Friday, December 13, 2013

SHIRIKA LA MAENDELEO CIDA KUPITIA MRADI WA WAZAZI NA MWANA (THE MnW PROJECT) LAKABIDHI SIMU SITINI MKOANI RUKWA KURAHISISHA MAWASILIANO KATIKA VITUO VYA AFYA

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima akipokea boksi la simu kutoka kwa Bi Safia Telatela ambae ni Mratibu wa Mradi wa Wazazi na Mwana nchini (The WnM Project) kwa ajili ya kusaidia mawasiliano kwa vituo vya afya Mkoani Rukwa katika kupambana na vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga. Jumla ya simu sitini aina ya Nokia zimetolewa katika maeneo ya mradi huo Mkoani Rukwa ambayo ni Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Kalambo na Nkasi. Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Tawala Mkoa hu amelishukuru shirika la maendeleo CIDA kwa kufadhili mradi huo utakaosaidia kuokoa maisha ya mama wajawazito na watoto kwa kurahisisha mawasiliano na sehemu zenye huduma sahihi za afya.
Afisa Tawala wa Mradi huo wa Wazazi na Mwana (MnW) Bwana Mashauri Ndebile akionyesha moja ya simu hizo aina ya Nokia kwa waandishi wa habari waliohudhuria katika hafla hiyo ya makabidhiano. Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo CIDA na kutekelezwa na Miradi Mitatu ya Plan, Africare, Jhpiego kwa kushirikiana na MOHSW. Mradi huo unatekelezwa katika Mikoa miwili nchini ambayo ni Mwanza kwa Wilaya za Ilemela na Sengerema na Rukwa kwa Wilaya za Kalambo, Nkasi na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Vijijini.
Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima akizindua simu hizo kwa kupiga simu moja ya majaribio. 
Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima (kushoto) akimkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Ndugu Kimulika Galikunga Boksi moja lenye simu ishirini kwa ajili ya vituo vya afya katika halmashauri hiyo. 

Bi Safia Telatela ambae ni Mratibu wa Mradi wa Wazazi na Mwana nchini (The WnM Project) akizungumza katika hafla hiyo ambapo alisema lengo kubwa la mradi huo ni kuona vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga vinapungua na hatimae kuisha kabisa, alisema hilo litawezekana pale jamii, taasisi binafsi, mashirika ya maendeleo na Serikali zitakaposhirikiana katika kuleta ustawi katika eneo hilo.

Picha ya Pamoja

Thursday, December 12, 2013

KAMATI MAALUM YA BUNGE IKIONGOZWA NA MHE. JAMES DAUD LEMBELI MKOANI RUKWA KUTATHMINI NA KUFATILIA JUU YA MATOKEO YA OPERESHENI TOKOMEZA

