Tuesday, March 13, 2012

KIKAO CHA 22 CHA BODI YA BARABARA MKOANI RUKWA CHAFANYIKA LEO, MAAZIMIO MBALIMBALI YAFIKIWA


 Katibu wa Kikao cha Bodi ya barabara Mkoa wa Rukwa ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa huo Alhaj Salum Mohammed Chima akitoa neno la ukaribisho kwa wajumbe wa kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa RDC Mkoani humo leo.

 Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Dkt. Rajab Rutengwe kulia akiteta na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Joyce Mgana wakati kikao hicho kikiwa kinaendelea.

Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akitoa hotuba ya ufunguzi. 

MANENO YA UFUNGUZI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA ENG.STELLA MARTIN MANYANYA (MB) YA KIKAO CHA BODI YA BARABARA TAREHE 13/3/2012
Mhe. Mwenyekiti wa CCM, Ndugu H. Matete,
Katibu Tawala wa Mkoa, Ndugu Salum M. Chima,
Waheshimiwa. Wakuu wa Wilaya, Col. John Antonyo. Mzurikwao, Bibi Joyce Mgana, na Dr. Rajab Lutengwe,
Wah. Wabunge,
Meya, na Wenyeviti wa Halmashauri zote za Mkoa wa Rukwa ,
Wakurugenzi,
Meneja wa Tanroad Rukwa, Katavi,
Wakuu wote wa Idara,
Mabibi na Mabwana.
Rukwa Ruka!, Sumbawanga Ng’ara!
-          Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai.

-         Pili napenda kuwakaribisha katika Kikao hiki, na poleni kwa safari kwa wale mliotoka mbali. Aidha kwa kuwa hiki ni kikao chao cha kwanza nachukua nafasi hii kuwakaribisha rasmi Mameneja wa Tanroads hawa wawili.
1.   Eng. Florian M. Kabaka – Rukwa
2.  Eng. Isaak  Kamwelwe – Katavi
kuungana nasi katika kuhakikisha kuwa Rukwa na Katavi inapitika wakati wote, na kuifanya kuwa ni Mikoa bora ya kuwekeza.
-         Napenda pia kuchukua nafasi hii kuwapongeza Mameneja wote wawili wa Tanroads, Manispaa, Halmashauri pamoja na Makandarasi wao kwa jinsi ambavyo walitoa ushirikiano katika kuboresha barabara zetu na kuzifanya zipitike katika kipindi hiki chote cha masika, lakini kwa namna ya pekee kufuatia ujio wa Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hali ya Barabara
Kwa ujumla wake Mkoa uliweza kupokea wageni toka Mellenium Challenge Account – Tanzania MCA – T na kufanya nao mazungumzo hapo Mkoani kwetu na pia na Mkuu wa Mkoa katika Kikao cha pamoja na Mikoa wa Ruvuma tarehe 9/3/2012.  Ugeni huo uliongozwa na Ndugu Benard  S. Mchomvu wa MCA-T, ndugu Anold J. Maenda PC – Tanroads HQ na Josephat Kanyunyu Outreach Officer MCA - T na kwa upande wa mfadhili ndugu Karl Fickenscher MCC Tanzania,– T.
Maelezo yao ni kuwa wanaridhika na maendeleo ya barabara wanazozifadhili na wanategemea kukamilisha ujenzi huo ifikapo Juni 2013. Pia Mkoa uliomba kuifikiria barabara Mpanda – Inyonga katika awamu ya pili.
Lakini pia hata kwa macho kazi zinazoendelea zinaridhisha.
-         Pia tunayo habari njema kwa wananchi wa Laela kuwa kufuatia maombi yetu ya kuwaomba kutengeneza daraja la Laela kwenda kituo cha Afya, wanakubali na hivyo wapo katika mchakato wa maandalizi muhimu juu ya utekelezaji wake.
Kwa upande wa barabara Kuu zinazofadhiliwa na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, juhudi za kupata pesa zinaendelea japo katika miezi hii mitatu, kazi zimepungua kasi.
Hata hivyo mkoa umefuatilia na kupata ahadi ya kupewa kipaumbele mara tu pesa zikipatikana, hasa ikizingatiwa umuhimu wa barabara hizo katika kusafirisha mazao ya chakula.
Hali ya barabara za Halmashauri, zinaendelea kutengenezwa kwa kiasi chake, lakini kwa uzito wa pekee, kikao kipate taarifa kuwa niliandika barua kuiomba Wizara ya Ujenzi ili ione uwezekano wa kuisaidia barabara ya Kalambo Ranch – Kala ambayo hali yake ni mbaya sana, na mfuko wa Halmashauri pekee hauwezi kufanikisha ipasavyo.
-         Nimepata malalamiko mengi ya barabara ya mjini ya Chanji, naona kikao hiki pia kitaazimia.
-         Pamoja na uhaba huo kifedha unaotokana na majukumu mengi ikiwemo kuondoa kero ya umeme, na sasa madai ya Madaktari, Mkoa unampongeza sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Serikali yake kwa jinsi ambavyo amedhamiria kwa dhati kuondoa kero za mikoa ya pembezoni ikiwemo hasa za Barabara.  Mwenyezi Mungu ampe maisha marefu.
-         Pia tunawashukuru wafadhili wetu wa Marekani.
-         Waheshimiwa Wajumbe, baada ya maneno haya ya utangulizi, nawaomba wajumbe wote tutoe ushirikiano katika kujadili na kutoa mawazo yetu kikamilifu ili kuhakikisha kuwa Mkoa wetu unaruka.
Na sasa natamka kuwa Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoani Rukwa na Katavi kimefunguliwa rasmi.
 Sekretarieti ya kikao hicho ikiwa kazini kuhakikisha kuwa hakuna neno linalotoka kwenye kinywa cha wajumbe katika kikao hicho bila kuingia kwenye karatasi zao.

