Thursday, May 17, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AWAAPISHA WAKUU WAPYA WA WILAYA MKOANI HUMO LEO NA KUWAPA MAAGIZO 16 YA KUAZA KUFANYIA KAZI

 Mkuu Mpya wa Wilaya ya Sumbawanga Mathew S. Sedoyeka akila kiapo cha utii mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya leo katika ukumbi wa Ikulu ndogo katika Manispaa ya Sumbawanga baada ya uteuzi wa hivi karibuni wa Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kushika madaraka hayo kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali John Antonyo Mzurikwao. 
 Mhe. Sedoyeka akisaini kiapo hicho mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Stella Manyanya.

 Mkuu wa Wilaya mpya ya Kalambo Luteni Edward O. Lenga akila kiapo cha kuiongoza Wilaya hiyo mpya mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mkuu wa Wilaya wa Kwanza wa Wilaya hiyo mpya iliyomegwa kutoka katika Wilaya ya Sumbawanga.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akimkabidhi kitendea kazi Mkuu wa Wilaya mpya ya Kalambo Luteni Edward Lenga ambayo ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atayoitumia kama muongozo wa shughuli zake za kila siku awapo madarakani.

 Mkuu mpya wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta akila kiapo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya leo katika ukumbi wa Ikulu ndogo Mkoani Rukwa. Mkuu huyo wa Wilaya maechukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Joyce Mgana baada ya uteuzi wa hivi karibuni wa Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akisaini hati ya kiapo cha Mhe. Iddi Kimanta baada ya kuwaapisha wakuu wote watatu wa Wilaya za Sumbawanga, Kalambo na Nkasi.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Francis Kilawe akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kutoa neno baada ya kuwaapisha wakuu hao wa Wilaya.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akihutubia washiriki waliohudhuria hafla hiyo ya kuwaapisha wakuu wapya wa Wilaya za Mkoa wa Rukwa. Katika hotuba yake hiyo alitoa maagizo 16 kwa Wakuu hao wa Wilaya na kuwataka wayafanyie kazi kwani ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoukabili Mkoa wa Rukwa. Maagizo hayo yanapatikani chini kwenye Hotuba ya Mkuu huyo wa Mkoa.

Hotuba ya Mkuu wa Mkoa iliyokuwa na maagizo 16 kwa Wakuu wa Wilaya waloapishwa. Kuisoma shuka hadi mwisho wa Post hii.

 Mkuu mpya wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta akitoa neno lake la salamu katika hafla hiyo. Alisema kuwa kuja kwake Rukwa ni kwa ajili ya kuwatumikia wananchi kwa uwezo wake wote na si vinginevyo. Alitoa kaulimbiu yake mpya ya Wilaya yake ya Nkasi kuwa ni"Nkasi Kasi zaidi". Aliendelea kusema kuwa "Mimi ni kamisaa wa Chama cha CCM ndani ya Wilaya yangu ya Nkasi" Aliahidi kutekeleza itikadi za Chama cha Mapinduzi katika kuleta maendeleo Wilayani humo.


 Iddi Kimanta akihutubia kwenye hafla hiyo baada ya kuapishwa.

 Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mathew S. Sedoyeka akitoa salamu zake mara baada ya kuapishwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo baada ya uteuzi wa hivi karibuni wa Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuiongoza Wilaya hiyo. Alisema kuwa hakuja Mkoani Rukwa kufanya biashara bali kuwatumikia wananchi.

 Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Luteni Edward O. Lenga akitoa salamu zake baada ya kuapishwa. Aliahidi kuafanya kazi bila maneno mengi.

 Baadhi ya watumishi katika Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa wakifuatilia matukio katika hafla hiyo.

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ikiongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Sunto Mantage(Nyuma) walikuwepo kushudia tukio hilo la kihistoria. Wakwanza kushoto ni Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu katika Sekretarieti ya Mkoa Rukwa Samson Mashalla, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Kanali John Antonyo Mzurikwao, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Joyce Mgana na Mkuu mpya wa Wilaya ya Sumbawanga Mathew S. Sedoyeka.

Sehemu ya washiriki wa hafla hiyo ya kihistoria ambayo walikuwepo viongozi mbalimbali wa Serikali, Viongozi wa Dini, wananchi na wagani mbalimbali walioalikwa pamoja na waandishi wa habari.

Ukumbi haukutosha hali iliyowalazimu baadhi ya wahiriki wa hafla hiyo kusimama nje ya ukumbi huo uliokuwa wazi kuwawezesha kushuhudia tukio zima la uapisho bila chenga.

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mathew S. Sedoyeka  akimtambulisha binti yake aliyemsindikiza kabla ya kula kiapo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akishiriki kwenye ngoma na kikundi cha Kanondo kilichokuwepo kuburudisha hafla hiyo.

Washiriki mbalimbali ndani ya ukumbi.