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili na Kamati ndogo ya Bunge inayofuatilia na kutathmini juu ya Operesheni TOKOMEZA iliyositishwa hivi karibuni na Serikali Ndugu James Daudi Lembeli  ambae pia ni Mbune wa Kahama (kushoto)akizungumza katika kikao na uongozi wa Mkoa wa Rukwa Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa huo jana tarehe 11 Disemba 2013. Mkuu wa Mkoa huo Injinia Stella Manyanya yuko safarini kikazi na katika hicho aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Methew Sedoyyeka (kulia). Wa pili kulia ni Katibu Tawala Mkoa huo Alhaj Salum Mohammed Chima.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili na Kamati ndogo ya Bunge inayofuatilia na kutathmini juu ya Operesheni TOKOMEZA iliyositishwa hivi karibuni na Serikali Ndugu James Daudi Lembeli akizungumza na wananchi wa kijiji cha Msila kilichopo kata ya Mtowisa Wilayani Sumbawanga ambao kijiji chao kiliathirika na Operesheni hiyo. Jumla ya nyumba 88 zilichomwa moto na makambi 186 ya wavuvi katika ziwa Rukwa. Kati ya nyumba hizo zilizochomwa ni nyumba tano tu ndio zilikuwa nje ya mita 500 ya maeneo ya hifadhi. Kwa mujibu wa bwana Lembeli tume yake itakamilisha taarifa yake na itasomwa bungeni tarehe 17 au 18 mwezi huu wa Disemba ambapo watawasilisha kilichojiri katika Operesheni hiyo pamoja kulishauri bunge na Serikali namna bora zaidi ya kuendeleza zoezi hilo.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Msila walipata fursa ya kutoa kero zao na maoni mbalimbali kwa kamati hiyo juu ya operesheni TOKOMEZA. Wengi wao walilalamika kuchomewa nyumba zao na wengine kuonekana kutokuwa na uhakika juu ya umbali na maeneo ya hifadhi wanaotakiwa kuishi kisheria na kufanya shughuli zao.   
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga akibainisha baadhi ya mambo katika mkutano huo uliofanyika katika kijiji cha Msila Wilayani Sumbawanga. Mkuu huyo wa Wilaya ya Sumbawanga Methew Sedoyyeka aliiomba kamati hiyo ya bunge kufikisha taarifa bungeni juu ya hali ilivyo hivi sasa ya migogoro ya wakulima na wafugaji na kwamba Serikali ione namna ya kusaidia kutenga maeneo maalum ya wakulima na wafugaji pamoja na kuzitumia ranchi za taifa zilizopo kuwapa wafugaji wakubwa wazalendo waweze kuziendeleza kuliko hivi sasa ambapo wawekezaji wa nje na waliopo wameshindwa kuziendeleza ipasavyo.

TAARIFA KWA UMMA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

MKOA WA RUKWA

Telegraphic: “REGCOM”

Simu. No:0252802137/2802138/2802144

Fax No. (025) 2802217/2802318

E-mail:rasrukwa@yahoo.com


OFISI YA MKUU WA MKOA,
    
P. O. Box 128,
SUMBAWANGA.

TAARIFA KWA UMMA.
 
Serikali Mkoani Rukwa inapenda kukanusha taarifa iliyotolewa na gazeti la Jambo Leo toleo namba 1546 la tarehe 3, Disemba 2013 iliyoandikwa na Mwandishi Gurian Adolf katika ukurasa wa 10 iliyokuwa na kichwa cha habari "TCCIA Rukwa yaomba mbolea ya DAP".
 
Sehemu ya taarifa hiyo ilieleza kuwa; Nanukuu "Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Rukwa, Shadrack Malila ameiomba Serikali kuwashauri wakulima wa Mkoa huo kutumia mbolea nyingine ya kupandia mahindi badala ya mbolea ya minjingu ambayo haijafanyiwa utafiti katika Mkoa huo."
 
Kwa mujibu wa gazeti hilo taarifa hiyo aliitoa mbele ya waandishi wa habari Ofisini kwake mjini Sumbawanga ambapo aliongeza kuwa "Tangu awali wakulima hao walikataa mbolea hiyo, baada ya kuitumia kupandia na kushindwa kustawisha vizuri mazao yao ya mahindi, tofauti na mbolea ya DAP ambayo husaidia kupatikana kwa mazao mengi”. Mwisho wa kunukuu.

 
Serikali Mkoani Rukwa inapenda kukanusha kuwa sio kweli kwamba mbolea ya minjingu haijafanyiwa utafiti kufaa kutumika katika Mkoa huu na kwamba haijapokea malalamiko yeyote yaliyo rasmi kutoka kwa wananchi (wakulima) juu ya ubora na ufanisi wa mbolea hiyo. Matokeo yake yameonekana kuwa ni mazuri hususani baada ya mbolea hiyo kuboreshwa zaidi na sasa inaitwa "Minjingu Mazao".

