Tuesday, December 25, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA ATOA CHAKULA CHA KRISMAS NA MWAKA MPYA KWA WAFUNGWA NA WATOTO YATIMA PAMOJA NA KUSKILIZA KERO ZAO

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akikabidhi zawadi za skukuu ya krismas na mwaka mpya 2013 kwa watoto yatima wa kituo cha Bethania mjini Sumbawanga. Katika msimu huu wa Skukuu Mkuu huyo wa Mkoa ameamua kusherehekea kwa kuwatembelea watoto yatima na wafungwa wa gereza mahabusu Sumbawanga na gereza la Mollo kwa kuwapa chakula cha skukuu pamoja na kuskiliza kero zao mbalimbali. Zawadi alizotoa ni Mbuzi, Mchele pamoja na sabuni za kufulia kwa watoto yatima wa kituo cha Bethania vikiwa na thamani ya Tsh. 380,000/=
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiwa kwenye picha ya pamoja na watoto yatima wa kituo cha Bethania Mjini Sumbawanga waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013 katika shule mbalimbali Mkoani Rukwa. Mkuu huyo wa Mkoa ameahidi kugharamia masomo yao kwa kidato cha kwanza na sare za shule pamoja na vitendea kazi vingine. Kulia ni Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Sumbawanga Ndugu Festo Chonya akimuwakilishha Mkuu wa Wilaya hiyo Ndugu Methew Sedoyyeka.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watoto yatima wa kituo cha Bethania Mjini Sumbawanga alipowatembelea kuwafariji kwa chakula katika msimu huu wa sikukuu.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akizungumza na watoto yatima wa kituo cha Bethania, kulia ni Mkuu wa kituo hicho Ndugu Emmanuel Mwampimbwe. Mkuu huyo wa Mkoa aliagiza watoto yatima katika kituo hicho pamoja na vituo vingine watambuliwe na watengenezewe vitambulisho vitakavyowawezesha kupatiwa huduma bure katika hospitali za Serikali Mkoani Rukwa.

Ndugu ASP. A. Kimati akisoma taarifa ya gereza la Mollo kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya alipotembelea gereza hilo jana kutoa salamu na chakula cha sikukuu kwa wafugwa wa gereza hilo na kuskiliza kero zao mbalimbali. Mkuu huyo wa Mkoa alipokea kero mbalimbali kutoka kwa wafugwa 195 wa gereza hilo ikiwemo uhaba wa sare za wafungwa, wafugwa kutopewa nakala za hukumu zao, kesi zao kusikilizwa kwa kiswahili lakini hukumu kuandikwa kiingereza, kutokukubalika kwa dhamana zao, kutokuwepo kwa hakimu katika Wilaya ya Nkasi, na baadhi ya kesi kuchelewa kuskilizwa.  
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akijumuisha ziara yake gerezani Mollo kwa kuzungumza na viongozi wa Jeshi la Polisi na Jeshi la magereza Mkoani humo ambapo aliahidi kufuatilia kero zote zilizowasilishwa kwa kushirikiana na pande zinazohusika kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi. Alisema kuwa ataendelea kuweka msukumo wa ujenzi wa mahakama za Nkasi na Wilaya mpya ya Kalambo. Aidha aliutaka uongozi wa gereza hilo kufyatua matofali kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wafungwa katika gereza hilo ambapo yeye atasaidia upatikanaji wa mabati na vifaa vingine vya madukani, kwa sasa mabweni yanayotumika katika gereza hilo ni ya mabati magumu ambayo kutokana na hali ya hewa ya maeneo hayo kunakuwa na baridi kali kwenye msimu wa baridi. 

No comments:

Post a Comment