Tuesday, February 7, 2012

WANANCHI KIJIJI CHA MILEPA MKOANI RUKWA WAMKATAA MWENZAO MBELE YA MKUU WA MKOA HUO LICHA YA JITIHADA ZAKE KUBWA ZA KUWASULUHISHA


Mwanakijiji wa Kijiji cha Milepa Said Mohammed akiwa na Mtoto wake kwenye Mkutano wa hadhara ambapo wanakijiji wenzake walimkataa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Manyanya kwa madai kuwa amekuwa akifanya nyumba yake kama mahakama huku akiwatoza faini wanakijiji aliokamata mifugo yao shambani kwake na wengine kuwafungulia kesi mbali na Kijiji chao ikiwemo katika Manispaa ya Sumbawanga ambapo huwa ngumu kwao kuhudhuria kutokana na umbali wakati kuna mahakama za karibu ambazo zina uwezo wa kusikiliza kesi hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Manyanya akiongea na wananchi wa Kijiji cha milepa katika kujaribu kutafuta ufumbuzi wa bwana Said Mohammed kufukuzwa kijijini hapo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Kanali John Antonyo Mzurikwao, Mwenekiti wa Kijiji hicho Godfrey Njelu na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa (RPC) Isunto Mantage.

 Wananchi wa Kijiji cha Milepa waliitikia wito wa Mkuu wa Mkoa na kuhudhuria kwa wingi kwenye Mkutano huo kama inavyoonekana pichani.
 Mkuu wa Mkoa akisisitizia jambo, Miongoni mwa mambo muhimu aliyoyasisitiza ni pamoja na uchangiajai katika mfuko wa afya ya jamii, uzazi wa mpango, kinamama kujifungulia hospitalini au kwenye vituo vya afya kuepuka vifo vya mama na mtoto,  na umuhimu wa wananchi kutojichukulia sheria mkononi. 

Wanafunzi pamoja na watoto pia walikuwepo kwenye Mkutano huo. Wengi wao walionekana kuhamasika kwa bwana Saidi kuondoka kijijini hapo.


 Wananchi mbalimbali wa kijijicha Milepa wakionyesha hasira zao huku wakielezea kero zao kwa Mkuu wa Mkoa zilizokuwa zikiwakabili dhidi ya bwana Said Mohammed aliyekataliwa kuishi kijijini hapo. 

Ilifika wakati mambo yakawa magumu, Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kuona wanakijiji wa kijiji hicho hawashikiki kuhusu hatma ya bwana Said kubaki kijijini hapo alilazimika kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutafuta suluhu ya jambo hilo. Alifikia muafaka kwamba bwana Saidi aondoke arudi Sumbawanga apate muda wa kutathmini hali aliyoiona na wananchi wa Milepa nao wapate fursa ya kuona kama wanaweza kumsamehe. Hata hivo bwana Saidi alishauriwa kujipnga upya kwa kuona ni jinsi gani ataanzisha maisha mapya sehemu tofauti na Milepa kwa usalama wake binafsi kwani Serikali haina uwezo wa kumlinda mwananchi mmoja mmmoja. Mkuu wa Mkoa alisema Ofisi yake itaangalia ni jinsi gani ya kumsaidia bwana Saidi baada ya kukataliwa kijijini kwao.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akimkabidhi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwenyekiti wa Kijiji cha Milepa katika Wilaya ya Sumbawanga Godfrey Njelu ili aitumie kama dira ya kuwaongoza watu wake na kuitumia katika kutatua migogoro mbalimbali. Aidha alimuasa atumie katiba hiyo kuwaelimisha wananchi kwenye mikutano ya hadhara kuwaweka sawa wananchi katika mchakato wa maandalizi ya kuandaa katiba mpya. Mkuu huyo wa Mkoa alitumia katiba hiyo kutatua mgogoro wa mwananchi Said Mohammed ambaye alikataliwa kuishi kijijini hapo


WANANCHI wa kijiji cha Milepa kilichopo wilayani Sumbawanga, wamemfukuza rasmi mbele ya uongozi wa mkoa wa Rukwa, mkazi mwenzao anayedaiwa kuwa kinara wa vitendo vya unyanyasaji na kuwalipisha faini wananchi wenzake kinyume na utaratibu.

