Tuesday, April 3, 2012

HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA RUKWA MHE. INJINIA STELLA MARTIN MANYANYA WAKATI WA MAKABIDHIANO YA MKOA MPYA WA KATAVI TAREHE 31 MACHI 2012 MJINI MPANDA

Mhe. Dkt. Rajabu Mtumwa Rutengwe, Mkuu wa mkoa wa katavi,
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mpanda, na vyama vingine vya siasa,

Wahe. Wabunge,

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Rukwa na Katavi,

Viongozi wote wa Serikali wa mikoa ya Rukwa na Katavi,
Viongozi wa Dini,
Watumishi wote wa wa Serikali na Taasisi Binafsi,
Waandishi wa habari,
Wananchi wote Mabibi na Mabwana,
Tumsifu Yesu Kristo, Asalaam Aleykhum.
Mhe. Mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Katavi,
ndugu yetu Dkt. Rajabu Mtumwa Rutengwe, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Rukwa mpya na mkoa wako wa Katavi, pia kwa niaba yangu mimi mwenyewe kukupongeza sana wewe pamoja na familia yako kwa kuonekana mbele ya chaguo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho kikwete, na hivyo kukuteuwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa kwanza wa Katavi kuanzia tarehe 15 mwezi Machi, 2012.

Mhe. Mkuu wa mkoa wa Katavi,
Kwa mara nyingine tena napenda kumpongeza Katibu Tawala wa kwanza wa Mkoa wa Katavi Eng. Emmanuel Kalobelo kwa nafasi hiyo adimu aliyoipata kufuatia kuteuliwa kwake na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kushika wadhifa huo.
Mhe. Mkuu wa mkoa wa Katavi,
Ama kweli, haki ya mtu hailiwi, na mcheza kwao hutuzwa. Mlifanya kila liwezekanalo kuisaidia wilaya ya Mpanda ambayo sasa ni mkoa wa katavi, ili ipige hatua mbele kimaendeleo. Nayo haijawasahau, wanakatavi wamepiga la mgambo wakiwemo machifu wetu, Chifu Beda, Kayamba na wenziwe walisema nanukuu, “Tunaomba msituhamishie hawa watu wetu, ikibidi muwaboreshe tu”, Mheshimiwa Rais wetu amewasikia, na leo mmefikia hapo mlipo!.
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Katavi,
Hilo ni fundisho katika maeneo mengi ya kiutendaji. Kwanza kwa mtumishi yeyote popote alipo, ni vema afanye vizuri kwenye nafasi yake, kwani hajui malipo ya baadaye, pengine nafasi hiyohiyo ndiyo itakayomwinua.
Mhe. Mkuu wa mkoa wa Katavi,
Napata furaha zaidi kwa sababu naamini nami ni sehemu ya mafanikio hayo. Kwani Mkoa wangu wa Rukwa mama, kwanza ulipata Mheshimiwa Waziri Mkuu, sasa “umejifungua” mkoa wenyewe wa Katavi, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Katibu Tawala wa Katavi na Inshallah, Tutaendelea kuwapata wengi zaidi. Tuzidi kuomba Mungu. 
Mhe. Mkuu wa mkoa wa Katavi,
Naomba upokee taarifa ya inayoeleza mambo ya kiujumla kuanzia ukurasa wa 1 hadi 5. Pamoja na Taarifa hii maelezo mengine ya kina ya kiutendaji utayapata katika taarifa rasmi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Alhaji Salum Chima. Tafadhali uzipitie taarifa hizi kwa umakini wakati umetulia, na jambo lolote lenye utata nitaomba tuwasiliane. Hata hivyo kuna mambo machache ambayo ni vema kuyatamka sasa;
1.  Ninakukabidhi mkoa wako ukiwa katika hali shwari, pamoja na matukio machache ya uhalifu ambayo hujitokeza mara mojamoja, hivyo hayapaswi kupuuzwa kwani yana athari kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
2.  Mkoa kupitia Halmashauri zake umeendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa nguvu zote.