 
Napenda ifahamike wazi kuwa tafiti mbalimbali za udongo zimefanyika Mkoani Rukwa mfano, taarifa ya BRALUP, 1977, Tafiti za udongo zilizofanywa na Kituo cha Utafiti cha Uyole na Sampuli mbalimbali zilizopelekwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kutoka Halmashauri ya wilaya ya Nkasi miaka ya 2008-2010 na kuonesha sehemu kubwa ya udongo wa maeneo ya Uwanda wa juu wa Ufipa (Ufipa Plateau) kuna upungufu mkubwa wa kirutubisho cha aina ya Naitrojeni kulingana na mahitaji yake kwa mimea jamii ya nafaka, hasa mahindi chotara.

 
Aidha, majaribio ya kutumia aina na viwango mbalimbali vya mbolea kwa zao la mahindi ikiwemo Minjingu yamefanywa kupitia Kituo Kidogo cha Utafiti cha Uyole kilichokuwa wataalam huko Nkundi na mashamba ya majaribio sehemu mbalimbali na kutoa matokeo yaliyofanyiwakazi. Kufuatia majaribio hayo, Mkoa wa Rukwa ulitoa mapendekezo kwa kampuni ya Minjingu Mines & Fertilizer ya kubadilishwa kwa umbile la mbolea ya Minjingu kutoka katika umbile la unga (powder form) na kuwa katika umbile la sasa la chengachenga ili kuwa rahisi wakati wa kuweka mbolea shambani. Pia Mkoa ulipendekeza mbolea hiyo iwekewe kirutubisho aina ya Nitrojeni ili kukidhi mahitaji ya udongo wa sehemu kubwa ya Ukanda wa juu wa Ufipa, mapendekezo ambayo yamezingatiwa zimefanywa na matokeo yake kuonekanika.

 
Mashamba Darasa yanayohusisha mbolea ya Minjingu Mazao yameanzishwa na kuendeshwa sehemu mbalimbali za Mkoa katika msimu uliopita wa 2012/2013 na kukaguliwa na Viongozi kuona ufanisi wake. Yapo mashamba yaliyofanya vizuri na yapo ambayo hayakufanya vizuri. Hali ya tofauti kama hiyo hutokea kwa aina zote za mbolea zinapotumika katika maeneo tofauti. Ikumbukwe kuwa ardhi ipo hai na hutofautiana kutoka sehemu moja na nyingine!

 
Tafiti nyingi zimeonesha kuwa wakulima wengi wameshindwa kupata matokeo mazuri katika kilimo kwa kushindwa kufuata masharti ya wataalam wa kilimo hata kama wakitumia mbolea ya aina yeyote. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Profesa Kauzeni na wenzake katika vijiji vya Ntendo na Mtimbwa mwaka 1998, pamoja na mambo mengine ilibainika kuwa wakulima wachache waliomudu kutumia mbolea au mbegu bora hawakuzingatia viwango vilivyopendekezwa na wataalam. Walitumia karibu nusu tu ya mapendekezo, Mfano Hekta moja iliyopandwa mahindi zilitakiwa kutumia kilo 125 za TSP Triple Super Phosphate ( P2O5) 18% na kilo 250 za UREA (N) 46%, ili kuvuna tani sita za mahindi sawa na kilo 6,000 au wastani wa magunia 60 kwa hekta. Waliofanya vizuri kidogo walitumia kilo 100 tu za TSP na kilo 100 za UREA.

 
Kufuatia taarifa hiyo, Uongozi wa Mkoa wa Rukwa haupendi kuingilia uhuru wa mtu wa kupata na kutoa habari kama Mtanzania mwingine yeyote. Ni vema mtu akatoa taarifa anazozifahamu vizuri/zilizofanyiwa utafiti, zisizoleta mtafaruku au kuipotosha jamii na zisizolenga kuvutia maslahi binafsi kwa namna yeyote ile.

