Tuesday, November 19, 2013

WEZI WA MAFUTA KWENYE MALORI YA UJENZI WA BARABARA ZA LAMI WAFUMANIWA NA MSAFARA WA MKUU WA MKOA WA RUKWA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiwafokea wafanyakazi wawili wa kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering (Group) Corporation kutoka China baada ya kufumwa na msafara wake wakiiba mafuta ya Diesel kwenye tanki la lori la la kumwagilia maji (Boza) la kampuni hiyo tarehe 19 Novemba 2013 Katika kijiji cha Ntendo Manispaa ya Sumbawanga. Mkuu huyo wa Mkoa alikemea tabia hiyo ya wafanyakazi wezi na kusema umekua ni ugonjwa wa mda mrefu unaozorotesha kukamilika kwa ujenzi wa barabara za lami zinazoendelea kujengwa Mkoani Rukwa.
 
Wafanyakazi hao waliokamatwa ni dereva William Ebron (kulia pichani)
na kibarua Isaya Godwin  ambao walifumwa majira ya saa nne asubuhi wakinyonya mafuta kwenye tanki la Lori hilo lenye namba za usajili T-518 BDV mali ya kampuni hiyo kwa kutumia mpira wa kupitishia maji na kumuwekea mteja kwenye dumu la lita tano, hata hivyo mteja huyo alifanikiwa kukimbia. Baada ya kuhojiwa walidai kuwa mteja wao huyo angelipia lita hizo tano kwa Tsh. 3500/= bei ambayo kihalali haiwezi kununua japo lita mbili za mafuta hayo katika soko. 
 
 Msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ulikua ukielekea katika kata ya Mtowisa kwa ajili ya shughuli za kuhamasisha maendeleo ambapo ulikumbana na mkasa huo njiani katika Kijiji cha Ntendo. Barabara ya Sumbawanga - Namayere inajenga kwa kiwango cha lami na mkandarasi Jiangxi Geo-Engineering (Group) Corporation kutoka China chini ya Mhandisi Mshauri Nicholas O’Dwyer and Company Limited kutoka Ireland akishirikiana na Apex Engineering Ltd. kutoka Tanzania kwa gharama ya Sh. bilioni 78.8 ambazo ni fedha za ndani.
 
Watuhumiwa William Ebron (kulia) na kibarua Isaya Godwin (kushoto) muda mfupi baada ya fumanizi wakiwa hawana cha kujitetea.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiwakabidhi wezi hao kwa vyombo vya usalama ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Watuhumiwa wakiwa mikononi mwa Polisi.
Mashuhuda wa tukio hilo.
Baada ya kuanza ziara yake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akimuapisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Adam Misana (wapili kulia) na baadhi ya watendaji wa Kata ya Mtowisa na Kijiji cha Muze juu ya utekelezaji wa maazimio na makubaliano waliowekeana. Maazimio hayo ni pamoja na kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shuguli za maendeleo ya vijana, kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wakulima na wafugaji katika kila kijiji kuepusha migogoro ya wakulima na wafugaji, kuwekeana utaratibu maalum wa idadi ya mifugo inayotakiwa kufugwa kulingana na ukubwa wa maeneo husika, uhifadhi wa mazingira hususani ujenzi wa vyoo kuepukana na maradhi ya milipuko pamoja na maagizo mengine mbalimbali yaliyotolewa na Mkuu huyo wa Mkoa. 
Katika ziara yake hiyo alifanya mikutano minne ikiwepo miwili ya nje na miwili ya ndani ambapo maagizo mbalimbali kwa ngazi ya Wilaya, Halmashauri na vijiji yalitolewa kwa watendaji husika.

No comments:

Post a Comment