Monday, March 12, 2012

SIKU YA WANAWAKE DUNIANI MACHI 8 ILIVYOADHIMISHWA KATIKA HALMASHAURI YA WILAYA YA SUMBAWANGA

Vijana wa kisukuma wakicheza ngoma wakati wa sherehe hizo

Wanawake wa kata ya kipeta wilaya sumbawanga wakicheza ngoma kuadhimisha siku ya wanawake duniani

Afisa maendeleo ya jamii wilaya ya Sumbawanga bi BAHATI MGIMWA akizungumza kwenye maadhimisho hayo

Kijana kisukuma akiwa amechora picha ya ng'ombe katika kiatu chake km ishara ya kuipenda kazi yake ufugaji,hapa akiongoza ngoma

Mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wanawake Scolastica Malocha akiangalia risala ya wanawake baad ya kukabidhiwa

Na Ramadhan Juma-Afisa Habari Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga

TAREHE 8 Machi mwaka huu, Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga Vijijini iliungana na jumuiya nyingine nchini na Dunia kwa ujumla katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa katika tarehe tajwa ya kila mwaka.
Sherehe za maadhimisho hayo katika ngazi ya wilaya hiyo yalifanyika katika kijiji cha Kipeta Kata ya Kipeta ambapo mamia ya wakazi wa Kata hiyo walihudhuria maadhimisho hayo.
Mgeni rasmi katika maadhimisho ya mwaka huu alikuwa diwani wa viti maalum kupitia kata ya Kipeta Scolastica Malocha ambaye ni mke wa Mh. Mbunge wa jimbo la Kwela Ignas Malocha.

Wanawake hao walisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi  ambapo walizitaja changamoto kadhaa ambazo bado zinaendelea kuwa kikazo kwa wanawake wa wilaya hiyo ikiwemo kuachiwa shughuli za kilimo na waume zao kwa kiasi kikubwa huku wakinyanyaswa wakati wa mavuno.
Wanawake hao pia walilalamikia suala la kuzalishwa watoto wengi na waume zao huku wa wakipendekeza wanaume wao kupatiwa elimu ya uzazi wa mpango ili kupunguza hali hiyo.
Katika risala hiyo walisema kitendo cha wanawake kuzalishwa watoto wengi ndio sababu ya wanawake wengi wa vijijini kupata ugonjwa wa Fistula kwa sababu wanazaa maramara na kupoteza nguvu haraka.
Pia walilalamikia vitendo vya wanawake wazee wilayani humo kuuawa mara kwa mara kwa tuhuma za uchawi kwa kigezo cha kuwa na macho mekundu.
Walisema wanawake wengi wazee wamekuwa wakipatwa na matukio ya kuchomewa moto nyumba za wanamoishi hali inayowanya kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao waliyoishi tangu utotoni.
Akijibu risala hiyo mgeni rasmi Scolastica Malocha alikemea kitendo cha baadhi ya watu kujichukulia hatua mkononi na kuwaua wanawake wazee kwa sababu ambao hazina ushahidi na kwamba ni kinyume na sheria huku akiwataka kuacha mara moja vitendo hivyo.
Alisema kitendo cha mzee kuwa na macho mekundu haimaanishi kuwa ni mchawi bali mabadiliko ya kibaolojia ambayo hutokea kwa mwanadamu kutokana na umri wake kuwa mkubwa.
Naye kaimu mkurugenzi wa wilaya ya sumbawanga Crispin Luanda alihutubia umati wa wakazi hao ambapo alisema licha ya  umoja wa mataifa kutenga siku maalum ya kumuadhimisha mwanamke takribani miaka 100 iliyopita, bado wanamke anaendelea kunyanyaswa katika baadhi ya mambo ikiwemo fursa za elimu, afya na hata mgawanyo wa kazi katika familia. 
Kwa upande wake afisa maendeleo ya jamii wa wilaya hiyo Bi Bahati Mgimwa aliwataka wanawake kuzidi kujiamini na kuthubuti kujihusisha na shughuli za kiuchumi ili waweze kujijengea uwezo wa kujitegemea kuliko kumtegemea mwanaume moja kwa moja hali itakayosaidia kupunguza manyanyaso kutoka kwa wanaume wao.

No comments:

Post a Comment