 
Serikali ya Mkoa imesikitishwa na taarifa aliyoitoa Bwana Malila. Ni dhahiri kuwa ametumia vibaya nafasi yake ya uenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Rukwa kuwashawishi wakulima wa Mkoa huu kuwa mbolea ya Minjingu haifai na haitowapa mavuno mazuri. Ikumbukwe kuwa Bwana Malila ambae ni msambazaji wa pembejeo zenye ruzuku ya Serikali katika Manispaa ya Sumbawanga kwa mwaka huu 2013/14 pia ni mfanyabiashara wa pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea anayoipigia chapuo ya Diammonium Phosphate maarufu kama DAP.

 
Ifahamike pia kuwa Bwana Malila aliwahi kuwa na Mkataba na Kampuni ya Minjungu Mines& Fertilizer Ltd katika msimu wa kilimo wa mwaka 2009/2010. Kama kweli mbolea hiyo haifai mbona aliwahi kuwa wakala na akaisambaza kwa wakulima bila kutoa matamko kama haya? Ni dhahiri kuwa taarifa yake hiyo ina mgongano wa kimaslahi na hailengi katika kuboresha kilimo kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa.
 
Imetolewa na:
 
Albinus Mugonya,
Kaimu Katibu Tawala Mkoa,
RUKWA.
 
10 Disemba, 2013

Monday, December 9, 2013

KATIBU TAWALA MKOA WA RUKWA ALHAJ SALUM CHIMA AONGOZA MAHAFALI YA KWANZA YA ISTIQAAMA ENGLISH MEDIUM AND PRE-PRIMARY SCHOOL YA MJINI SUMBAWANGA

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima akizungumza katika mahafali ya kwanza ya shule ya Awali ya Istiqaama iliyopo Majumbasita katika Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa  Katika hotuba yake hiyo aliwaasa waislamu kuwaendeleza watoto wao kielimu katika taasisi za kidini zilizopo ili waweze kupata elimu zote za kitaaluma na kidini waweze kuwa na ujuzi na maadili mema. Aliwataka pia Waislamu kujenga tabia ya kuchangia taasisi zao ili ziweze kusonga mbele katika malengo waliojiwekea. Pichani kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Ndugu Adam Misana. 
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Istiqaama English Medium and Primary School ya Sumbawanga Amr Said akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza katika mahafali hayo. Katika risala iliyosomwa kwa Mgeni Rasmi ambaye ni Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima Shule hiyo ilianza rasmi Januari mwaka huu 2013 ikiwa na wanafunzi 48 na hidi hivi sasa ina wanafunzi 6. Shule hiyo inayoendeshwa na taasisi ya kidini ya ISTIQAAMA ina mpango wa kujenga shule ya msingi katika kipindi cha mwaka 2014-2017 na shule ya Sekondari katika kipindi cha mwaka 2018-2021.  
Zoezi la utoaji wa vyeti kwa wahitimu

Wahitimu wa kike
Wahitimu wakiumeni
Sehemu ya washiriki wa hafla hiyo, kushoto kwao waliketi wanawake.
Baadhi ya watoto wakiwa wanacheza katika moja ya sehemu za michezo katika shule hiyo. Pichani nyuma ni sehemu ya madarasa ya shule hiyo.

Friday, December 6, 2013

MKURUGENZI MKUU WA MFUKO WA AKIBA YA WAFANYAKAZI SERIKALINI "GEPF" AONANA NA KUUTAMBULISHA MFUKO HUO KWA VIONGOZI WA MKOA WA RUKWA

