Tuesday, April 24, 2012

ANAYEDAIWA KUWA MTOTO WA STEVEN KANUMBA AIBULIWA SUMBAWANGA MKOANI RUKWA

Mtoto aitwaye Johnson Steven Kanumba  mwenye   umri  wa  miaka   mitatu na miezi  minne juzi   akiwa na mama  yake  mzazi  Paskalia Macha (20)  mkazi  wa kitongoji  cha Bangwe  mjini  Sumbawanga  wakiwa katika eneo la nyumba ya mama yake mzazi na Paskalia katika kitongoji cha Mafulala nje kidogo ya mji wa Sumbawanga. Mama huyo anadai  baba  mzazi  wa mtoto  huyo  ni  msanii maarufu  wa  tasnia   ya  filamu nchini, Steven Kanumba.

Mtoto Johnson Steven Kanumba akiwa amepakatwa na   bibi yake  aitwaye  Viginia Makungu (69) ambaye  ni  mama  mzazi  wa  Paskalia Macha (20) katika  eneo  la  nyumba  ya  bibi   huyo   katika   kitongoji  cha  Mafulala  nje kidogo ya  mji  wa Sumbawanga.

Na Peti Siyame - Rukwa

SAKATA la kujitokeza kwa wanawake wanaodai kuzaa na  aliyekuwa msanii wa filamu nchini, Steven Kanumba, limezidi kushika kasi  baada ya mwanamke mwingine Paskalia Macha (20) mkazi wa kitongoji cha Bangwe  mjini hapa kudai kuzaa na msanii huyo.
  Mwanamke huyo amevuta hisia za wakazi wengi mjini hapa alipojitokeza  hadharani na kudai kuwa mtoto wake wa kiume aliyemzaa miaka mitatu na miezi  minne iliyopita, baba yake mzazi ni Kanumba aliyefariki dunia hivi karibuni.


Kusoma zaidi Bofya Read More chini kushoto kwako

Kanumba alikufa usiku wa kuamkia Aprili 7 na kuzikwa siku tatu baadaye kwenye  makaburi ya Kinondoni.
  Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi nyumbani kwa mama yake mzazi,  Virginia Makungu (69) alimtaja mwanawe huyo kuwa ni Johnson Steven Kanumba.  Paskali ambaye kwa sasa anaishi kinyumba na Giles Mtula (27) mwoka mikate  tangu mwaka jana, tayari ana mtoto mwingine wa kike aitwaye Vero mwenye umri  wa mwezi mmoja.
  Alidai kuwa Johnson alizaliwa katika hospitali ya Mwananyamala Desemba 18,  2008, lakini alipomjulisha Kanumba alimjibu kuwa hiyo ni zawadi pekee  aliyomwachia maishani.

