘‘TAARIFA YA MAFANIKIO YA MIAKA 50 YA UHURU MKOA WA RUKWA DESEMBA 1961 - DESEMBA, 2011”

Mkoa umeweza kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania bara kwa kufanya maonesho Viwanja vya Sabasaba vya Mwalimu J.K. Nyerere vilivyopo Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 1 - 12 Desemba, 2011. Katika ngazi ya Mkoa maadhimisho yalifanyika Mjini Namanyere, kwa kuambatana na maonesho ya shughuli mbalimbali za idara za serikali na mashirika ya Umma zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wajasiriamali na Wadau wengine wa Maendeleo.

26.0.0      UTAWALA BORA.
26.1.0      TAARIFA YA MAMLAKA YA SERIKALI ZA MITAA.
26.1.1      MAPATO YA HALMASHAURI
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mwaka huu wa fedha 2011/12 Halmashauri zililenga kukusanya Sh,8,725,183,992/= hadi kufikia Desemba 2011 zimeweza kukusanya Sh 2,057,492,786/ sawa na asilimia 24 ya lengo la mwaka.

26.1.2      UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO.
Katika mwaka wa 2011/12 Halmashauri zilitengewa jumla ya Sh. 19,991,691,428/= ambapo hadi Desemba 2011 fedha zilizopokelewa ni Sh.5,337,582,874/= sawa na asilimia 27 tu ya lengo.

Miradi ya maendeleo imekuwa ikitekelezwa kulingana na fedha zinavyopokelewa. Halmashauri zinakabiliwa na changamoto za kuchelewa kupata fedha kutoka Serikali Kuu.

26.1.3.     VIKAO VYA KISHERIA.
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Halmashauri zimeendelea kuendesha vikao vyao vya Kisheria kama kawaida.

26.1.4.     HALI YA WATUMISHI.
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Halmashauri zote za Mkoa wa Rukwa na Katavi zina Wakurugenzi wenye sifa isipokuwa nafasi moja tu ya Mkurugenzi wa Mpanda Mji inakaimiwa kutokana na kustaafu kisheria kwa Mkurugenzi aliyekuwepo baada ya kufikia umri wa miaka 60. Aidha nafasi nyingi za Wakuu wa Idara zimejazwa isipokuwa nafasi chache tu za Wakuu wa Idara ya Afya Manispaa na Sumbawanga zinakaimiwa pamoja na nafasi ya Mhandisi wa Maji na Ujenzi Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Halmashauri zinakabiliwa na uhaba wa watumishi katika Sekta ya Afya na Elimu


26.1.5      HOJA ZA UKAGUZI.
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Halmashauri zimeendelea kujibu hoja za ukaguzi za ndani na nje za mwaka 2009/2010 hii inalenga pia kuboresha hali ya usimamizi wa matumizi ya fedha. 
26.2.0.  MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA
Elimu imetolewakupitia vipindi vya redio mara tatu, machapisho (1325), Semina kumi na mbili (12), mikutano ya hadhara thelathini (30) na vilabu vya wapinga rushwa Mashuleni sitini na mbili (62). Aidha, TAKUKURU pia imeendelea kuchunguza makosa ya rushwa hasa katika pembejeo za kilimo ambapo kati ya Julai 2011 hadi Januari 2012 kesi za pembejeo zipatazo (12) zimefunguliwa mahakamani ambapo washitakiwa wapatao thelathini (30) wakiwemo mawakala na watendaji wa Serikali wamefikishwa mahakamani.

26.3.0.  HALI YA MAGEREZA MKOANI
Mkoa una magereza matano ambayo ni Gereza Mollo, Mahabusu Sumbawanga, Mahabusu Mpanda, Kalila na Kitete.

(i)           Magereza ya Kilimo:
Kilimo kina fanyika katika magereza ya Mollo, Kalila na Kitete yenye ukubwa wa ekari  41,648.75 kati ya hizo ekari 18,868.25 zinafaa kwa kilimo, ekari 21,425.5  zinafaa kwa malisho

(ii)          Magereza ya Mahabusu
Mkoa una magereza mawili ya Mahabusu Sumbawanga  na Mpanda yenye uwezo wa kuhifadhi wahalifu 211.  Kwa sasa yanahifadhi wahalifu mpaka 730.

      (iii)    Kilimo na Mifugo.
Eneo linalolimwa na magereza yetu lina ukubwa wa hekta 373 na jumla ya mifugo inayofugwa ni 341 ikihusisha Ng’ombe, Mbuzi na Nguruwe. 

