Monday, January 28, 2013

MAGAZETI YA LAO JUMANNE JANUARI 29 - 2013

 
 
.
KUSOMA MAGAZETI YA LEO

HAYA NDIYO MANUFAA YA WANAMTWARA IWAPO GESI ITAPELEKWA DAR ES SALAAM - NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI ANENA

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene-
---
Na Mwandishi
SERIKALI imetaja manufaa na faida ambazo wanatarajia kuzipata wananchi wa Mtwara pamoja na Lindi endapo gesi itasafirishwa kwenda Jijini Dar es Salaam.

 
Imesema Mkoa wa Mtwara ndipo utakapo jengwa mtambo mkubwa wa kusafishia gesi hiyo kabla ya kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam kwa matumizi ya uzalishaji umeme na matumizi ya moja kwa moja viwandani.

 
Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alipokuwa akizungumza katika Kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Radio One jijini Dar es Salaam.


Naibu waziri huyo ameweka wazi kuwa mkoani Mtwara licha ya Serikali kupanga kujenga viwanda vingine kadhaa, inajenga mtambo wa megawati 250 ambao utakuwa ukizalisha umeme na mwingine kujengwa mkoani Lindi eneo la Somanga Funga utakao kuwa ukizalisha megawati 520.

 
Akifafanua zaidi Simbachawene alisema eneo la Mikindani katika Kijiji cha Msijute mkoani Mtwara kinatarajiwa kujengwa kiwanda kikubwa cha saruji Afrika Mashariki na Kati chenye uwezo wa kutoaji ajira kwa watu 6000 jambo ambalo ni manufaa ya Wanamtwara.
Alisema pia tayari kuna wawekezaji wa viwanda vya mbolea wamejitokeza kujenga viwanda mkoani Mtwara na Serikali itaviacha vinu vya kuchimba na kusindika gesi eneo hilo jambo ambalo bado ni manufaa makubwa kwa wananchi.

 
“Viwanda vya kusindika gesi hii vimepangwa kujengwa maeneo ya Lubasi, Kishere, Mchinga Bay, Lindi, Sudi Bay, Airport pamoja na Mikindani…viwanda vyote hivi vitatoa ajira kubwa sana,” alisema Naibu Waziri.

 
Alisema licha ya manufaa hayo, gesi itakapopelekwa Dar es Salaam itazalisha umeme wa uhakika pamoja na kutumika moja kwa moja viwandani jambo ambalo litailetea taifa tija kubwa ikiwa ni pamoja kupunguza ukali wa maisha.

 
“Ni kweli gesi imepatikana Mtwara lakini ni lazima uipeleke sokoni ili iweze kupata soko (wateja)…Dar es Salaam ndio kwenye soko, huwezi ukaiacha Mtwara ambako hakuna soko; mbali na kuzalisha umeme kuna viwanda 37 na hoteli kadhaa zinataka ziitumie moja kwa moja ni lazima iletwe huku, Mtwara pale hakuna soko,” alisema.

 
Aidha alitolea mfano kuwa zipo nchi mbalimbali ambazo zimegundua gesi lakini zimelazimika kuisafirisha kwa mabomba kwenda eneo la soko. Alibainisha kuwa nchi ya Urusi inasafirisha gesi yake hadi nchini Ujerumani huku Iran ikisafirisha hadi India gesi yake kutafuta soko lilipo.

 
Alisema miundombinu mikubwa ya umeme ipo jijini Dar es Salaam hivyo kuna kila sababu ya gesi hiyo kuletwa jijini humo ili iweze kuzalisha umeme na matumizi ya viwandani moja kwa moja pamoja na matumizi mengine, ambapo tayari wateja wamepatikana.
 
Aidha aliongeza kuwa uzalishaji umeme wa kutosha kwa kutumia gesi utapunguza bei ya umeme na kuuzwa kati ya senti 6 na 8 za Marekani jambo ambalo litapunguza ugumu wa maisha na pia bei ya bidhaa nchini.
 
Pamoja na hayo amevitaka baadhi ya vyama vya siasa na taasisi zisizo za Serikali (NGO’s) zinazowapotosha Wanamtwara juu ya mradi huo kuacha kitendo hicho kwani hakuna asiyejua umuhimu wa gesi hiyo kuja Dar es Salaam.