  Akihadithia mlolongo wa maisha yake, alidai kuwa hakuhitimu elimu ya msingi  kwani aliishia darasa la tano na kwa ridhaa ya mama yake mzazi, alimkabidhi  kwa mwanamke aishie Dar es Salaam kufanya kazi za ndani, lakini tajiri wake  huyo ambaye hakutaka kumtaja jina alimpeleka kufanya kazi ya baa Mtoni  Mtongani.
  Alidai kuwa kazi ya baa ilimshinda, hivyo akiwa na mhudumu mwenzake wake kike  walitoroka na kujihifadhi kwa msamaria mwanamke mwingine aliyekuwa akiishi  Gongo la Mboto na kuwa mfanyakazi wake wa ndani.
  Habari zingine zilidai kuwa akiwa anafanya kazi katika baa ya Mtoni Mtongani  alianza uhusiano na Kanumba. “Alijitambulisha kwangu kuwa Steven Kanumba  mwenyeji wa Shinyanga … nilianza naye uhusiano kimapenzi mwaka 2006 nikiwa  msichana mdogo wa miaka 14 na alikuwa akinifuata mara kwa mara Gongo la Mboto  na mwaka 2008 nilipata ujauzito wake.
“Hakunilazimisha kufanya naye mapenzi bali nilimkubalia kwa hiyari yangu  mwenyewe,” alisema. Lakini kwa uchungu mkubwa alidai kuwa alipomfahamisha  kuwa ana ujauzito Kanumba aliukana kuwa hahusiki kwa lolote na ujauzito huo,  ila kama ni kweli basi ni zawadi maalumu kwa maisha yake yote.
“Kaka yangu alikuja Dar es Salaam na kunirudisha Sumbawanga kwa mama yangu  mzazi wakati huo mwanangu alikuwa na umri wa miezi sita nilipofika tu mama  yangu mzazi aliponiuliza nimezaa na nani sikumficha, nilimweleza wazi kuwa  baba wa mtoto ni Kanumba, lakini amemkataa.
 “Mama alinitunza na  mjukuu wake hadi mwaka jana nilipoanza kuishi kinyumba na Giles … sasa tuko  katika mipango ya kumbatiza maana mimi ni Mkatoliki,” alisema.
  Paskalia alidai kuwa ndugu zake wote akiwamo mumewe, aliwafahamisha baba wa  mtoto huyo tangu Kanumba akiwa hai. Hivi sasa anaomba ndugu wa marehemu waje  Sumbawanga wamchukue mtoto wao, kwani anadai ni damu yao halali, ili  wamsomeshe kwa kuwa hana uwezo wa kumsomesha.
“Ninachotaka ni ndugu zake waje wamwone mtoto huyu, ni damu yao halali,  wamsomeshe …kama wana shaka niko tayari mwanangu afanyiwe vipimo vya vinasaba  ili ninayosema yajidhihirishe,“ alisema.
  Giles alipohojiwa alikiri kuishi kinyumba na Mama Johnson tangu mwaka jana na  kwamba alipoanza uhusiano naye, alimweleza bila kumficha kuwa baba mzazi wa  Johnson ni Kanumba.
“Mie mtoto huyu namfahamu kama Johnson Steven Kanumba mtoto wa msanii maarufu  nchini, kwanza sikuamini kabisa lakini nilianza kuamini, kwani kama mara  mbili hivi Kanumba alikuwa akimpigia simu mke wangu akisisitiza kuwa hayuko  tayari kutoa matumizi yoyote kwa Johnson ila eti amempa kama zawadi yake mke  wangu.
“Mara ya mwisho ilikuwa siku mbili hivi kabla hajafikwa na mauti, kauli  ambayo imewachukiza baadhi ya ndugu wa mke wangu, wakiichukulia kauli hiyo  kuwa ni matusi kwao.
“Mke wangu alilia sana baada ya kujulishwa kuwa baba wa Johnson ni marehemu,  kwa kweli aliomboleza kivyake haikuwa rasmi … mie binafsi naamini Kanumba ni  baba mzazi wa Johnson,” alisema baba wa kambo wa Johnson.
 Mama mzazi wa  Paskalia alikiri kuwa binti yake alimweleza kuwa baba wa mtoto huyo ni  Kanumba ambaye baadaye alianza kumwona kupitia filamu alizoigiza.
“Mjukuu wangu Johnson ni mkimya sana wakiwapo wageni, lakini wakiondoka huwa  anaigiza yote, nadhani ana kipaji cha kuigiza kama marehemu baba yake.
“Tulipigwa na butwaa siku moja kabla ya kufariki dunia kwa baba yake, kwani  ilipofika jioni, ghafla alilia huku akigaragara chini mbele yangu akimtaja  baba yake … ndipo kesho yake tukasikia kupitia vyombo vya habari kuwa baba  yake amefariki dunia.” Alisema yeye na wanafamilia wote wako tayari mjukuu  wake huyo afanyiwe vipimo vya kitaalamu ili ukweli ujulikane.
“Mie sikubali mjukuu wangu tumpeleke Dar bali hao ndugu zake waje huku ili  tukubaliane maana sitaruhusu wamchukue mpaka wanilipe fidia kwa mila za  Kifipa kuna malipo ya mama kwa kuwa ameshamwaribu binti yangu, pia kwa kuwa  nimemtunza mtoto wao, lazima wanilipe, ila siko tayari kusema ni kiasi gani  ni mambo ya kujadiliana na kukubaliana,” alisema.
  Johnson alipoulizwa jina la baba yake alitaja Steven Kanumba hata  alipooneshwa picha ya marehemu na kutakiwa amtambue ni nani kwa mastaajabu ya  wengi alimwonesha akisema, “huyu ni baba yangu.”
Ndugu wakiwamo kaka za mama wa Johnson walikiri kwamba aliwajulisha kuwa baba  mzazi wa Johnson ni Kanumba mara aliporejea hapa mtoto huyo akiwa na umri wa  miezi sita.
“Kwanza sikuamini baadaye nilipobaini kuwa baba wa Johnson ni Steven Kanumba  mwigizaji maarufu wa filamu nilipokuwa nikimwona akiigiza katika runinga.  Dada (Paskalia) alinijulisha hayo mwaka 2010,“ alisema Humphrey Kalulu (16)  mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Sekondari ya Chanji mjini humo, ambaye  alijitambulisha kuwa ni binamu wa Paskalia.
  Hata hivyo, baadhi ya ndugu wa Paskalia akiwamo binamu yake aitwaye Godfrey  Makungu, hawako tayari ndugu wa Kanumba kumchukua Johnson kwa kile wanachodai  kuwa marehemu katika uhai wake alimkana mtoto huyo hivyo walikwenda mbali  hata kumlazimisha Paskalia akatae Kanumba kuwa baba mzazi wa Johnson.
  Habari za ndani kutoka familia hiyo zilidai kuwa baadhi ya ndugu wa Paskalia  wakiongozwa na Godfrey, waliandaa mipango ya kumpeleka Paskalia na Johnson  Namanyere wilayani Nkasi wakaishi huko ikiwa ni jitihada za kumficha mtoto  huyo ili asichukuliwe.
 Wakazi wengi wa  hapa na kwingineko wamekuwa na maoni tofauti, wengi wakitaka mtoto huyo  afanyiwe vipimo vya vinasaba .
“Miye naomba ndugu wa marehemu Kanumba waje wamshuhudie mtoto huyu kwa kweli  anafanana na baba yake, ili kama wana shaka basi vipimo vya DNA vitumike  kubaini haya … maana limekuwa kwa wengine kama fumbo, basi ni lazima  liteguliwe kama ni kweli basi wasimnyime ndugu yao fursa ya kumpa elimu, “  alisema Afred Manyika, mfanyabiashara maarufu mjini hapa.

5 comments:

 1. Huge body, ni kweli nchi itajengwa na wenye nchi sisi wananchi wa Mkoa wa Rukwa/Katavi lazima tupigane kuhakikisha Mkoa unatoka kimaendeleo

  ReplyDelete
 2. Ahsante sana kutuhabarisha just keep it up Mwanahabari na mawasiliano.Monica

  ReplyDelete
 3. I am so glad to read your wonderful article. Im looking forward to read more of
  your works and posts. You did a good job! Try to visit my site too and enjoy.

  triciajoy.com

  www.triciajoy.com

  ReplyDelete
 4. I am so glad to read your wonderful article. Im looking forward to read more of
  your works and posts. You did a good job! Try to visit my site too and enjoy.

  triciajoy.com

  www.triciajoy.com

  ReplyDelete