Tuesday, September 17, 2013

WAFANYAKAZI WA KAMPUNI YA AASLEAFF BAM INAYOJENGA BARABARA YA LAELA SUMBAWANGA WAGOMA, SERIKALI YA MKOA WA RUKWA YAINGILIA KATI KUTAFTA SULUHU

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiongoza kikao baina ya uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Rukwa na uongozi wa kampuni ya Aasleaff Bam International inayojenga barabara kuu ya lami kutoka Laela - Sumbawanga katika Camp za kampuni hiyo zilizopo Kyanda kwa lengo la kutafuta suluhu baada ya baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo wasiozidi 700 wakiwepo madereva wa magari na mitambo kugoma kufuatia madai mbalimbali.  Madai hayo ni pamoja na kuondolewa kwa mshauri wa mambo ya ulinzi katika mradi huo kwa madai kuwa alimtisha kwa bastola mfanyakazi mwenzao kwa kumuhusisha na mambo ya wizi, kulipwa mshahara sawa baada ya serikali kutangaza kima kipya cha chini bila kujali tofauti za ujuzi walionao, kuondoshwa kwa fedha ya chakula na malazi kama ilivyokuwa ikitolewa mwanzo.
 
Wakizungumzia kero hizo uongozi wa kampuni hiyo umesema mazungumzo yalikuwa yakiendelea kati ya uongozi wa wafanyakazi pamoja na madai mengine yaliyokuwa yameshafikishwa ngazi za juu yakisubiri maamuzi kutoka kwa uongozi wa kampuni hiyo na Serikali kwa ujumla.

Mshauri wa mambo ya usalama katika kampuni ya Aasleaff Bam International Ndugu Morgan  aliyedaiwa kumtisha kwa bastola moja ya mfanyakazi katika kampuni hiyo kwa madai ya kujihusisha na vitendo vya wizi wa mafuta na vifaa mbalimbali vya ujenzi katika kampuni hiyo. Hata hivyo baada ya kuhojiwa na Polisi Ndugu Morgan alikanusha madai hayo na kusema kuwa ni ya kusingiziwa kutokana na hatua zake za kudhibiti wizi katika maeneo yao ya kazi.

Ndugu Rogers Ndosi aliyadai kutishwa kwa bastola na Ndugu Morgan na kusababisha zaidi ya nusu ya wafanyakazi katika kampuni hiyo kugoma kumshinikiza Morgan kuondolewa katika kampuni hiyo. Walidai kuwa Morgan aondoke au laa wao wataondoka.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na wafanyakazi waliogoma wa Kampuni ya Aasleaff Bam International na kuwaomba warudi kazini mpaka hapo atakapokuwa ametafta suluhu ya mgogoro huo kwa kuzishirikisha pande husika katika kutatua kero walizoziwasilisha kwake. Hata hivyo hakusita kukemea vitendo vya wizi vinavyofanywa ndani kampuni hiyo na kusema kuwa vinazorotesha kukamilika kwa mradi huo. 

Majadiliano yakiendelea.
 
Mmoja ya wafanyakazi walliogoma akitoa kero zao mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya.

No comments:

Post a Comment