Monday, December 17, 2012

KUFUATIA MFAMASIA KUMNYIMA DAWA MGONJWA AMBAYE NI MLEMAVU WA NGOZI (ALBINO) MKUU WA MKOA WA RUKWA AAGIZA ACHUKULIWE HATUA KALI IWE FUNDISHO KWA WENGINE

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiongea na uongozi wa hospitali kuu ya Mkoa wa Rukwa alipotembelea hospitalini hapo kumjulia hali mgonjwa Sebastian Chambanenge (41) mlemavu wa ngozi ambaye siku moja kabla alimtembelea Mkuu huyo ofisini kwake kumuomba msaada ambapo anakabiliwa na ugonjwa wa jicho unamsumbua kwa takriban miaka miwili sasa na kumpeleka hospitalini hapo kuona ni jinsi gani ya kuweza kumsaidia. Pamoja na hilo alitoa tamko (Maagizo) kali kwa uongozi wa hospitali hiyo kutokana na huduma isiyoridhirisha aliyopewa mgonjwa huyo kama linavyosomeka hapo chini :

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akisoma maagizo hayo kwa uongozi wa hospitali kuu ya Mkoa wa Rukwa. Maagizo hayo yapo hapa chini:
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya kushoto akimjulia hali Mgonjwa Sebastian Chambanenge (41) ambaye anaendelea kupatiwa huduma katika hospitali kuu ya Mkoa wa Rukwa iliyopo Mjini Sumbawanga. Mgonjwa huyo anakabiliwa na uvimbe mkubwa kwenye jicho ambapo chanzo chake kwa mujibu wa madaktari hospitalini hapo bado hakijajulikana ila kinahisiwa kuwa ni kansa ya ngozi ambayo kitaalamu hujulikana kama "Squamous cell Carcinoma". Pamoja na hayo, mgonjwa Sebastian hali yake kiuchumi ni duni hivyo kwa yeyote mwenye uwezo na nia ya kumsaidia kwa namna yeyote ile anaweza kuwasiliana nasi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa kupitia 025-2802137 / 2802138 au namba yangu ya Mkononi 0766-731185.  

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akimkabidhi Dkt. Mwanisawa (katikati) baadhi ya vifaa ikiwemo nguo, sabuni, na dawa ya mswaki kwa ajili ya mgonjwa Sebastian Chambanenge (hayupo pichani).
 
Sebastian Chambanenge (41) baada ya kupewa huduma ya kwanza ya kusafishwa kidonda katika hospitali kuu ya Mkoa wa Rukwa iliyopo Mjini Sumbawanga. Mgonjwa huyu bado anahitaji matibabu makubwa kuinusuru afya yake. 
 

Tarehe 14 Disemba 2012 Mgonjwa Sebastian ambaye ni Mlemavu wa ngozi alikuja ofisini kwangu akiomba msaada kuhusu ugonjwa unaomkabili ikiwemo kidonda kwenye shavu na jicho lililopofuka kutokana na hali ya ugonjwa. Hali yake ilikuwa si ya kuridhisha.
Kwa kuwa nilikuwa na wageni wengine nilimwagiza katibu wangu alishughulikie. Hivyo alitumwa Dereva wangu ampeleke kwa kutumia gari ya Mkuu wa Mkoa.
Baada ya kufika hospitali na kumkabidhi kwa Daktari (Kaimu Mganga Mkuu, alimhudumia ipasavyo na akamwandikia dawa muhimu, yeye mwenyewe akiwa na maandalizi ya kuingia Theatre.
Mgonjwa alipomwona Mfamasia Rhoda Kiponde alimpa dawa moja tu, na akamweleza kuwa nyingine akanunue kwenye maduka ya dawa. Hali hiyo ilimchanganya mgonjwa na kurudi tena Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huku akilalamika kuwa yeye hana fedha ya kununulia dawa, hata pesa aliyojia wamemchangia walimu wa Laela na Wasamaria wema wengine.
Kwa Mazingira hayo niliwasiliana na Daktari ili kujua uhalisia wa tatizo hilo na akanieleza kuwa ni vema mgonjwa alazwe kutokana na tatizo lake.  Kwa kuwa Daktari alikuwa na operation nyingine nilimshauri aendelee na mimi nitashughulika na waganga nitakaowakuta. Niliona ni vema niemde mimi mwenyewe (Mkuu wa Mkoa). Nilimshauri mgonjwa akubali kulazwa ili atibiwe chini ya uangalizi wa karibu.
Nilipofika hospital nilimkuta Mwangalizi wa Odfisi Winifrida Kuingwa akinisubiri. Mgonjwa akafanyiwa utaratibu wa kulazwa. Kisha tukafuatilia kujua kama dawa alizokosa mgonjwa kweli hazipo hospitali hiyo.
Tulipomwona Mfamasia aliyekuwa zamu (Rhoda Kiponde), baada ya kumpa cheti na kueelezwa kuwa niliye mbele yake ni Mkuu wa Mkoa alitaka kutoa dawa tena zile ambazo alishampa mara ya kwanza hali akijua kuwa dawa zile alishatoa. Hiyo ni kwa sababu cheti hakikuonyesha dawa zilizokosekana. Alipohisi kuwa anafuatiliwa akasisitiza kuwa dawa zile hazipo na haziletwi hospitali hiyo kabisa. Alipoulizwa kuwa sasa kama haziletwi wagonjwahao wanatibiwa na nini alijibu kuwa unaweza kuchanganya Ampicilini na Cloksilini ndipo unapata “Ampclox” (Kama inavyoeleweka kiutaalamu wao). Nilimwuliza sasa kwa nini usichanganye? Akajibu kuwa ipo Ampiciline tu. Na sasa akaweka alama ya dawa zisizokuwepo
Nikamwuliza zimeisha lini na mmeagiza lini? Akajibu haagizi yeye, ndipo tukakubaliana tumfuate anayeagiza (store)
Tulipofika kule tulipouliza juu ya dawa hizo tukaambiwa zipo na tukapewa, na akasisitiza kuwa kila wakati huwa zipo dawa za akiba.
Kutokana na mazingira hayo sikuridhishwa kabisa na huduma aliyopewa mgonjwa. Mfamasia baada ya kuona cheti kilichoandikwa na Daktari wake, tena kwa kuzingatia unyeti wa mgonjwa hususani mlemavu wa ngozi, na hali yake ya kipato alistahili kujiridhisha kwa kiwango cha juu kuwa dawa hizo kweli hazipo hospitalini hapo. Aidha nimekuwa nikipokea malalamiko mengi ya hospitali juu ya wagonjwa kunyimwa dawa kwa visingizio mbalimbali.
1.     Hivyo basi nawaagiza Viongozi husika (RAS, Mganga Mkuu wa Mkoa) kuhakikisha kuwa Mfamasia huyo Rhoda Kiponde anaondolewa mara moja kufanya kazi katika kitengo hicho na ikibidi ahamishwe.
2.     Uhakiki wa wafamasia na elimu na sifa zao ufanyike kwani pia kuna malalamiko nimeletewa ofisini kwangu kuwa kuna watumishi wenye viwango halisi na vyeti vya ufamasia wamezuiwa kufanya kazi kwa mujibu wa taaluma yao na kuwakumbatia wasio na ujuzi unaostahili.
3.     Nipate taarifa juu ya utekelezaji ndani ya siku saba kuanzi tarehe ya agizo hili.

Eng. Stella M. Manyanya (MB)
MKUU wa MKOA wa RUKWA

 

No comments:

Post a Comment