Monday, May 21, 2012

WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA AWATAKA MA-RC NA MA-DC KUJITOA ZAIDI KATIKA KUTAFUTA SULUHISHO LA MATATIZO YA WANANCHI NA SIO KUWA SEHEMU YA MATATIZO HAYO

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia (kushoto) na Waziri wa Zamani na mwanasiasa mkongwe, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru katika Kikao cha Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa kwenye Kituo cha mikutano cha St. Gaspar Mjini Dodoma May 21,2012. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
 
Waziri wa zamani na Mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale Mwiru akitoa mada katika Kikao cha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Makatibu Tawala wa Mikoa kwenye Kituo cha Mikutano cha St.Gaspar Mjini Dodoma May 21, 2012.
 
Baadhi ya washiriki wa Semina ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati alipofungua kikao chao kwenye Kituo cha Mikutano cha St. Gaspar Mjini Dodoma May 21, 2012.
 
 
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala na Wakuu wa Wilaya wote nchini wajitoe zaidi katika kutafuta suluhisho la matatizo yanayowakabili wananchi wanaowaongoza badala ya wao pia kuwa sehemu ya matatizo hayo.
Ametoa wito huo leo (Jumatatu, Mei 20, 2012) wakati akifungua mafunzo maalum ya siku 10 kwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala na Wakuu wa Wilaya yanayoanza leo kwenye ukumbi wa St. Gaspar mjini Dodoma.

Akinukuu maneno ya hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere, Waziri Mkuu alisema: “Kiongozi anayetakiwa kwa Taifa letu, lazima awe anakerwa na matatizo ya wananchi” na kwa maana hiyo anatarajia kuwa viongozi hao watakuwa viongozi wa aina hiyo baada ya kumaliza mafunzo hayo.

“Ninyi kama viongozi na watendaji wakuu katika maeneo yenu ni timu muhimu katika kufahamu changamoto, matatizo na kero walizonazo wananchi hasa wale wanaoishi vijijini ambao ni asilimia 80 ya Watanzania wote,” alisema.

Alisema ili kuwasaidia wananchi kuondokana na umaskini, viongozi hao wanategemewa kuonesha njia ya nini kifanyike ili kukabiliana na changamoto na malalamiko ya wananchi.

“Mnapaswa kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayowakabili badala ya kuwa sehemu ya matatizo yao. Ili muweze kuyafanikisha haya yote sharti kila mmoja wenu atambue na kukubali kuwa uongozi ni kufanya kazi zaidi na kwa hiyo mnapaswa kujitolea zaidi kwa umma na wala siyo nafasi ya kujinufaisha binafsi au kuona mmpata ofisi ya kupiga mbwembwe,” alisisitiza.

Aliwataka mara baada ya kumaliza mafunzo haya, awe ni Mkuu wa Mkoa au wa Wilaya, kila mmoja mmoja anapaswa kujiuliza kuna kiwango gani cha umaskini katika eneo aliliopangiwa; aangalie pia pato la wastani la mwananchi katika wilaya au mkoa wake likoje na kuainisha kama ongezeko la idadi ya watu katika mkoa au wilaya yake linaendana na ukuaji wa uchumi katika eneo husika.

“Mnapaswa pia kuzijua na kuzitambua fursa za kiuchumi zilizopo ndani ya mkoa au wilaya husika; mziainishe ni fursa zipi za kuichumi za haraka (quick wins) zinazoweza kumtoa mwananchi kwenye umaskini; na zaidi ya yote muangalie ni kwa namna gani mwananchi wa kawaida atawezeshwa kutumia fursa zilizopo kuondoa umaskini unaomzunguka,” aliongeza.

Alisema wanatakiwa kuhakikisha kuwa maeneo yao yanakuwa na miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa viwango stahiki na kwamba thamani ya fedha inaonekana. Vilevile alisisitiza kuwepo kwa nidhamu katika ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za umma na kujiridhisha kuwa zinatumika kwa manufaa ya wananchi.

“Ninawasihi sana Wakuu wa Mikoa na Wilaya mkasimamie vizuri ukusanyaji wa mapato kwenye halmashauri zenu kwa sababu ndiko viliko vyanzo vikuu vya mapato. Katika bajeti iliyopita, Halmashauri zilipanga kukusanya sh. bilioni 320/- lakini hadi kufikia Januari mwaka huu, ni sh. bilioni 90/- tu ambazo zilikuwa zimekusanywa.”

“Ni lazima RC na DC mlione hili… lazima muweke mbinu za kufuatilia ukusanyaji wa mapato katika mamlaka zenu za Serikali za Mitaa ili kusaidia kuleta maendeleo katika maeneo yenu kwa kutumia vyanzo mlivyonavyo,” alisisitiza.

Akifafanunua kuhusu majukumu ya jumla ya viongozi hao, Waziri Mkuu aliwataka wakapambane na rushwa, dawa za kulevya, tatizo la ajira kwa vijana na kuhakikisha kuwa mikoa na wailaya zao zina akiba ya chakula cha kutosha.

“Ni aibu kwa RC au DC kuomba chakula kwani si kweli kwamba hapakuwa na fursa nyingine za kuepuka hali hiyo. Fursa za kuzalisha mazao mbadala zipo, himizeni watu wenu walime mazao yanayostahimili ukame, yanayokomaa kwa muda mfupi, na ikibidi muwasisitize wazalishe chakula cha ziada ili wawe na akiba ya kutosha na pia waweze kuuza na kupata fedha,” aliongeza.

Aliwataka wahimize dhana ufugaji nyuki katika maeneo ya kilimo na ufugaji ambako wamepangiwa kwani ni eneo ambalo halijapewa msukumo licha ya kuwa lina fursa kubwa ya kuongeza kipato kwa wananchi wanaowaongoza.

“Wasaidieni wananchi kuongeza kipato kwa kujiingiza katika ufugaji nyuki… bei ya asali inapanda kila siku. Ethiopia ni nchi ya jangwa lakini wenzetu wamefika mbali kiuchumi kutokana na ufugaji nyuki na urinaji asali,” alifafanua.

Mafunzo hayo yanahudhuriwa na Wakuu wa Mikoa 24, Makatibu Tawala wa Mikoa 25 na Wakuu wa Wilaya 133. Jumla ya watoa mada 39 wanatarajiwa kutoa mada katika mafunzo hayo wakiwemo mawaziri 17.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 998,
DODOMA.
JUMATATU, MEI 20, 2012.
 

No comments:

Post a Comment