Thursday, March 15, 2012

MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI YA USHAURI YA MKOA WA RUKWA TAREHE 14/02/2012

 
MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI YA USHAURI YA MKOA (RCC)     CHA 23  KILICHOFANYIKA  TAREHE 14/03/2012.
1.    Mkoa umeazimia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania            Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa jinsi alivyoushughulikia mgogoro wa mgomo  wa Madaktari kwa hekima na busara kubwa.

2.    Mkoa uone namna ya kuwapongeza madaktari na watumishi wa Afya  wa Mkoa wa Rukwa ambao hawakugoma katika vipindi vyote vya mgomo.

3.    Halmashauri zote zihakikishe zinaunga mkono suala la usafi wa mazingira katika maeneo yao kama ilivyo kauli mbiu ya “Sumbawanga Ng’ara”.

4.    Ukomo wa bajeti ya Mkoa wa Rukwa ubakie uleule  na ukomo wa bajeti wa Mkoa mpya wa Katavi uandaliwe

5.    Halmashauri zote zihakikishe zinakamilisha viporo vya miradi ya nyuma na kuwa na miradi michache inayokubalika na yenye tija itakayotekelezwa na kukamilika kwa wakati.
6.    Halmashauri zihakikishe majengo yote marefu yanawekewa vizuia radi
7.    Meneja wa TANESCO akumbushwe juu ya ujenzi wa kitaalam wa nguzo za umeme ili zisiathiriwe na radi.
8.    Halmashauri zihakikishe kuwa zinapima maeneo na kasi ya upimaji iongezeke pia wanakijiji wapimiwe maeneo yao ili kuongeza thamani na kupewa fursa ya kukopa kutoka taasisi za fedha.
9.    Halmashauri zihakikishe kuwa kila kijiji kinakuwa na Afisa ugani na pale inaposhindikana taarifa itolewe mapema ili kuona namna ya kuwapata au kutatua tatizo hilo.
10. Katika bajeti za mwaka 2012/2013 za Mamlaka za Serikali za Mitaa, ziwekwe bajeti kwa ajili ya usafi wa mazingira.
11.   Sera ya Ujasiriamali itafutwe na Wajumbe wagawiwe katika kikao kijacho.
12.   Ufanyike ufuatiliaji wa kina ili kujua ni kwa nini wanafunzi wanaofaulu hawajui kusoma, kuhesabu na kuandika.
13.   Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga iandae taarifa ya kina juu ya Maombi ya kufuta usajili wa vijiji kumi (10), taarifa hiyo ioneshe hali ya maeneo hayo na Mpango Mkakati wa Halmashauri kuhusiana na wakaazi wa vijiji hivyo. Taarifa hiyo iwasilishwe kwenye Kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Sekretarieti ya Mkoa, utekelezaji utaletwa kikao kijacho.
14.   Uongozi wa Mfuko wa Kuboresha Mazingira ya watumishi Mkoa wa Rukwa uimarishe uwazi kwa wadau wake na mikakati yote ya Mfuko iwashirikishe Wadau wake katika kufanya maamuzi.
15.   Kwa kuwa miundombinu ya Walemavu ni hitaji la Kisheria, kila jengo la umma lazima lioneshe njia ya Walemavu.
16.   Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa na Katavi pamoja na Halmashauri zake ziendelee kuboresha bajeti ya 2012/2013 kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) pamoja na Mwongozo wa Bajeti ya 2012/2013 – 2016/2017.
17.   Halmashauri zihakikishe zinabaini vizuri vyanzo vyake vya mapato ya ndani na kuboresha makusanyo yake ikiwemo uhakiki wa mara kwa mara wa makisio na kusimamia vizuri mawakala wa ushuru.
18.   Mkoa ufanye mkakati wa pamoja kati ya Mkoa na Halmashauri katika mazoezi ya ukusanyaji wa mapato.
19.   Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga, Manispaa ya Sumbawanga pamoja na Sekretarieti ya Mkoa zishughulikie mgogoro wa mipaka ya ardhi ya Mwekezaji Efatha na vijiji vya Sikaungu na Msanda Muungano; kazi hii ikamilike ndani ya mwezi mmoja.
20.   Mkoa umeupokea na kuukaribisha kwa mikono miwili mradi wa kusaidia Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto na kusimimamiwa na AFRICARE utakaotekelezwa katika wilaya za Sumbawanga na Nkasi; Kituo cha Afya cha Mtowisa na Wampembe ambako huduma ya upasuaji itafanyika.

No comments:

Post a Comment