Tuesday, October 22, 2013

MKUTANO WA WADAU WA UTEPE MWEUPE (WHITE RIBBON ALLIANCE ) WA UZAZI SALAMA TANZANIA WAENDELEA MKOANI RUKWA

Mratibu wa taifa wa utepe mweupe wa Uzazi salama Tanzania Dkt. Rose Mlay akiwasilisha mada iitwayo "Wajibika Mama Aishi" katika Mkutano na viongozi wa idara ya afya pamoja na wadau wa Sekta hiyo Mkoani Rukwa katika ukumbi wa RDC tarehe 21 Oktoba 2013 kujadili matumizi bora ya bajeti zilizowekwa na kuzipa kipaombele katika kusaidia uhai wa mama wajawazito katika vituo vya afya Mkoani Rukwa. Akielezea lengo la taasisi hiyo ya "White Ribbon" alisema ni kuimbusha Serikali ya Tanzania kutekeleza ahadi yake ya kuwa na asilimia hamsini ya vituo vya afya Mkoani Rukwa vitakavyotoa huduma kamili za dharura za uzazi zikiwa ni pamoja na upasuaji kumtoa mtoto na kutoa damu salama zinapohitajika ifikapo 2015.
 
Mganga Mkuu Hospitali kuu ya Mkoa wa Rukwa Dkt. John Gurisha akitoa maelezo mafupi juu ya huduma za kinamama wajawazito Mkoani Rukwa katika Mkutano huo. Alisema kuwa changamoto kubwa inayoikabili sekta ya afya Mkoani Rukwa ni uhaba wa watumishi katika sekta ya afya, uhaba wa magari ya wagonjwa kuweza kuwasaidia wananchi waliombali na huduma za afya pamoja na Vituo vingi vya afya na zahanati kutokuwa na vyumba vya upasuaji hususani katika maeneo ya mwambao na maeneo mengine ya pembezoni. Kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima na Kushoto ni Mratibu wa taifa wa utepe mweupe wa Uzazi salama Tanzania Dkt. Rose Mlay.

Baadhi ya watumishi wa idara ya afya Mkoani Rukwa na wadau wengine wa sekta hiyo wakisikiliza uwasilishwaji wa mada mbalimbali katika Mkutano huo. Shirika la Utepe Mweupe  Tanzania "White Ribbon Alliance for Safe Motherhood in Taznania(WRATZ)" linaendeleza kampeni yake ya miaka mitatu iitwayo "Wajibika Mama Aishi" (Be Accountable sa Mama can Survive Childbirth) kwa kuendesha mikutano na Semina mbalimbali kwa wadau wa afya katika ngazi ya Serikali na kijamii katika maeneo mbalimbali hapa nchini; Lengo kuu likiwa kuikumbusha Serikali juu ya utekelzaji wa ahadi yake ya kuboresha huduma kamili za dharura za uzazi zikiwa ni pamoja na upasuaji kumtoa mtoto na kutoa damu salama zinapohitajika ifikapo 2015. Ahadi hiyo kwa kiasi kikubwa inaendelea kutekelezwa na Serikali ya awamu ya nne na ifikapo mwaka 2015 itakuwa kipindi cha kuifanyia tathmini.

No comments:

Post a Comment