Friday, March 9, 2012

MKUU WA WILAYA YA MPANDA AWAONYA WATENDAJI WALA RUSHWA, ASEMA WATAZITAPIKA


Na  Willy Sumia, Mpanda

SERIKALI wilaya ya Mpanda mkoa tarajiwa wa Katavi imewaagiza watendaji wa kata na vijiji kuwajibika katika maeneo yao ya kazi ili kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Mpanda, Dr Rajabu Rutengwe Machi 9, 2012 katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Mpanda wakati akifunga kikao cha ushauri cha wilaya ya Mpanda DCC.

Mkuu huyo wa wilaya amesema hivi sasa watendaji wengi wamekuwa wakisubiria maagizo katika utendaji kazi wao bila kujali kuwa kutenda kazi zao bila maagizo ni nguzo ya utendaji kazi  wao.

Amesema katika miji mingi wilayani Mpanda uchafu umeendelea kuchukua nafasi kubwa kuliko hali inayotakiwa kwani katika hali halisi hakuna haja ya kuwa na miji michafu wakati kila mji una watendaji wa serikali wanaotakiwa kuwajibika.

Ametoa mfano wa mji wa Ikola kuwa kituo kikuu cha magonjwa wa kuhara na kutapika ugonjwa ambao kimsingi unasababishwa na uchafu hivyo endapo watendaji wataweza kuwajibika na kufanya kazi ipasavyo uchafu ungeondoka wenyewe hata hao wagonjwa wangeeleweka kuwa wametoka mbali.

Ameziagiza serikali za vijiji na kata kuwajibika katika suala la mifugo iliyoingia kiholela katika maeneo yao kwani amesema kuwa taarifa za uhakika zinaelekeza kuwa upo ushahidi wa kutosha kuwa wapo baadhi ya watendaji wa kata na vijiji wamekuwa wakichukua pesa ili kuruhusu mifugo kuingia katika maeneo yao.

“ ndugu zangu nawaeleza kitu kimoja kikubwa ni kuwa waliokula pesa watazitapika maana naagiza au ng’ombe waondoke wewe ubaki au wewe uondoke  ng’ombe wabaki, sina namna lazima uwajibike kwa ng’ombe uliowapokea” amesema mkuu wa wilaya.

Kwa upande mwingine mkuu wa wilaya ameshukuru maafisa mipango wa halmashauri ya wilaya ya Mpanda kwa kufanya vema katika maandalizi ya miradi ya maendeleo inayoleta mafanikio makubwa katika vijiji na kuweza kuondoa kero mbalimbali kwa wananchi wa wilaya yake.

Mkuu wa wilaya ametoa taarifa katika kikao hiki kuwa kuanzia Machi 12, 2012 ataanza ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika kila kata ambapo ataweza kupokea taarifa za miradi, taarifa ya kazi, kukagua miradi na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara katika kila palipo na mradi wa maendeleo.

Mada zilizojadiliwa katika kikao cha leo cha DCC ni pamoja na kupitia mpango na bajeti ya halmashauri ya wilaya ya Mpanda ya mwaka 2012/2013, kupitia mpango wa bajeti ya halmashauri ya wilaya ya Mlele kwa mwaka 2012/2013 pamoja na uzoefu wa nchi ya Japan katika ugatuaji wa madaraka.

No comments:

Post a Comment