Thursday, November 14, 2013

COSTECH YATOA FEDHA KIANZIO (SEED FUND) TSH. MILIONI 8 KWA KONGANO LA UMOJA WA WAFUGAJI WILAYANI NKASI MKOANI RUKWA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injnia Stella Manyanya akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni nane (8) Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Wafugaji wa Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa Ndugu Pancras Maliyatabu kama fedha ya kianzio kwa Kongano la umoja wa wafugaji hao zilizotolewa na Tume ya Sayansi na Teknolojia nchini (COSTECH) kwa lengo kuendeleza ufugaji wa kisasa usioathiri mazingira na kumnufaisha mfugaji kiuchumi. Kulia ni Ndugu Festo Maro Afsa Utafiti Mkuu wa COSTECH na kushoto ni Katibu wa Umoja wa Wafugaji hao Ndugu Jisena Biliya.
Viongozi wa Umoja wa Wafugaji wa Wilayani Nkasi wakionyesha hundi yenye thamani ya shilingi milioni nane waliyopewa na COSTECH kama "Seed Fund" kwa ajili kuendeleza kongano la wafugaji Wilayani humo. Kulia wanaoshuhudia ni Ndugu Festo Maro Afsa Utafiti Mkuu wa COSTECH na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na Wanakongano wa Umoja wa Wafugaji wa Wilayani Nkasi (hawako pichani) katika Mkutano uliofanyika Kalambo Ranch  Wilayani humo tarehe 14 Novemba 2013. Mkuu huyo Mkoa aliwataka wafugaji kufuga kisasa bila kuathiri mazingira kwa kufuga mifugo michache inayoendana na maeneo husika, aliwataka pia wafugaji kuwaendeleza watoto wao kielimu tofauti na ilivyo hivi sasa amabao wengi wao hufanyishwa kazi za uchungaji wa mifugo. Katika hotuba yake fupi alitoa agizo kwa halmashauri zote Mkoani Rukwa kuweka kipaombele katika kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji na wakulima katika kila kijiji na kujiwekea mkakati wa idadi ya mifugo itakayofugwa kulingana na ukubwa wa eneo la malisho.
Ndugu Festo Maro Afsa Utafiti Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Nchini COSTECH akizungumza na wanakongano wa Umoja wa Wafugaji wa Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa jana tarehe 14 Novemba 2013. Katika maelezo yake alisema kuwa sio kila Kongano hupewa fedha za kianzio bali hushindanishwa na kwamba Kongano la Umoja wa Wafugaji wa Wilayani Nkasi likiwa na wanachama 167 limeibuka washindi kwa kuwa na mipango thabiti ya kuendeleza shughuli zao za ufugaji kisasa kwa kuwainua kiuchumi, kielimu, kiafya na kubwa zaidi bila kuathiri mazingira. Alisema Lengo la COSTECH kutoa misaada kama hiyo ni kuwawezesha wadau wafanye shughuli zao kisayansi zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aweze kuzungumza na Wanakongano wa Umoja wa Wafugaji wa Wilayani humo ambao yeye ndie muasisi wa umoja huo. Katika neno lake la awali alimtaarifu Mkuu huyo wa Mkoa kuwa Umoja huo ulianzishwa mwaka jana 2012 tarehe 29 Agosti na kusajiliwa rasmi tarehe 30 Agosti 2013 ukiwa na wanachama 167 na lengo kuu likiwa ufugaji bora wa kisasa usioathiri mazingira na utakaomnufaisha mfugaji.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akimkabidhi Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Wafugaji wa Wilayani Nkasi Ndugu Pancras Maliyatabu Cheti rasmi cha usajili wa umoja huo uliosajiliwa rasmi tarehe 30 Agosti 2013. Katikati anaeshuhudia ni Katibu wa umoja huo ndugu Jisena Biliya.
Picha ya pamoja.

No comments:

Post a Comment