Friday, December 14, 2012

HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA RUKWA KWENYE KIKAO CHA UFUNGUZI WA KIKAO CHA UHAMASISHAJI WA MKAKATI WA MAWASILIANO YA MABADILIKO YA TABIA KATIKA KUPAMBANA NA MALARIA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akisoma hotuba ya ufunguzi wa kikao cha uhamasishaji wa mkakati wa mawasiliano ya mabadiliko ya tabia katika kupambana na Malaria kilichofanyika jana kwenye ukumbi wa mkutano wa Libori Centre wilayani Sumbawanga.
 
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Katavi Dkt. Yahya Hussein akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kufungua kikao hicho.

Mwenyekiti wa asasi  ya RODI akitoa maelezo mafupi na madhumuni ya kikao hicho mgeni rasmi ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
 
Picha ya pamoja ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na washiriki wa kikao hicho.
 
Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa na Katavi,
 
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na Katavi
Wataalamu na Watendaji kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
Wakurugenzi wa Halmashauri  za Mkoa wa Rukwa na Katavi,
Wawezeshaji wa Warsha hii,
Waganga Wakuu na Waratibu wa Malaria,
Wataalamu na Watendaji kutoka Hospitali ya Mkoa.
Watendaji kutoka Sekretarieti ya Mkoa,
Watendaji kutoka Halmshauri za Mkoa wa Rukwa na Katavi,
Ndugu Waandishi wa Habari,

 
Mabibi na Mabwana.
Asalam alykum, Bwana Yesu asifiwe, tumsifu Yesu Kristo.

 
Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kwa namna ya pekee kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutukutanisha Siku hii ya leo.

 
Aidha napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kuwasafirisha salama wale wote ambao wanatoka nje ya Manispaa yetu ya Sumbawanga poleni  kwa safari ndefu na karibuni sana, Manispaa yetu ya Sumbawanga hali ni shwari na tulivu Usalama umeimarishwa. Huduma zote za Msingi zipo mtafurahia uwepo wenu Mkoani Rukwa.

 
Napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wageni wetu kutoka wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na taasisi isiyo ya kiserikali ya Johns Hopkins University – (Center for Communication Programs) kwa kututembelea na kutoa mwanya wa kuwa na majadiliano ya pamoja namna ya kuukabiliana na  ugonjwa wa malaria katika Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Katavi. 

 
Napenda  kuipongeza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wadau na Wafadhili  mbalimbali kwa jitihada zinazofanywa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria nchini.

 
Mradi wa Communication and Malaria Initiative in Tanzania (COMMIT) unaotekelezwa na Johns Hopkins University Tanzania (JHU) unalenga kuleta mabadiliko ya tabia kwa wanajamii dhidi ya Malaria nchini Tanzania. Mradi umetekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano(5) lakini kwa Rukwa na Katavi umetekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili.

 
Mradi huu unatekelezwa kwa kutumia mawakala wa kusaidia kubadilisha tabia ndani ya jamii katika Kata za mradi ambao hujulikana kwa majina ya CCA (Community Change Agent).

 
Mafanikio mazuri kwa jamii katika kutumia mawasilianao yanayolenga kubadilisha tabia na kutoa elimu  mbalimbali Kama;

 
·        Matumizi sahihi ya vyandarua vyenye Viuatilifu kila siku kwa mwaka mzima.

 
·        Hati punguzo kwa Wajawazito.

 
·        Kuhudhuria Kliniki mapema kwa wajawazito.

 
·        Dawa ya kinga ya Malaria kwa wajawazito.

 
·         Matumizi sahihi ya Dawa ya mseto ya Malaria.

 
·        Kuwahi vituo vya huduma mtu anapojihisi kuwa na dalili za malaria.

 
Elimu hii imekuwa ikitolewa kwa njia mbalimbali kwenye mikusanyiko ya watu kama vile kwenye Masoko, Shule, Vituo vya Afya na sehemu nyingine. Pia kwa mtu mmoja mmoja kupitia nyumba kwa nyumba.