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini (GEPF) Bwana Daud Msangi akizungumza na viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Rukwa alipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo Injinia Stella Manyanya kwa lengo la kuutambulisha mfuko huo na faida zake. Mfuko huo una fursa mbili za kujiunga ambazo ni kwa njia ya lazima kama ilivyo kwa mifuko mingine ya hifadhi ya jamii kwa watumishi wa Serikali na njia nyingine ni ya hiari kwa wafanyakazi wote wakiwemo wa Serikali, Sekta binafsi na hata wale waliojiajiri wenyewe. Kwa wale wateja waliojiunga na mfuko huo kwa hiari wana uwezo wa kuchukua mafao yao kwa muda mfupi tofauti na ule mfumo wa lazima wa Serikali ambao ni lazima mteja afikie umri wa kustaafu.
Wajumbe wa kikao hiki walikuwa Wakuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nkasi na Kalambo. Wakuu wa Idara wote katika Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa, Wakurugenzi wa halmashauri za Manispaa ya Sumbawanga, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbwanga, Kalambo na Nkasi pamoja na baadhi ya wataalamu kutoka katika maeneo hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Moshi Chang'a (wa pili kulia) akichangia katika kikao hicho ambapo alisema Wilaya mpya ya Kalambo ina fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo sekta ya nyumba za ofisi na makazi ambayo ni fursa kwa mfuko huo wa GEPF kuwekeza kwa kujenga nyumba hizo katika Wilaya hiyo na Mkoa kwa ujumla. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta. Kulia kwa Mhe Chang'a ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Albinus Mugonya na Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu Ndugu Samson Mashalla.
Sehemu ya wajumbe katika kikao hicho.

RAIS KIKWETE AOMBOLEZA KIFO CHA MZEE MANDELA, ATANGAZA SIKU 3 ZA MAOMBOLEZO KITAIFA, BENDERA KUPEPEA NUSU MLINGOTI

Image: BRITAIN-SAFRICA-POLITICS-HEALTH-MANDELA-FILES
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
press@ikulu.go.tz             
Fax: 255-22-2113425
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za rambirambi Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini na kupitia kwake, kwa mkewe Bi. Graca Machel, wanafamilia wote na wananchi wote wa Afrika ya Kusini kufuatia kifo cha Mzee Nelson Mandela kilichotokea tarehe 5 Desemba, 2013 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
 
Rais ameuelezea msiba huu kuwa ni msiba mkubwa kwetu sote.
“Afrika ya Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla imepoteza mtu mashuhuri na shujaa mkubwa wa Karne ya 20 na 21.Tunaelewa machungu waliyonayo wananchi wa Afrika ya Kusini kwa kupoteza kiongozi shupavu, jasiri, mwana mapinduzi , mvumilivu na mstahimilivu”.
Ameongeza Rais Kikwete.
 
Rais amemuelezea Mzee Mandela kuwa ni kielelezo cha aina yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe, huruma na upendo uliomuwezesha kuwaunganisha wananchi wa Afrika ya Kusini kuwa taifa moja baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
 
“Mandela ni mfano bora kwa wanadamu wa jinsi binadamu muungwana anavyopaswa kuwa . Ni wajibu wa wana Afrika Kusini, Afrika na dunia kwa jumla kuiga mfano wake hasa moyo wake wa uzalendo, kujitolea hata maisha yake kwa ajili yake na wananchi wenzake” .Rais ameongeza kusema, “Tuzidi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Mzee Mandela mahali pema peponi”.
 
Kufuatia kifo hicho Rais ametangaza siku 3 za maombolezo kuanzia leo tarehe 6 hadi 8 Disemba, 2013.
 
Aidha, Mheshimiwa Rais ameagiza kuwa katika siku hizo 3 bendera zote zipepee nusu mlingoti.
 
