Thursday, December 12, 2013

TAARIFA KWA UMMA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

MKOA WA RUKWA

Telegraphic: “REGCOM”

Simu. No:0252802137/2802138/2802144

Fax No. (025) 2802217/2802318

E-mail:rasrukwa@yahoo.com


OFISI YA MKUU WA MKOA,
    
P. O. Box 128,
SUMBAWANGA.

TAARIFA KWA UMMA.
 
Serikali Mkoani Rukwa inapenda kukanusha taarifa iliyotolewa na gazeti la Jambo Leo toleo namba 1546 la tarehe 3, Disemba 2013 iliyoandikwa na Mwandishi Gurian Adolf katika ukurasa wa 10 iliyokuwa na kichwa cha habari "TCCIA Rukwa yaomba mbolea ya DAP".
 
Sehemu ya taarifa hiyo ilieleza kuwa; Nanukuu "Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Rukwa, Shadrack Malila ameiomba Serikali kuwashauri wakulima wa Mkoa huo kutumia mbolea nyingine ya kupandia mahindi badala ya mbolea ya minjingu ambayo haijafanyiwa utafiti katika Mkoa huo."
 
Kwa mujibu wa gazeti hilo taarifa hiyo aliitoa mbele ya waandishi wa habari Ofisini kwake mjini Sumbawanga ambapo aliongeza kuwa "Tangu awali wakulima hao walikataa mbolea hiyo, baada ya kuitumia kupandia na kushindwa kustawisha vizuri mazao yao ya mahindi, tofauti na mbolea ya DAP ambayo husaidia kupatikana kwa mazao mengi”. Mwisho wa kunukuu.

 
Serikali Mkoani Rukwa inapenda kukanusha kuwa sio kweli kwamba mbolea ya minjingu haijafanyiwa utafiti kufaa kutumika katika Mkoa huu na kwamba haijapokea malalamiko yeyote yaliyo rasmi kutoka kwa wananchi (wakulima) juu ya ubora na ufanisi wa mbolea hiyo. Matokeo yake yameonekana kuwa ni mazuri hususani baada ya mbolea hiyo kuboreshwa zaidi na sasa inaitwa "Minjingu Mazao".

 
Napenda ifahamike wazi kuwa tafiti mbalimbali za udongo zimefanyika Mkoani Rukwa mfano, taarifa ya BRALUP, 1977, Tafiti za udongo zilizofanywa na Kituo cha Utafiti cha Uyole na Sampuli mbalimbali zilizopelekwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kutoka Halmashauri ya wilaya ya Nkasi miaka ya 2008-2010 na kuonesha sehemu kubwa ya udongo wa maeneo ya Uwanda wa juu wa Ufipa (Ufipa Plateau) kuna upungufu mkubwa wa kirutubisho cha aina ya Naitrojeni kulingana na mahitaji yake kwa mimea jamii ya nafaka, hasa mahindi chotara.

 
Aidha, majaribio ya kutumia aina na viwango mbalimbali vya mbolea kwa zao la mahindi ikiwemo Minjingu yamefanywa kupitia Kituo Kidogo cha Utafiti cha Uyole kilichokuwa wataalam huko Nkundi na mashamba ya majaribio sehemu mbalimbali na kutoa matokeo yaliyofanyiwakazi. Kufuatia majaribio hayo, Mkoa wa Rukwa ulitoa mapendekezo kwa kampuni ya Minjingu Mines & Fertilizer ya kubadilishwa kwa umbile la mbolea ya Minjingu kutoka katika umbile la unga (powder form) na kuwa katika umbile la sasa la chengachenga ili kuwa rahisi wakati wa kuweka mbolea shambani. Pia Mkoa ulipendekeza mbolea hiyo iwekewe kirutubisho aina ya Nitrojeni ili kukidhi mahitaji ya udongo wa sehemu kubwa ya Ukanda wa juu wa Ufipa, mapendekezo ambayo yamezingatiwa zimefanywa na matokeo yake kuonekanika.

 
Mashamba Darasa yanayohusisha mbolea ya Minjingu Mazao yameanzishwa na kuendeshwa sehemu mbalimbali za Mkoa katika msimu uliopita wa 2012/2013 na kukaguliwa na Viongozi kuona ufanisi wake. Yapo mashamba yaliyofanya vizuri na yapo ambayo hayakufanya vizuri. Hali ya tofauti kama hiyo hutokea kwa aina zote za mbolea zinapotumika katika maeneo tofauti. Ikumbukwe kuwa ardhi ipo hai na hutofautiana kutoka sehemu moja na nyingine!

 
Tafiti nyingi zimeonesha kuwa wakulima wengi wameshindwa kupata matokeo mazuri katika kilimo kwa kushindwa kufuata masharti ya wataalam wa kilimo hata kama wakitumia mbolea ya aina yeyote. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Profesa Kauzeni na wenzake katika vijiji vya Ntendo na Mtimbwa mwaka 1998, pamoja na mambo mengine ilibainika kuwa wakulima wachache waliomudu kutumia mbolea au mbegu bora hawakuzingatia viwango vilivyopendekezwa na wataalam. Walitumia karibu nusu tu ya mapendekezo, Mfano Hekta moja iliyopandwa mahindi zilitakiwa kutumia kilo 125 za TSP Triple Super Phosphate ( P2O5) 18% na kilo 250 za UREA (N) 46%, ili kuvuna tani sita za mahindi sawa na kilo 6,000 au wastani wa magunia 60 kwa hekta. Waliofanya vizuri kidogo walitumia kilo 100 tu za TSP na kilo 100 za UREA.

 
Kufuatia taarifa hiyo, Uongozi wa Mkoa wa Rukwa haupendi kuingilia uhuru wa mtu wa kupata na kutoa habari kama Mtanzania mwingine yeyote. Ni vema mtu akatoa taarifa anazozifahamu vizuri/zilizofanyiwa utafiti, zisizoleta mtafaruku au kuipotosha jamii na zisizolenga kuvutia maslahi binafsi kwa namna yeyote ile.

 
Serikali ya Mkoa imesikitishwa na taarifa aliyoitoa Bwana Malila. Ni dhahiri kuwa ametumia vibaya nafasi yake ya uenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Rukwa kuwashawishi wakulima wa Mkoa huu kuwa mbolea ya Minjingu haifai na haitowapa mavuno mazuri. Ikumbukwe kuwa Bwana Malila ambae ni msambazaji wa pembejeo zenye ruzuku ya Serikali katika Manispaa ya Sumbawanga kwa mwaka huu 2013/14 pia ni mfanyabiashara wa pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea anayoipigia chapuo ya Diammonium Phosphate maarufu kama DAP.

 
Ifahamike pia kuwa Bwana Malila aliwahi kuwa na Mkataba na Kampuni ya Minjungu Mines& Fertilizer Ltd katika msimu wa kilimo wa mwaka 2009/2010. Kama kweli mbolea hiyo haifai mbona aliwahi kuwa wakala na akaisambaza kwa wakulima bila kutoa matamko kama haya? Ni dhahiri kuwa taarifa yake hiyo ina mgongano wa kimaslahi na hailengi katika kuboresha kilimo kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa.
 
Imetolewa na:
 
Albinus Mugonya,
Kaimu Katibu Tawala Mkoa,
RUKWA.
 
10 Disemba, 2013

No comments:

Post a Comment