 
Hadi  mradi unamaliza muda wake Johns Hopkins University (JHU) waliona ni vyema kuwe na mikakati ambayo itasaidia mradi endelevu ndani ya jamii. Hivyo, JHU imefanikiwa kupata fedha za kuendesha mradi  kwa kipindi cha mwaka mmoja. Wameamua kwa awamu hii  washirikiane na jamii na Serikali kusimamia huduma hii ambayo imeonyesha mafanikio mazuri ndani ya jamii kwa kipindi chote cha maisha yake.

 
Johns Hopkins University (JHU) kwa kushirikiana na RODI, imeandaa semina hii inayoshirikisha wadau mbalimbali muhimu katika kufikia lengo lililokusudiwa. Michango yetu ni muhimu sana ndani ya Idara na jamii, hivyo tushirikiane kwa pamoja tuone tunafanyeje na ni mikakati ipi inayoweza kusaidia kuleta mabadiliko ya kitabia katika jamii.

 
Pamoja na mikakati iliyopangwa kuendeshwa na Johns Hopkins University CCP TZ katika mradi wa COMMIT kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja mkoani Rukwa na KATAVI ni kuona kwamba JHU kama taasisi isiyo ya kiserikali inatoa mchango wake katika jamii. Pia ofisi ya RAS/DED kupitia Halmashauri ndani ya ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya kunakuwepo bajeti kwa ajili ya CCA (Community Change Agent) ya kuendesha mapambano dhidi ya Malaria kupitia mabadiliko ya tabia ndani ya Wilaya husika mara baada ya mradi huu wa COMMIT kuisha.

 
Nimatumaini yetu sisi kama  wadau, Wote  kwa pamoja tutapanga mikakati itakayotoa dira nzuri inayoshirikisha wadau wote muhimu katika  mapambano dhidi ya malaria mkoani Rukwa.

 
Ndani ya warsha hii wanashiriki watalamu kutoka sekta ya Afya ,Maafisa mipango, Taasi binafsi ‘CBO’s zinazoshiriki katika mradi huu  ili kwa pamoja tusaidiane kupanga mipango itakayoleta tija nzuri ya mabadiliko ya kitabia ndani ya jamii. Pamoja na kujadili mipango endelevu ya shughuli za malaria pia warsha hii itatoa mwanya wa kujadili maada kuhusu uongozi na mipango.

 
Pamoja na taarifa hizo zinazoashiria mradi kuwa na mafanikio makubwa, ni vema sasa taarifa kamili zitakazoeleza mafanikio hayo ziwe kwa undani zikielezea mafanikio katika ngazi ya Kata, Wilaya na Mkoa ili matokeo ya mradi yaweze kupimika vizuri zaidi.

 
Mwisho nawatakia majadiliano mema na yenye tija ninawataka mshiriki kikamilifu katika kuibua mkakati wa kupambana na Malaria. Ili Mkakati huo uweze kuwa rahisi kutekelezwa na Wadau wote pia mnajukumu la kuhakikisha elimu inatolewa katika maeneo yenu ya kazi kwa kuwa na  vikao vya kuelimisha watendaji, waheshimiwa madiwani na Wananchi kwa ujumla.

 
Vilevile mkakati huo uwasilishwe kwenye vikao halali vya Halmashauri,(CCHP) ili sisi wote tuwe washiriki katika kazi ya kuelimisha na kuhamasisha Wananchi kuupokea na kutekeleza mradi huu.

 
Nashukuru kwa kunisikiliza.

 
MABADILIKO YA KITABIA YANAWEZEKANA, TUSHIRIKIANE KUTOKOMEZA MALARIA.
Natamka kuwa Warsha
 hii imefunguliwa rasmi
Eng.
Stella Martin Manyanya(Mb)
MKUU WA MKOA WA RUKWA

No comments:

Post a Comment