Dua za viongozi wa Dini nazo hazikusahaulika.

Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya wa pili kushoto na Wakuu wa Wilaya wapya, Kutoka kulia ni Wilaya ya Sumbawanga Mathew S. Sedoyeka, Iddi Kimanta (Nkasi) na Luteni Edward O. Lenga (Kalambo).

Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya wa tatu kushoto, Wakuu wa Wilaya wapya za Sumbawanga Mathew S. Sedoyeka wa kwanza kulia, Luteni Edward O. Lenga (Kalambo) wa kwanza kushoto na Iddi Kimanta wa tatu kulia (Nkasi) na Wakuu wa Wilaya waliomaliza muda wao Kanali John Antonyo Mzurikwao wa pili kutoka kushoto (Sumbawanga) na Mama Joyce Mgana wa pili kutoka kulia (Nkasi)

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na Wakuu wa Wilaya waliomaliza muda wao na kushindwa kuteuliwa tena kwa sababu mbalimbali ikiwepo umri.

Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Wakuu wapya wa Wilaya na viongozi wa dini.

Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Wakuu wapya wa Wilaya Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Sabas Katepa wa pili kulia na Naibu Meya Aurelia Knyengele wa tatu kushoto.

HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA RUKWA WAKATI WA KUWAAPISHA WAKUU WA WILAYA ZA SUMBAWANGA, KALAMBO NA NKASI LEO TAREHE 17 MEI 2012 KATIKA VIWANJA VYA IKULU NDOGO YA SUMBAWANGA