 
“Hivi ni nani asiyejua kuwa tatizo la kutokua na umeme wa uhakika nchini ndilo linalokwamisha uchumi wa nchi…Tanzania inapoteza bilioni 4.5 kwa ajili ya kununua mafuta ya kuzalisha umeme kwenye mitambo yake, sasa gesi itaokoa fedha hizi,” alisema Simbachawene.
 
Hata hivyo amesema Serikali haiwezi utekeleza mradi huo kwa nguvu bali itaendelea kuwaelimisha Wanamtwara umuhimu na manufaa ya gesi hiyo kuletwa Dar es Salaam na inaimani wataelewa na malumbano kumalizika.

Monday, January 14, 2013

MWANRI AMALIZA ZIARA YAKE YA SIKU SABA MKOANI RUKWA, ASEMA HALMASHAURI ZITAKAZOPATA HATI CHAFU KUTOPATA RUZUKU SERIKALINI

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ndugu Agrey Mwanri akitoa maelekezo mbalimbali kwa uongozi wa Mkoa wa Rukwa katika majumuisho ya ziara yake iliyodumu kwa muda wa siku saba Mkoani Rukwa ambapo alitembelea miradi zaidi ya 22 ambayo baadhi yake aliiwekea mawe ya msingi. Katika hotuba yake hiyo alitoa maagizo mbalimbali ambayo yote yalikuwa yakilenga kwenye utawala bora, matumizi bora ya fedha za Serikali katika miradi pamoja utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010. Katika hotuba yake iliyodumu kwa zaidi ya saa tatu alizionya halmashauri zote nchini zitakazopata hati chafu kuwa hazitapata fedha ya ruzuku ya miradi ya maendeleo (LGCDG-Local Government Capital Development Grant) ikiwa ni kutoa funzo kwa watendaji wa halmashauri pamoja na kupandisha hasira za madiwani ili waweze kuisimamia vizuru halmashauri husika. 

Mama Grace Mwanri, mke wa Naibu Waziri wa TAMISEMI Agrey Mwanri akitoa ushuhuda kuhusu utendaji wa mumewe "Anavyoongea na kutenda mume wangu ndivyo alivyo hata nyumbani na si kwamba anafanya hivyo kupata sifa wala umaarufu kwani mara zote huwa hapendi mambo ya kipuuzipuuzi" alisema mama Mwanri.

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima akizungumza kuwatambulisha wageni na washiriki katika kikao hicho cha majumuisho kwa mgeni rasmi Ndugu Agrey Mwanri kushoto. Katika hotuba yake fupi alimuhakikishia Naibu Waziri kuwa maagizo yote aliyoyatoa kwenye ziara yake yatafanyiwa kazi na kwamba miradi iliyokuwa na mapungufu itarekebishwa.

Naibu Waziri Mwanri akizungumza na washiriki wa kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa Dini, Chama na Serikali. Taasisi za Umma, mashirika binafsi, wajasiriamali, na watumishi mbalimbali wa halmashauri na taasisi za Umma.

Sehemu ya washiriki wa kikao hicho katika ukumbi wa RDC katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa wakifuatilia hotuba ya majumuisho ya Ndugu Mwanri.

Kutoka kushoto ni Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu Mkoa wa Rukwa Ndugu Samson Mashalla na Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Sumbawanga Ndugu Festo Chonya wakifuatilia kikao hicho.

Baadhi ya wadau walioshiriki kikao hicho wakifuatilia kwa makini, wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Ndugu Godfrey Shona, Kaimu Mkurugenzi manispaa ya Sumbawanga, Mbunge Mst. na muwekezaji wa ndani Ndugu Chrissant Majiyatanga Mzindakaya na kwa kwanza kulia ni muwekezaji wa ndani Ndugu Reina Lukara.

Naibu Waziri wa TAMISEMI Agrey Mwanri akimkabidhi maagizo yatokanayo na ziara yake ya siku saba Mkoani Rukwa Katibu Tawala wa Mkoa huo Alhaj Salum Mohammed Chima aweze kuyafanyia kazi katika Mkoa wake.

Naibu Waziri wa TAMISEMI Agrey Mwanri akimkabidhi maagizo yatokanayo na ziara yake ya siku saba Mkoani Rukwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Ndugu Moshi Chang'a aweze kuyafanyia kazi katika Wilaya yake.

Naibu Waziri wa TAMISEMI Agrey Mwanri akimkabidhi maagizo yatokanayo na ziara yake ya siku saba Mkoani Rukwa Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Ndugu Idd Kimanta aweze kuyafanyia kazi katika Wilaya yake.