26.3.1. CHANGAMOTO:
 • Ukosefu wa jengo la Ofisi ya Magereza Mkoa kwani inayotumika sasa ni nyumba ya mtumishi na mabanda yaliyoongezwa kwa muda.
 • Ukosefu wa gereza la mahabusu wilaya ya Nkasi. 
 • Ukosefu wa maji katika magereza yetu hasa gereza Kalila na Kitete


26.4.0.  USALAMA WA RAIA:

Kumekuwepo na ongezeko la makosa na uhalifu kama vile mauaji kwa imani za ushirikina, unyang’anyi wa kutumia nguvu, kuchoma nyumba moto na uvunjaji yameongezeka. 

26.4.1 MAFANIKIO:

Juhudi za Jeshi la Polisi katika kupambana na uhalifu tumefanikiwa kupunguza mauaji ya vikongwe wanaotuhumiwa kwa imani za kishirikina, jakapokuwa katika takwimu zetu zinaonesha kuwa mauaji yamezidi, sio kwa vikongwe ni kwa rika mbali mbali hasa umri wa kati ya miaka 40 hadi 50. 

26.4.2 CHANGAMOTO:

a.   TATIZO LA ARDHI:  wananchi wengi vijijini wanauana kugombea mashamba.

b.   MIFUGO:  Ongezeko la mifugo vijijini imekuwa ni chanzo cha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

c.   MATUKIO YA KUCHOMA NA KUBOMOLEANA NYUMBA:
Baada ya mavuno wananchi huchomeana na kuboleana nyumba kwa kisingizio cha imani za kishirikina.

26.5.0.  MASUALA YA UHAMIAJI:

Mkoa ulibaini kuwa na wahamiaji haramu elfu kumi na nne mia nne thelathini na tatu (14,433) kutoka Congo DRC, Burundi, Zambia  na Rwanda. 

26.5.1 MAKAZI YA WAKIMBIZI YA KATUMBA NA MISHAMO:

Mkoa unayo makambi mawili ya Wakimbizi ya Katumba na Mishamo yenye wakimbizi zaidi ya 200,000. Wakimbizi hawa wamekuwa ni tatizo la kiusalama katika Mkoa wetu baadhi wanajihusisha na matukio ya ujambazi na unyang’anyi hata kuhusika na kununua maeneo ya ardhi ya Wananchi.

26.5.2. MAFANIKIO:

Wahamiaji haramu 255 wamekamatwa kwa mwaka 2011, wengine walipelekwa Mahakamani wengine walifungwa na wengine 172 walipewa hati ya kufukuzwa nchini (PI. NOTICE)

26.5.3. CHANGAMOTO:

Vituo vya mipakani ukiondoa kituo cha Kasesya havina majengo ya Ofisi. Suala la usafiri ni tatizo kwa vituo vyote hasa vituo.

26.6 ULINZI WA MGAMBO:

Mkoa huendesha mafunzo ya Mgambo kila mwaka, lengo la mwaka uliopita lilikuwa ni kutoa mafunzo ya Mgambo kwa wanamgambo 600, mafunzo yalianza Julai, 2011. Mafunzo yalitolewa katika vituo vinne (4) ambapo washiriki 596 walianza mafunzo na waliohitimu ni 420 na kufanya Mkoa wetu kuwa na jumla ya wanamgambo 15,155.

27.0. SENSA YA WATU NA MAKAZI
Mheshimiwa Makamu wa Rais, Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ambayo imepangwa kufanyika nchini mwezi Agosti mwaka 2012 yameanza katika mkoa wetu ambapo hatua za maandalizi zilizofanyika hadi sasa ni pamoja na wataalam wa kutenga maeneo wanaendelea na kazi mkoani na mpaka sasa wameshamaliza kazi hiyo katika Halmashauri za Wilaya Sumbawanga, Manispaa ya Sumbawanga na katika Tarafa ya Mpimbwe. Hivi sasa wanaendelea na kazi hiyo katika Halmashauri ya Wilaya Nkasi. Kazi hii inategemea kukamilika mwezi Februari, 2012.
28.0 HITIMISHO

Mheshimiwa Makamu wa Rais, Napenda kuchukua fursa hii kwa mara nyingine tena kukukaribisha Mkoani kwetu wewe na ujumbe wako nawatakia afya njema na kila la kheri katika kipindi chote cha ziara yako Mkoani Rukwa.

Tupo tayari kutekeleza yote utakayo tuagiza na kutuelekeza katika kipindi chote utakachokuwa pamoja nasi.

“KARIBU SANA   

No comments:

Post a Comment