Thursday, March 29, 2012

MKOA WA RUKWA WAPANIA KUHAKIKISHA WANAFUNZI WOTE WALIOFAULU NA KUCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA WANAKWENDA SHULE IFIKAPO MWEZI APRILI MWAKA HUU

Miongoni mwa madarasa mawili yaliyojengwa kwa fedha za Serikali katika Shule ya Kilimani katika Manispaa ya Sumbawanga ambayo yamekwama baada ya kukosekana michango ya wananchi ambapo ni sera ya Serikali kushirikisha wananchi katika miradi hiyo ya maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Manyanya, Diwani Kata ya Katandala Mhe. Kisabwite na wajumbe wa Kikundi Kazi kitachowajibika kuhamasisha wananchi katika uchangiaji katika Kata ya Majengo na Katandala. 

Mkoa wa Rukwa kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo umejipanga kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanakwenda shule kwa kuanza mapambano makali ya kukabiliana na changamoto zinazosababisha tatizo hilo. Hatua hiyo imekuja kutokana na baadhi ya wanafunzi waliofaulu kushindwa kwenda Shule kutokana na upungufu wa vyumba madarasa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Ndugu William Shimwela, jumla ya wanafunzi 678 kati ya wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu Mkoani Rukwa na kuchaguliwa wameshindwa kujiunga na shule walizopangiwa kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa.

Hali hiyo imeusukuma Mkoa kuona kuna haja kubwa ya kuunganisha nguvu kati ya Serikali ya Mkoa, Halmashauri, Serikali za Mitaa ili kuhamasisha wananchi kuchangia kuondokana na tatizo hilo ambalo kimsingi limetokana na muamko hafifu wa wananchi kuchangia miradi hiyo.   

Miongoni mwa hatua zailizoanza kuchukuliwa ni pamoja na Mkoa kuunda Vikundi Kazi (Clusters) viwili vilivyojigawia maeneo ya kuhamasisha, kimoja kikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Injinia Stella Manyanya na kingine kikiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Salum Mohammed Chima ili kuhamasisha wananchi kutambua umuhimu wa miradi hiyo na kuweza kuchangia.

Kazi kubwa ya vikundi kazi hivyo ni kuhamasisha wananchi katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika ujenzi wa vyumba kadhaa vya madarasa ambavyo vimekwama kwenye baadhi ya Shule katika Manispaa ya Sumbawanga baada ya fedha iliyotolewa na Serikali kukosa nguvu na mchango wa wananchi.

Sera kuu ya Serikali ni kutoa fedha kiasi na kuacha sehemu kidogo ya wananchi kuchangia  katika baadhi ya miradi ili kuongeza uwajibikaji wa miradi hiyo kwa wananchi wenyewe. Zimechaguliwa Kata nne za mfano katika Manispaa ya Sumbawanga ambazo ni Majengo. Katandala, Kizwite na Chanji.

Serikali imetoa jumla ya Shilingi milioni 18 kwa Kata mbili za Majengo na Katandala kujenga madarasa manne katika shule ya Kilimani. Mpaka sasa madarasa hayo yameshindwa kukamilika kwa kukosa michango ya wananchi.

Kila darasa moja linategemewa kuchukua wanafunzi 40, hivyo vinahitajika vyumba vya madarasa 16 kuondoa tatizo hilo katika Manispaa ya Sumbawanga ambapo vitawatosheleza wanafunzi 678 walioshindwa kwenda shule kutokana na uhaba wa vyumba hivyo.  

OFISI YA MKUU WA MKOA RUKWA INAOMBA WANANCHI WOTE WENYE UCHUNGU NA ELIMU KUUNGA MKONO JUHUDI ZILIZOANZISHWA NA SERIKALI KUCHANGIA ILI ZOEZI LA UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA UWEZE KUKAMILIKA KWA WAKATI NA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA WAWEZE KWENDA SHULE MARA MOJA. AIDHA OFISI INAPENDA KUWASHUKURU WALE WOTE AMBAO MPAKA SASA WAMECHANGIA. 

  Bwana Elias Bebwa Mkurugenzi Mtendaji wa Seca Contractors akikabidhi shilingi milioni moja kwa Mkuu wa Mkoa Rukwa Injinia Stella Manyanya Ofisini kwake leo kama mchango wake kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Manispaa ya Sumbawanga ikiwa ni jitihada za Serikali ya Mkoa wa Rukwa katika kuhamasisha wananchi na wadau kuchangia katika sekta ya Elimu. Kulia ni Katibu wa Mkuu huyo wa Mkoa Frank Mateny.

No comments:

Post a Comment