Mkazi huyo aitwaye Said Mohamed (40) ambaye awali walitangaza kumtimua kijiji hapo mei 30 mwaka jana, alipeleka malalamiko yake ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa, ambapo mkuu huyo wa mkoa, Injinia Stella Manyanya, akiwa na viongozi wengine wa mkoa na wilaya walilazimika kufika kijiji hapo kwa lengo la kusaka suluhu lakini wananchi hao walikataa kumpokea mkazi huyo.


Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji hapo, baadhi ya wananchi waliopewa fursa hiyo walisema kuwa hawako tayari kuishi katika kijiji hicho na Mohamedi kwa kuwa amewafanyia vitendo vya uonevu na unyanyasaji kwa muda sasa ambapo amefikia hatua hata ya kufanya nyumbani kwake mahakama kuwahukumu wanakijiji wenzake.

Vitendo hivyo ni pamoja na kuwalipisha faini kubwa kunyume na utaratibu wakati pia yeye si kiongozi wa kijiji, ambapo mara kadhaa mifugo inapoingia katika shamba lake au kupita nyumbani kwake amekuwa akitoza faini kuanzia shilingi 300,000 hadi 500,000 kitu ambacho kinawaumiza wananchi na wale wasio na uwezo wa kulipa faini hizo amekuwa akikamata mifugo yao na kuitaifisha.

Mmoja wa wananchi hao, Potino Simfukwe alisema kuwa kamwe hawawezi kumruhusu Mohamedi kuendelea kuishi kijijini hapo, kwa kuwa wamechoka vitendo vyao vya dhuruma na uonevu ambao ameufanya kwa muda mrefu sasa.

"hatuwezi kumpokea huyo mtu...... mkuu wa mkoa tunakuheshimu sana tunaomba ondoka naye kwa kuwa tofauti na hivyo ipo siku polisi watakuja na kukamata watu wote hapa kijijini na kutupeleka jela" alisema Simfukwe pasipo kufafanua.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho, Godfrey Njelu aliongeza kuwa malalamiko dhidi ya Mohamedi ni ya muda mrefu sasa na kijiji kilishafanya uamuzi wa kumfukuza katika mkutano wa hadhara wa kijiji ambao mihustari yake ipo hivyo wao kama viongozi wanatekeleza maagizo ya wananchi na si vinginevyo.

Akijibu hoja hizo Mohamedi ambaye ni mzaliwa katika kijiji hicho, alisema kuwa chanzo cha viongozi hao kumchukia na kushinikiza wananchi wamfukuze ni kwa sababu amekuwa akitumia fursa ya uelewa alionao kuhoji mapato na matumizi kijijini hapo. 

Kwa mujibu wa bwana Said ambaye alipewa fursa na Mkuu wa Mkoa ya kujitetea alisema kuwa amekuwa akihoji uingiaji wa wafugaji wa ng'ombe wakiwa na makundi makubwa ya mifugo pasipo kufuata taratibu wakati kijiji hakina maeneo ya malisho, upasua mbao kiholela pasipo vibali, Uvuvi Haramu, mapato na matumizi ya kijiji kwani ni mwaka wa pili tangu aanze kuhoji hakuna majibu yanayoridhisha.


Kwa upande wake Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa hali ilipofikia ni mbaya na hawezi kupinga uamuzi wa wanakijiji hao ila kinachoweza kufanyika kwa sasa ni mwananchi huyo kukaa na kutafakari ni namna gani atakavyoendesha maisha yake eneo jingine,kwa amani na utulivu huku uongozi wa mkoa ukiangalia ni hatua zipi utachukua ili kuweza kumsaidia mkazi huyo na familia yake lakini kwa sasa inabidi arejee mjini Sumbawanga kwa muda akisubiri taratibu hizo kufanyika.

No comments:

Post a Comment