3.  Kuna suala la kuendeleza mahusiano kati ya mkoa wa Rukwa mpya na Katavi (UMARUKA), ni muhimu na ni matarajio yetu kuwa tutaendeleza.
4.  Tarehe 17 Mwezi Oktoba 2011, Mkoa wa zamani wa Rukwa kwa kushirikiana na mkoa wa Kigoma ulifanya Kongamano kubwa la Uwekezaji wa Kanda ya ziwa Tanganyika mjini Mpanda, Kongamano ambalo lilivuta hisia na kuhudhuriwa na watu wengi mashuhuri wakiwemo Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na (Mwana Katavi), Mhe. Dkt. Mary Nagu Waziri Ofisi ya Rais Uwezeshaji na Uwekezaji, Wabunge, Viongozi wa Vyama vya siasa, Mabalozi 34 kutoka nchi mbalimbali, Wakurugenzi wa mashirika mbalimbali na Wakuu wa Taasisi za Umma na binafsi, Wajasiriamali pamoja na wananchi wa makundi yote kwa ujumla wake kwa waume.
5.  Kufuatia kongamano hilo kuna maamuzi ambayo ni vema sasa Mikoa yote miwili yaani Rukwa na Katavi iyazingatie kama ilivyo kwenye maazimio yetu.
6.  Kufuatia Tamasha la Utamaduni wa wana Rukwa na Katavi, iliazimiwa Mikoa yetu itenge maeneo kwa ajili ya kuanzisha makumbusho na kuendeleza mila na desturi za makabila ya Mikoa husika.
7.  Kuendeleza juhudi zilizokwishaanza za ujenzi wa Chuo Kikuu cha Katavi.
8.  Kuendeleza mahusiano ya karibu kati ya uongozi wa Mkoa na wananchi wetu.
9.  Kuendelea kuimarisha miradi ya mwamapuli, kituo cha Afya cha Inyonga na miradi yote mikubwa iliyokuwa katika hatua za utekelezaji katika mkoa wa katavi.
10.             Kufuatia maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhakikisha kuwa Wilaya zinakuwa na wataalamu wa nyuki na kuendeleza utalii.
11.             Kuendeleza Uhifadhi wa mazingira pamoja na ufugaji wenye tija ikiwemo Mpango wa matumizi bora ya ardhi.
12.             Kuendeleza Kilimo Kwanza na kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati, na kukuza kilimo cha kisasa ikiwemo kutumia matrekta, plau na kuongeza thamani mazao pamoja na kutafuta masoko.
13.             Kufuatilia kwa karibu Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kizi, Kibaoni mpaka mwanzo wa Mbuga za Katavi, na kisha mwisho wa mbuga za katavi, stalike hadi mpanda. Pia kufuatilia kwa karibu upembuzi yakinifu wa eneo hilo na kuona umuhimu wa kuhusisha bonde la mpimbwe kupata barabara ya kiwango cha lami kutokana na sifa yake ya uzalishaji wa chakula ikiwemo mpunga.
11       Kufuatia Ziara ya Mheshimiwa makamu wa Rais kuandaa maeneo yanayohitaji kupata umeme wa solar kama Vile hospitali ya Inyonga n.k na apelekewe mara moja ili aweze kutusaidia kupata ufadhili wa miradi hiyo kama alivyotuelekeza kupitia barua yake yenye kumbukumbu
no. SH/VP/CAB 276/278/01.
14.             Kufuatilia Uboreshaji wa barabara ya Mpanda -Inyonga hadi Koga ambayo        upembuzi yakinifu upo hatua za       mwisho na kutafuta        ufadhili, pia ahadi ya   mheshimiwa Makamu wa Rais ya    kusaidia kupata ufumbuzi wa barabara hiyo.
15.             Kikundi cha ngoma ya askari cha inyonga       kupatiwa        uniform
16.             Mlemavu wa Mwamapuli kupatiwa bati 20
17.             Kuendeleza vikao vya Ujirani mwema na mikoa      ya jirani        Tabora, Kigoma, mikoa ya wafugaji    na Shimyanga, Mwanza, Shimiyu, Geita na ya   mpakani Kagera na Mara.
