Friday, January 17, 2014

MKUU WA MKOA WA RUKWA AONANA NA TIMU MAALUUM YA KUHAKIKI MAENEO MAPYA YA UTAWALA KUTOKA TAMISEMI, AISHAURI MAMLAKA HUSIKA KUANGALIA UPYA VIGEZO VINAVYOTUMIKA KUGAWA MAENEO MAPYA YA UTAWALA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na timu maalum inayohakiki maeneo mapya ya utawala kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Pichani kulia na timu yake ya Mkoa iliyokuwa ikiratibu maeneo hayo ofisini kwake leo tarehe 17 Januari 2014. Timu hiyo kutoka TAMISEMI inaongozwa na Mwanasheria wa TAMISEMI Ndugu Eustard Ngatale (watatu kulia).

 Katika kikao hicho kifupi Mkuu huyo wa Mkoa ameiomba mamlaka husika kupitia timu hiyo kuangalia upya vigezo vinavyotumika katika kugawa maeneo mapya ya utawala na upandishaji wa madaraja kutoka kijiji, kata, Tarafa, Halmashauri, Miji na Manispaa. 

Alisema kuwa kuna maeneo mengine ambayo yakiangaliwa kwa kigezo kimoja cha wingi wa watu bila kuangalia umbali wa huduma na giografia ya eneo husika unakuta wananchi wanakosa huduma zao za msingi na kupata tabu kubwa katika kuzipata.

 Alitolea mfano vijiji vikubwa vya mwambao ambavyo kupata huduma katika kata zao ni lazma wavuke upande mmoja wa Ziwa kwenda upande mwingine jambo ambalo ni hatarishi kama ilivyotokea kwa wananchi wa Kijiji cha Kipwa Mwambao mwa Ziwa Tanganyika ambao hivi karibuni walipoteza watu 15 katika ajali ya boti walipokwenda kupata huduma ya afya. Wengi ya waliofariki katika ajali hiyo mbaya walikuwa ni watoto chini ya umri wa miaka 5.  
Kikao kikiwa kinaendelea ambapo kwa upande wake Mwanasheria wa TAMISEMI Ndugu Eustard Ngatale alisema kuwa kubariki na kuhalalisha uanzishwaji wa maeneo mapya ya Utawala vipo vitu mbalimbali vya kuzingatia ambavyo ni pamoja na kuwepo kwa makubaliano ya wananchi na viongozi wa maeneo husika kupitia mihutasari ya vikao maalumu vya kisheria vya WDC, Halmashauri, DCC na RCC katika ngazi ya Mkoa.

No comments:

Post a Comment