Thursday, March 1, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AFUNGA RASMI MAFUNZO YA SIKU NNE YA WAWEZESHAJI KONGANO JIJINI DAR JANA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akihutubia wanawarsha wa mafunzo ya uwezeshaji kongano waliohitimu mafunzo hayo jana katika ukumbi wa BeachComber Hotel Resort jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Dkt. D. Mafunda Kaimu Mkurugenzi Mkuu Tume ya Sayansi na Teknolojia na Injinia Peter Chisawilo Katibu wa PACF - Afrika. Jumla ya wahitimu 46 wamehitimu mafunzo hayo yakiwa na lengo la kukuza uwezo kwa wanawarsha katika kuhamasisha na kuanzisha ushirikiano kati ya sekta binafsi, serikali na wanataaluma katika kongano mahsusi kwenye maeneo mbali mbali hapa nchini. Mafunzo haya yameandaliwa na tume ya sayansi na teknolojia kwa kushirikiana na PACF –Tanzania na ufadhili kutoka Sweden.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akihutubia wanawarsha, Miongoni mwa mambo aliyosisitiza kwa wahitimu wa mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa lengo la mafunzo waliyoyapata linafikiwa kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutumia mafunzo waliyoyapata kuwaelimisha watanzania wenzao ili kuweza kuondokana na lindi la umaskini na kujenga taifa la kijasiriamali.  

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alikabidhi vyeti kwa wahitimu wawezeshaji 46 wa warsha hiyo ya mafunzo ya Kongano yaliyodumu kwa muda wa siku nne kuanzia tarehe 27 Februari hadi tarehe 01 Machi 2012 katika Hoteli ya BeachComber Resort ya Jijini Dar es Salaam.

Wanawarsha na wahitimu wa mafunzo hayo wakifuatilia mada mbalimbali kutoka kwa wawezeshaji wa mafunzo hayo. Washiriki wa mafunzo hayo wanatoka nchi nzima Tanzania Bara na visiwani na zinajumuisha kongano za Asali, usindikaji wa mafuta ya alizeti, uhandisi ,Viungo Zanzibar na Kilimo cha samaki (fish farming), useremala,utalii, Uyoga, ufugaji wa kuku, uchongaji wa sanaa(Wood crafts), na useketaji (Handloom Cluster) na kilimo cha mboga mboga.

Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya na wawezeshaji wa warsha pamoja na wanawarsha wahitimu 46 wa mafunzo ya uwezeshaji wa kongano yaliyofanyika BeachComber Resort jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 27 Januari-01 Februari 2012.

No comments:

Post a Comment