18.             Kuendelea kushughulikia suala la Wakimbizi   waliomo katika mkoa wa katavi na kulipatia      ufumbuzi kwa kuhusisha ngazi za juu.
19.             Kuendelea kuhakikisha watoto wote waliofaulu      wanajiunga na kidato cha kwanza.
20.             Kuweka ratiba maalum pamoja na mikakati kwa ajili ya Uzinduzi rasmi wa mkoa wa Katavi, pamoja na mambo mengine muhimu kama vile Ofisi ys Mkuu wa mkoa wa Katavi, Uwanja wa ndege, Tathmini ya uwekezaji, Baraza la uwekezaji na one stop centre ya uwekezaji na kadiri itakavyoonekana inafaa kwa manufaa ya Mkoa wa Katavi na Taifa kwa Ujumla.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi,
Kwa namna ya pekee, napenda kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. J. K. Kikwete Kwa kuniwezesha mimi mwanamke kushika nafasi hii nyeti ya uongozi. Pia Namshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharb Bilal ziara yake ilituwezesha kupata ufumbuzi wa mabo mengi ikiwemo tatizo la umeme kwenye maeneo yasiyo na umeme, Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda(MB) kwa kutuongoza na kutusaidia kila wakati katika kutekeleza majukumu ya Mkoa wetu wa Rukwa na hivi Kutuwezesha Leo Kupata Mkoa wa Katavi. Pia nawashukuru Wakuu wa Mkoa wa Rukwa pamoja na Viongozi wengine wa Chama Tawala na Serikali walionitangulia kwani waliweka Msingi Imara. 
Napenda kukushukuru wewe mwenyewe, kwa jinsi ulivyonipa ushirikiano wakati ukiwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda pamoja na Katibu Tawala wa Katavi wakati akiwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpanda kwa ushirikiano wa hali ya juu mlionipa na kuwezesha kazi zangu kuwa rahisi, hasa katika eneo la wilaya ya Mpanda ambayo sasa ni Mkoa wa Katavi. Namshukuru Pia Mwenyekiti wa Chama Tawala (CCM) Mkoa, Ndugu H. Matete kwa ushirikiano mkubwa aliotoa kwetu. Aidha napenda kumshukuru sana Katibu Tawala Wa Mkoa wangu wa Rukwa mpya Alhaji Salum Chima, pamoja Kamati yetu ya ulinzi na Usalama, na ninaomba niwatambue kama ifuatavyo:
1.  Mhe. Joyce Mgana (DC Nkasi)
2.  Mhe. Kanali John Mzurikwao (DC Sumbawanga)
3.  Alphonce Hamis (RSO)
4.  Isuto D.Mwantage (RPC) na Kaimu wake Mwaruanda
5.  Wilson R. M Bambanganya (RIO)
6.  Gasto A. Mkono (TAKUKURU)
7.  Lt Kanali Jonathan B. Shayo (MMM)
8.  ASCP George Kiria (RPO)
 
Nawashukuru sana watumishi wote wa Serikali pamoja na Wadau wote wa Maendeleo wa Mkoa wa Rukwa bila kuwasahau Waandishi wa habari.
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Katavi,
Naomba niwashukuru wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa na Katavi Kwa Ushirikiano mliouonyesha kwangu katika kipindi chote toka nilipoteuliwa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kushika wadhifa huu wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambao tarehe 1/3/2012 umegawa eneo na kuwa Rasmi Mkoa wa Katavi.  
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi,
Kwa kuwa sio rahisi kuyataja mambo yote hapa au yamkini kuwashukuru wote hapa, nikiri tu kwa kusema nakuamiri kwa uwezo wako uliotukuka na hakika kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu hakuna litakalokushinda. 
Asanteni sana na Mwenyezi Mungu azidi kutubariki.
Mha. Stella Martin Manyanya (MB)
MKUU WA MKOA WA RUKWA

No comments:

Post a Comment