Naibu Waziri wa TAMISEMI Agrey Mwanri akimkabidhi maagizo yatokanayo na ziara yake ya siku saba Mkoani Rukwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Ndugu Mathew Sedoyeka aweze kuyafanyia kazi katika Wilaya yake.

Thursday, January 10, 2013

MHE. MWANRI AZITAKA HALMASHAURI ZOTE NCHINI KUSIMAMIA VIZURI FEDHA ZA MIRADI YA SERIKALI

Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. Agrey Mwanri akipima kwa tape maalum urefu wa moja ya barabara zilizojengwa na Manispaa ya Sumbawanga katika Mji huo kuhakikisha kama barabara hiyo imejengwa kwa vipimo vilivyoanishwa kwenye mpango wa ujenzi huo (BOQ). Naibu Waziri huyo alitumia fursa hiyo kuziasa halmashauri zote nchini kusimamia vyema fedha za Serikali katika miradi kuhakikisha inafanana na thamani ya fedha zilizotumika, alilazimika kusema hayo baada ya kubaini mapungufu mbalimbali katika mradi huo wa barabara na miradi mingine aliyofanikiwa kuitembelea Mkoani Rukwa.

Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. Agrey Mwanri akikagua barabara za lami zilizo chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga zilizojengwa hivi karibuni. Katika ukaguzi huo alibaini mapungufu mbalimbali katika ujenzi huo na kuagiza Halmashauri hiyo kuhakikisha mapungufu hayo yanaondolewa. Aliitaka pia halmshauri hiyo kusimamia vyema kazi za Serikali kuepusha minong'ono inayotoka kwa wananchi juu ya utendaji mbovu wa baadhi ya watendaji Serikalini.

Mhe. Agrey Mwanri akiweka jiwe la msingi kiwanda cha unga cha Malangali kinachomilikiwa na muwekezaji wa ndani mapema hivi leo. Kwa sasa Mkoa wa Rukwa una viwanda vitatu vya unga vinavyomiliwa na wawekezaji wa ndani.  

Naibu wa Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Agrey Mwanri akikagua kiwanda cha unga cha Malangali Mjini Sumbawanga leo alipotembelea kiwandani hapo kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi.

Mhe. Mwanri akizungumza na wakazi wa Mji wa Sumbawanga katika Stendi kuu ya mabasi ya Mjini hapo ambapo alipokea kero mbalimbali ikiwepo ubovu wa miundombinu ya umeme na barabara katika stendi hiyo. Aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Sumbawanga kufanya Mkutano wa hadhara na wananchi hao kuskiliza kero zao zote pamoja na kuzitaftia ufumbuzi na kumpelekea taarifa ya utekelezaji.

Katika hali isiyotegemewa msafara wa Mhe. Mwanri ulipowasili katika kijiji cha Mlanda katika Manispaa ya Sumbawanga kwa ajili ya Mkutano wa hadhara ulikuta msiba ambapo walishiriki na kutoa ubani ambapo Mhe. Mwanri alitoa laki moja na alfu mbili na aliyekuwa Mbunge wa Sumbawanga Mjini CCM ambaye pia ni Mjumbe wa halmashauri kuu Taifa ya CCM (NEC) kupitia Mkoa wa Rukwa Aeshi Hillal alikabidhi shilingi alfu hamsini. 

Tuesday, January 8, 2013

TAARIFA YA MKUU WA MKOA WA RUKWA KWA NAIBU WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU-TAMISEMI-MHE.AGGREY MWANRI-ZIARANI MKOANI RUKWA

 

ZIARA YA MHE. MWANRI MKOANI RUKWA


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Aggrey Mwanri akikagua mradi wa maabara katika kituo cha afya cha Matai katika Wilaya mpya ya Kalambo leo. Naibu Waziri huyo amepiga marufuku miradi yote ya serikali hususani inayohusisha mbao kupigwa rangi na badala yake ipakwe vanish, hiyo ni kutokana na baadhi ya wakandarasi kutumia staili hiyo kuiibia Serikali kwa kuweka mbao za bei nafuu na kuzipiga rangi. Mhe. Mwanri yupo Mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi ya siku saba ambapo ataembelea halmashauri zote za Mkoa wa Rukwa na kukagua miradi mbalimbali iliyopo chini ya Halmashauri hizo.