Mhe. Mathew Sarja Sedoyeka, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Edward Ole Lenga, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo,
Mhe. Iddi Hassani Kimanta, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi,
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, na vyama vingine vya siasa,
Waheshimiwa Wabunge,
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Rukwa,
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya wastaafu,
Viongozi wote wa Serikali wa mkoa wa Rukwa,
Viongozi wa Dini,
Watumishi wote wa wa Serikali na Taasisi Binafsi,
Waandishi wa habari,
Wananchi wote, Mabibi na Mabwana,
Tumsifu Yesu Kristo, Asalaam Aleykhum, Yamposuta.
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutujalia uzima, kukusanyika leo na kushuhudia tukio hili muhimu la kihistoria la Wakuu wa Wilaya wapya kuapishwa katika kushika madaraka yao.
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kwa kuteuliwa kwenu na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Tanzania kushika nafasi hizi za Ukuu wa wilaya katika Mkoa wa Rukwa. Naamini Dola imewachuja miongoni mwa watanzania wapatao milioni arobaini na tano na kuona mnanafaa. Mmepewa heshima kubwa ambayo mna kila sababu ya kuifanyia kazi inayolingana na thamani yake.
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Napenda pia kuwashukuru Wakuu wa Wilaya waliomaliza muda wao kwa ushirikiano mkubwa walionipa katika kipindi chao chote cha uongozi nikiwa pamoja nao takriban miezi tisa sasa, walikuwa mahiri kwa kazi zao, walifanya kazi kwa bidii bila kuchoka, kwa uzalendo mkubwa tumeshirikiana katika mambo mengi, nitawakumbuka hasa kwa utii wenu katika maagizo niliyokuwa nikiwapa. Ninaamini yawezekana hawakuweza kuteuliwa tena kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo ikiwemo umri. Hata hivyo Nchi yetu bado itaendelea kuwahitaji na kuwatumia katika baadhi ya maeneo yetu.
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Leo ni siku ya kusherekea, lakini pamoja na hayo naomba niwape matarajio ya wananchi wa mkoa wa Rukwa, wanakutegemeeni sana kuwapa uongozi ulio karibu nao kwa kuwashirikisha, kuzifahamu kero zinazowahusu na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka na wa kudumu. Nyinyi sio Malaika wa kuweza kufanya kila kitu, lakini mahali juhudi ilipofanyika panajulikana. Nawaombeni kutoka ofisini na kuwafuata watu waliko.
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Kwa kuwa Nchi yetu inakabiliwa na changamoto za aina mbalimbali, mojawapo ikiwa ni suala la ongezeko idadi ya watu, ujinga, maradhi na mahitaji ya kukuza uchumi, ikiwemo ardhi na mazingira, siasa safi na uongozi bora, sisi ndio vinara tuliokabidhiwa na Mheshimiwa Rais kwa niaba yake ni lazima tutimize wajibu wetu.
Kwa hali yoyote ile tusiitake wala kuivumilia rushwa, kwetu wenyewe wala kwa watumishi wetu, tusioneane haya, wala majibu yasiyoeleweka pale tumapoona dhahiri kuna ubadhirifu wa mali ya umma au kujaribu kuyumbisha huduma kwa wananchi, tuchukue hatua zinazostahili bila kusita.
Katika suala la amani, wengi wanajaribu kulinganisha siasa zao wakimwenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, lakini wakati huo huo wanachochea migogoro katika jamii, migongano na wakati mwingine kusababisha uvunjifu wa amani, kuwakataza watu kujitolea katika shughuli za maendeleo n.k.
Mwalimu hakufanya hivyo hata kidogo, hayo kwake yalikuwa ni mwiko. Na alichukuwa hatua mara moja kwa wale wanaokiuka haki na misingi. Kama sisi ni waumini wa Mwalimu tutayafanya aliyokuwa anayataka na kuyafanya Mwalimu.
Tumedhamiria kuona Rukwa inakuwa Salama, vitendo vya kikatili vinavyoendelea hasa kipindi cha mavuno kwa kuwaua wenzao kwa kisingizio cha imani za kishirikina, huo ni ujambazi tu sawa na mwingine wowote ule lazima tufuatilie kwa karibu, tutoe elimu na kuwachukulia hatua kali za kisheria wote. Na wananchi watusaidie kutoa taarifa.
Mkoa wetu ni mkoa wa kilimo na Ghala la chakula linalotegemewa kitaifa. Tuhakikishe wakulima wanafikishiwa huduma zinazostahili kwa wakati.
Maagizo muhimu ya kuanzia 
1.  Kukuza na kuimarisha Ushirikiano miongoni mwa wadau wote.
2.  Kusimamia kwa karibu zoezi  la mchakato wa marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuhakikisha kuwa linaendeshwa kwa uhuru, uwazi na amani.
3.  Suala la Usimamizi wa matumizi ya pesa za serikali, sitaki kusikia hati chafu kutoka katika mkoa wangu na halmashauri zake. Nawapongeza kwa mwaka huu mkoa wetu ulikuwa safi.
4.  Kutambua na kuziendeleza fursa za kiuchumi ikiwemo Utalii, uwekezaji katika sekta ya madini na nishati, biashara, viwanda na maeneo yote kama miongozo mbalimbali ya nchi inavyotaja.
5.  Usafi wa Mazingira ni agenda ya kudumu, kila mkazi au taasisi lazima ihakikishe kuwa maeneo yao yanayowazunguka ni safi. Sumbawanga Ng’ara na Halmashauri zake zote Ng’ara.
6.  Rukwa salama- Mradi wa kujitolea katika ujenzi wa nyumba za Askari polisi upewe nsukumo katika Manispaa na Halmashauri zote.
7.  Kuendelea na kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ili watoto wote wanaochaguliwa kuingia kidato cha kwanza waweze kupata nafasi.
8.  Kufuatilia kwa karibu zoezi la Sensa ya Taifa itakayofanyika tarehe 26 Augasti 2012 ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau katika kutoa elimu.
9.  Kupanga mikakati ya kuwaendeleza kielimu viongozi wa ngazi ya chini ikiwa ni pamoja na watendaji wa vijiji na wenyeviti wa vijiji hasa katika elimu ya uongozi.
10.             Kuhakikisha kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala - Chama cha Mapinduzi ya 2010, pamoja na Sera zake zinatekelezwa kikamilifu ikiwemo kusimamia ujenzi wa barabara katika maeneo yetu.
11.             Kutambua kuwa Msingi wa Itikadi ya chama cha Mapindizi, na katiba ni Watu, hasa wanyonge, wakulima na wafanyakazi ni muhimu sana kuwa nao jirani ili kujua wanasema nini, kero zao nini, na kupata ufumbuzi wa pamoja.
12.             Kuhakikisha kuwa Ajira ni kazi yoyote ile halali inayompatia my kipato. Nawaomba Vijana wa vijiwe wasisumbuliwe, vijana wa Bodaboda wasisumbuliwe, wafanyabiashara ndogondogo wasisumbuliwe. Wapangwe, wapewe elimu ya ujasiriamali, watengewe maeneo ya kazi ili mradi nao pia wathamini ofisi zao, yaani mahali walipo pawe safi.
13.             Tujitahidi kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kutenga maeneo ya shughuli hizo.
14.             Wilaya ya Nkasi na Kalambo kuhakikisha kuwa kwa njia ya kujitolea Tunajenga mahakama za wilaya ili kuondoa kero ya kufuata huduma hiyo sumbawanga.
15.             Kufutilia kwa karibu hali ya usalama wa mwambao wa ziwa Tanganyika
16.             Wilaya ya Kalamba kuhakikisha kuwa soko la samaki la Kasanga linapata umeme.
Mwisho nizide tena kumshukuru Mheshimiwa Rais Kwa kuniteulia ninyi waheshimiwa wakuu wa wilaya ilitusaidiane katika gurudumu hili la maendeleo. Nawashukuru pia wananchi wote kwa kujitokeza kwa wingi katika shughuli hii muhimu ya leo.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
Eng. Stella Martin Manyanya (Mb)
MKUU WA MKOA WA RUKWA

No comments:

Post a Comment