 Wajumbe wa kikao hicho wakifuatilia agenda mbalimbali za kikao hicho

Wajumbe wa kikao hicho wakiendelea kusikiliza kwa umakini hoja mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa kwenye kikao hicho
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa Florian Kabaka akiwasilisha taarifa ya Idara yake kwenye kikao hicho.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM) akiwasilisha moja ya hoja zake katika kikao hicho.  

Wa kwanza kutoka kushoto ni Meneja wa Tanroads Mkoa wa Rukwa Frorian Kabaka, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya, Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaji Salum Chima na Makamu Mwenyekiti wa kikao hicho Ignas Malocha. 
 Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Dkt. Rajab Rutengwe akizungumza kwenye kikao hicho, kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Joyce Mgana.

 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Injinia Emmanuel Kalobelo akiperuzi kabrasha la kikao hicho.
 
MAAZIMIO YA KIKAO CHA BODI YA BARABARA CHA TAREHE 13 MACHI, 2012

1.         Barabara za Kitosi – Wampembe, Nkana – Kala na Korongwe zichukuliwe na TANROADS au zipewe msaada maalum kwani zinahitaji fedha nyingi, na ni barabara za mpakani.
2.    Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ihakikishe barabara ya Sopa – Kamawe – Kasanga – Ngorotwa inatengewa fedha katika budget ya mwaka 2012/2013 kuliko kutegemea maombi maalum.
3.    TANROADS wamalizie utengenezaji wa barabara ya Kipili kwenda kwenye Gati, na barabara hiyo iunganishwe kuwa ya TANROAD.
4.    Mwanasheria RS ahakikishe Halmashauri zinafuatilia na kupata sheria za barabara zilizopelekwa TAMISEMI ndani ya miezi miwili.
5.    Barabara ya Mpanda – Inyonga – Koga kwenda Tabora itengenezwe na kuwa nzuri kama ambavyo kipande cha Koga – Sikonge – Tabora ni kizuri.
6.  Uhamishaji wa barabara ya Mpanda – Inyonga na reli ya Mpanda – Tabora ufanyike ili kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege.
7.  Halmashauri zote na Manispaa zihakikishe zinatenga pesa maalum kwaajili ya matengenezo ya barabara za udongo za kijamii na mijini kwa kutumia nguvu kazi ya wananchi hasa vijana.
8.Kila ihakikishe kuwa inawatumia Wahandisi, na kama hawapo waajiriwe ili kuboresha kazi na kama wana matatizo waadhibiwe.
 
9.Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya wote wanaohusika na utekelezaji wa kazi za barabara  katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

No comments:

Post a Comment