Naibu Waziri TAMISEMI Mhe. Agrey Mwanri (kulia) akikagua ujenzi wa banio la mradi wa umwagiliji katika kijiji cha Katuka katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Mhe Mwanri aligoma kuweka jiwe la msingi katika mradi huu kutokana na mkandarasi kujenga mradi huo chini ya kiwango kinyume na mchoro halisi wa mradi huo. Aliagiza mapungufu yarekebishwe ndipo Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Moshi Chang'a aweke jiwe hilo kwa niaba yake.


Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Ndugu Moshi Mussa Chang'a akimkaribisha Mhe. Mwanri azungumze na wananchi wa Wilaya ya Kalambo katika ziara yake ambayo amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kutumia fursa ya miundombinu inayoendelea kujengwa Mkoani Rukwa pamoja na ujio wa Halmashauri yao mpya katika kuwekeza na kujiendeleza kiuchumi.

Kutoka kushoto ni Mama Mwanri mke wa Naibu Waziri, Mhe. Agrey Mwanri Naibu Waziri TAMISEMI, Mhe. Moshi Chang'a Mkuu wa Wilaya ya Kalmabo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Godfrey Schona wakiwa katika picha ya pamoja pembezoni mwa fukwe za Ziwa Tanganyika katika Hoteli ya Liemba Beach Resort walipotembelea ikiwa ni sehemu ya ziara yake Mkoani Rukwa.

Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. Agrey Mwanri akiweka jiwe la msingi katika nyumba ya mganga wa kituo cha afya Matai mapema hii leo. Katika miradi miwili aliyotembelea Mhe. Mwanri aligoma kuweka mawe ya msingi hadi hapo marekebisho aliyoagiza yatakapofanyiwa kazi ndipo mawe hayo yawekwe kwa niaba yake. 

Mama Mwanri akiwasalimu wananchi wa Matai katika Wilaya ya Kalmbo.


Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Kipeta kabla ya Mhe. Mwanri kuzungumza nao kwenye ziara yake ya kuhamasisha shughuli za maendeleo Mkoani Rukwa.

Naibu Waziri wa TAMISEMI Ndugu Agrey Mwanri akipanda kwa tahadhari kubwa katika daraja la Mto Momba linalounganisha wananchi wa Kilyamatundu Mkoani Rukwa na wale wa Kamsamba Mkaoni Mbeya. Daraja hili lililojengwa kwa kamba limekuwa halikidhi haja ya wananchi hao jambo wanaloomba Serikali kuwajengea daraja litakalowawezesha kuvuka na kuvusha mazao yao kirahisi. 

Tuesday, January 1, 2013

MAMA TUNU PINDA ASHIRIKI MKESHA WA MWAKA MPYA SAMBAMBA NA TAMASHA LA WANAWAKE MKOANI RUKWA (RUKWA WOMEN IN ACTION)

Mama Tunu Pinda mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwasili katika ukumbi wa St. Maurus Chemchem Mjini Sumbawanga jana katika sherehe aliyoalikwa na Mkuu wa Mkoa Rukwa Injinia Stella Manyanya ya kuaga mwaka 2012 na kukaribisha mwaka 2013 iliyoenda sambamba na tamasha kubwa la mwanamke wa Rukwa RUWA (Rukwa Women in Actiion). Tamasha hilo lililobuniwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa lina lengo la kuwanunganisha wanawake wa Mkoa wa Rukwa pamoja katika tamaduni zao tofauti katika kuwainua kiuchumi na kifikra ambapo walishiriki kwa kuonyesha tamaduni zao za ngoma, mavazi na chakula. Lengo la tamasha hilo pamoja na umoja huo ni kwa ajili ya kunadi na kuhamasisha utalii wa ndani, kuwawezesha kinamama wa kipato cha chini, kuhamasisha na kuwezesha vita dhidi ya umaskini, mimba za mashuleni, lishe bora na chanjo za afya kwa watoto wachanga na wanawake wa kipato cha juu kuwawezesha wa kipato cha chini.
 
 
Mama Tunu Pinda Mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akitoa hotuba yake katika tamasha hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza katika tamasha hilo kumkaribisha mke wa Waziri kuzungumza na washiriki zaidi ya mia sita walihudhuria katika tamasha hilo.

Mama Pinda (kulia), Mama Dora Rajab Rutengwe mke wa Mkuu wa Mkoa wa Katavi (wa pili kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Stella Manyanya na wanawake wengine wakijumuika kucheza muziki wa kwaito katika kupasha misuli moto kwenye tamasha hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akionyesha vazi linalotangaza utalii wa ndani na rasilimali muhimu kama misitu, wanyama pori, na samaki.


Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Moshi Mussa Chang'a ambaye alikuwa mshereheshaji mahiri (MC) katika hafla hiyo akiwa kazini. Chezea Chang'a wewe!

Sehemu ya watu walioalikwa katika tamasaha hilo. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu mia sita (600) walihudhuria.

Ilifika muda washiriki wa maonyesho hayo kupita mbele ya jukwaa kuu tayari kwa kuanza kuonyesha sanaa na mitindo mbalimbali.
 
Mmoja ya washiriki akionyesha moja ya vazi la kiutamaduni la asili ya makabila ya Rukwa kwa wazee wakati wa msimu wa baridi.
 
Katibu tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima akisakata ngoma ya kinyaturu katika tamasha hilo. Kulia ni mwanae Hussein Chima.
 
Mama Tatu Chima mke wa Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa akimpa zawadi ya shanga za kabila la kinyaturu Mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Tunu Pinda kabla ya kuanza kucheza ngoma ya kabila hilo. Kulia ni mumewe Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa (wa pili kushoto) Injinia Stella Manyanya akishiriki kwenye ngoma ya kabila lake la wangoni waliojumuika kwenye tamasha hilo kuonyesha baadhi ya tamaduni zao. Wa kwanza kushoto akionyesha uwezo mkubwa katika kusakata ngoma hiyo ni mwandishi wa habari wa channel ten Judy Ngonyani.  

Mduara pia umo katika ngoma za kabila la wangoni. 

Washiriki wa kabila la wahaya wakionyesha baadhi ya mavazi ya asili ya kabila lao.

Ngoma za kihaya.
 

Majaji waliohusika katika katika mashindano ya tamaduni za makabila tofauti ya Mkoani Rukwa, Mbeya, Iringa, Ruvuma, Kagera, Singida, Kigoma, Shinyanga na Mwanza. Mkoa wa Rukwa ulishinda katika Ngoma.

 Washiriki wa kabila la wafipa wakionyesha baadhi ya mavazi yao ya asili na baadhi ya zana zao za asili. 


 Sound ya ngoma ya kabila la wafipa ikitumbuiza katika tamasha hilo. Kigoda hutumika kusugua chungu ambacho hutoa mlio wa aina yake katika kunogeza ngoma ya kabila hilo.


 Washiriki wa kabila la wafipa wakionyesha tamaduni zao za kusaga unga na ulezi kwa kutumia zana za asili.

 Pombe ya asili ya kabila la wafipa inayotengenezwa kwa ulezi na kunyewa kwa mirija, raha duniani.
 
 Mambo yetu ya rusha roho nayo yalikuwepo. 

 Palikuwa hapatoshi.
 
Mvua ya shampen ya kukarisha mwaka mpya 2013 ikifunguliwa na mratibu wa tamasha hilo ambae pia ni Afsa maendeleo ya jamii Mkoa wa Rukwa Ndugu Deonisya Njuyui.
 
 Cheers kwa mwaka 2013. Mama Tunu Pinda Mke wa Waziri Mkuu akigonganisha glass na Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu Mkoa wa Rukwa Ndugu Samson Mashalla na Mke wa aliyekuwa Mbunge jimbo la Sumbawanga Mjini CCM Aeshi Hillal.
 
 Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Idd Kimanta akinywa togwa iliyoandaliwa na kabila la wafipa.
 
 Mbunge wa Jimbo la Kalambo Josephat Kandege nae akilamba tongwa.
 
 Mama Tunu Pinda Mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya wakionja ugali wa muhogo ulioandaliwa na kabila la Waha kutoka Kigoma.
  
 Ndizi kuku au Kuku ndizi kutoka katika kabila la wanyakyusa la Mkoani Mbeya.
 
 Maharage yaliyochanganywa na mboga za majani kutoka katika kabila la wanyakyusa la Mkoani Mbeya.
 
 Mshiriki Leah Mgagama kutoka katika kabila la wangoni akionysha moja ya vazi la kabila hilo na kifaa cha kuhifadhia chakula kisiharibike kijulikanacho kwa jina la "Kijamanda".
 
 Vazi la kitanzania likiwa na bandera ya taifa.
 
 Ilikuwepo mitindo mbalimbali ya mavazi.
 
 Onyesho la mavazi
 
 Onyesho ya vazi la mjamzito.
 
 Anthonia Nkyabonaki kutoka kabila la wahaya akionyesha mtindo wa mavazi.