Monday, December 3, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AONANA NA NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI, AMUOMBA KUIMARISHA HUDUMA ZA BANDARI, USAFIRI MAJINI NA ANGA MKOANI HUMO

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na Naibu Waziri wa Uchukuzi Dkt. Charles Tizeba alipomtembelea ofsini kwake leo. Naibu waziri huyo yupo Mkoani Rukwa ambapo atatembelea bandari ya Kasanga, Kipili, uwanja wa ndege wa Sumbawanga na eneo lilitengwa tangu mwaka 1984 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege katika kijiji cha Kisumba km 20 kutoka Mjini Sumbawanga.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akisisitiza jambo ambapo amemuomba Naibu waziri wa Uchukuzi (Kushoto) kuongeza nguvu katika kuimarisha miundombinu ya bandari na anga katika Mkoa wa Rukwa ambao unahitaji sana huduma hizo. Akizungumzia usafiri katika ziwa Tanganyika alisema ziwa hilo linahudumiwa na meli mbili ikiwemo Meli kongwe kuliko zote duniani inayobeba abiria ya Mv. Liemba ikiwa na umri wa miaka 100. Meli nyingine ni Mv. Muongozo ambazo hazikidhi mahitaji ya usafiri kwa wananchi wa mwambao. Alisema pia kuwa usafiri katika ziwa hilo ni muhimu katika kuimarisha biashara na nchi jirani za Kongo DR, Burundi na Zambia. Kulia kwake ni Katibu Tawala Mkoa huo Alhaj Salum Mohammed Chima.
 
Naibu waziri wa Uchukuzi Dkt. Charles Tizeba akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Ofsini kwake leo alipomtembelea ambapo atakuwa Mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi. Waziri huyo pia atafanya ziara katika Mikoa ya Katavi na Kigoma ambapo atakagua miundombinu ya Reli, Anga, na Bandari. Alimuahidi Mkuu huyo wa Mkoa kuwa Wizara yake imejipanga kuhakikisha miundombinu hiyo inaimarika Mkoani Rukwa kuwezesha bidhaa na mazao ambayo huzalishwa kwa wingi Mkoani humo kusafirishwa kirahisi kwenda katika maeneo yenye masoko. Mpaka hivi sasa ujenzi wa bandari ya Kasanga unaendelea kujengwa, pamoja na bandari ya kipili, fedha za kuboresha uwanja wa ndege wa Sumbawanga kwa kiwango cha lami zimeshapatikana na unasubiriwa muda wa mradi huo kutekelezwa. Hali kadhalika upo mpango wa muda mrefu wa kujenga uwanja mkubwa katika eneo la Kisumba.

No comments:

Post a Comment