Tuesday, October 1, 2013

MAALIF SEIF AFUNGA IJITIMAI YA KIMATAIFA MKOANI RUKWA SEPT 30, AWATAKA WAISLAMU KUWA WAMOJA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya kabla ya kuagana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad alimkbidhi zawadi mbalimbali ikiwemo nyama maalum inayotengenezwa na kiwanda cha Saafi kilichopo Sumbawanga Mkoani Rukwa na vitambaa maalum vya kushonea nguo na kanga. 
 

 Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad akisindikizwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya katika uwanja wa ndege wa Sumbawanga kwa ajili kuanza safari ya kurudi Zanzibar tarehe 30 Septemba 2013.
 
Makamu wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiagana na viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu waliohusika na maandalizi ya Ijitimai hiyo Mjini Sumbawanga. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Moshi Chang'a.
 
....................................................................................................
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, ametoa wito kwa waislamu kuungana kwa mambo ya msingi yaliyomo katika dini hiyo na kuacha kutofautia kwa sababu ya madhehebu yao.
 
Amesema kuwa na madhehebu tofauti ni neema katika dini, hivyo hakuna sababu ya kugawanyika kutokana na tofauti ya madhehbu waliyonayo waislamu.
 
Maalim Seif ametoa nasaha hizo wakati akifunga rasmi Ijtimai ya Kimataifa iliyofanyika Mjini Sumbawanga, Mkoani Rukwa. Amesema ni jambo la kushangaza kuona waislamu wanakubaliana katika mambo ya msingi, lakini wanatofautiana na kulumbana kwa mambo madogo ambayo hayana athari ndani ya misingi na mihimili mikuu ya dini.
 
Amefahamisha kuwa iwapo waislamu wataungana na kuwa kitu kimoja, wataweza kuwashinda maadui wa Uislamu ambao siku zote wamekuwa wakishabikia migawanyiko ndani ya dini hiyo, akiwataja baadhi ya maadui hao kuwa ni maradhi ya ukimwi na dawa za kulevya.
 
Kwa upande mwengine amesema wakati waislamu wakijadili juu ya maadili ya dini yao, pia hawana budi kuhimizana katika kukabiliana na maadui wanaoathiri maendeleo ya nchi ikiwa ni pamoja na janga la UKIMWI pamoja na matumizi ya dawa za kulevya. Amesema majanga hayo kwa kiasi kikubwa yanatokana na kuporomoka kwa maadili, na kwamba wanaoathirika zaidi ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
 
Ameongeza kuwa ni wajibu wa masheikh, walimu, wazazi na jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika kuelimishana juu ya majanga hayo, sambamba na kuachana na makatazo ya Mwenyezi Mungu yakiwemo pia vitendo vya zinaa.
 
Amesema, inaweza kueirejesha jamii katika maadili mema iwapo waislamu watakubali kufuata misingi thabiti na miongozo sahihi iliyomo katika uislamu.
 
Akizungumzia usalama wa nchi amesema wananchi hawana budi kuwa mstari wa mbele kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha amani inaendelea kuwepo nchini ukizingatia hali ya sasa ya ugaidi inayoitikisa dunia na afrika ya mashariki, akitolea mfano tukio la Westgate na kwamba kama limejitokeza Kenya basi hata Tanzania laweza kuja.
 
Naye Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, amewahimiza waislamu waliohudhuria katika Ijtimai hiyo ya siku nne, kuitumia kivitendo elimu waliyoipata juu ya dini yao.
 
Amewahimiza waislamu hao kuwafikishia wengine elimu hiyo, ili nao waweze kuitekeleza dini ya Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa maamrisho yake na mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW).
 
Kwa upande wake, Amiri wa Jumuiya ya Fiysabilillahi Tabligh Markaz Mkoani Rukwa Sheikh Abdallah Abubakar amewashukuru wailamu pamoja na viongozi wa Mkoa huo, kwa mshikamano walioonyesha katika kufanikisha Ijtimai hiyo.
 
Mapema akisoma Risala ya Jumuiya hiyo Amir Ali amesema Jumuiya imepata mafanikio makubwa tangu kuasisiwa kwake na kupatiwa usajili mwaka 1992, ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha waislamu katika kutekeleza maamrisho ya Munyezi Mungu na kuacha kabisa makatazo yake, iki kujijengea mustakbali mwema katika maisha ya akhera.
 
Viongozi mbali mbali wa dini na Serikali wameshiriki katika ufungaji wa Ijtimai hiyo akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk.

No comments:

Post a Comment