Imetolewa na;
 
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu,
 
DAR AS SALAAM.
06 Desemba,2013

Thursday, December 5, 2013

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AMUAGA BALOZI MPYA NCHINI NIGERIA OLE NJOOLAY

001-1Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na kumkaribisha Balozi mpya nchini Nigeria, Daniel Ole Njoolay, wakati alipofika ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, jana mchana kwa ajili ya kumuaga akielekea kuanza kazi rasmi. Picha na OMR 002-1Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika mazungumzo na Balozi mpya nchini Nigeri, Daniel Ole Njolay, wakati alipofika ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, jana mchana kwa ajili ya kumuaga akielekea kuanza kazi rasmi. Picha na OMR

Tuesday, December 3, 2013

MADIWANI WA MANISPAA YA MUSOMA WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO MKOANI RUKWA, WATEMBELEA MAKUMBUSHO NDOGO YA MKOA YALIYOPO KATIKA JENGO LA OFISI YA MKUU WA MKOA HUO

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Ndugu Albinus Mugonya akiwakaribisha Madiwani 12 wa Manispaa  ya Musoma (kulia) waliongozana na baadhi ya watumishi sita kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya. Msafara huo umefika Mkoani Rukwa kwa ziara ya kujifunza mambo mbalimbali ya kiuongozi kutoka kwa madiwani wenzao wa Manispaa ya Sumbawanga na Serikali ya Mkoa kwa ujumla.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Sabas Katepa akiwatambulisha madiwani mbalimbali kutoka Manispaa ya Musoma Mkoani Mara walipofika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa ajili ya utambulisho katika ziara yao ya mafunzo Mkoani Rukwa. 
Madiwani hao walipata fursa ya kutembelea ukumbi wa kurushia mawasiliano ya moja kwa moja (Video Conference) ambayo yanauwezo wa kuziunganisha ofisi mbalimbali za Serikali katika kikao kimoja. Pichani Mchambuzi wa mifumo ya Kompyuta Galus Ouma akitoa maelezo mafupi na namna mtandao huo unavyofanya kazi.
Madiwani hao walitembelea pia makumbusho ndogo ya Mkoa iliyopo katika jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa. Makumbusho hii imesimama kwa nguvu kubwa iliyowekwa na Mkuu wa Mkoa wa huo Injinia Stella Manyanya ambapo taarifa mbalimbali za kimkoa na taifa zinapatikana.
Baadhi ya tuzo mbalimbali ambazo Mkoa wa Rukwa umewahi kuzipata pia zinapatikana katika makumbusho hii.
Baadhi ya zana za asili ya jamii ya watu wa Rukwa zinapatikana katika makumbusho hii. 
Picha za Wakuu wa Mikoa waliowahi kuungoza Mkoa wa Rukwa tangu ulipoanzishwa mwaka 1974 zinapatikana katika makumbushi hii.
Picha ya Pamoja.

Monday, December 2, 2013

MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI MKOANI RUKWA, TAASISI MBALIMBALI ZA SERIKALI NA BINAFSI ZAPONGEZWA KWA KUWA MSTARI WA MBELE KATIKA VITA DHIDI YA UKIMWI

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Methew Sedoyyeka akihutubia wananchi katika viwanja vya shule ya msingi Kizwite katika Manispaa ya Sumbawanga katika kuadhimisha siku ya Ukimwi duniani iliyofanyika kimkoa katika Manispaa ya Sumbawanga. Akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya aliitaka jamii kukemea tabia hatarishi zinazopelekea ushawishi wa maambukizo wa virusi vya ukimwi ukiwemo ulevi uliokithiri, ngono zembe, ndoa za utotoni na mavazi yasiyeandana na maadili ya kitanzania.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Methew Sedoyyeka (kushoto) akimkabidhi kikombe kilichokua wa na ujembe maalum wa UKIMWI ("AMKA SASA" Pima VVU, Furahia Maisha) Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Albinus Mugonya kama pongezi kwa Ofisi hiyo kwa kuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya Ukimwi nchini. Zawadi mbalimbali zenye thamani ya Tsh. Milioni 6.4 zilitolewa kwa taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi kwa mchango wao mkubwa wa mapambano dhidi ya Ukimwi.
Sehemu ya wananchi waliohudhuria katika maadhimisho hayo.
Burudani na Muziki ilikuwa sehemu ya kunogeza maadhimisho hayo.