Saturday, January 25, 2014

SITASITA KUWAONDOA WATUMISHI / WAKUU WA IDARA WANAOWACHONGANISHA MADIWANI NA MKURUGENZI WAO - ASEMA INJINIA MANYANYA MKUU WA MKOA WA RUKWA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kilichofanyika jana tarehe 25 Januari 2014 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo uliopo Sumbawanga Mjini. 
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Methew Sedoyyeka akizungumza katika kikao hicho ambapo alitilia mkazo juu kuboresha elimu na ufaulu katika halmashauri hiyo ambayo haijafanya vizuri katika siku za karibuni. Alisisitiza pia umuhimu wa upandaji miti hususani katika msimu huu wa masika.
Mbunge wa Jimbo la Kwela (CCM) Ignas Malocha akishukuru ujio wa Mkuu huyo wa Mkoa katika kikao hicho na maelekezo aliyoyatoa ambayo alisema ni muongozo mzuri na wa kuzingatiwa katika maendeleo ya halmshauri hiyo.
Mkuu huyo wa Mkoa akizungumza na wajumbe wa kikao hicho kushoto wakiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na kulia wakiwa ni wakuu wa idara katika halmashauri hiyo.
Madiwani wa halmashauiri ya wailaya ya Sumbwanga.
Wakuu wa Idara Halmashauri ya Wilaya ya Sumbwanga.
Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya, Madiwani na Viongozi wa Chama tawala (CCM) walioalikwa katika kikao hicho.

........................................................

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya amewaonya watumishi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga wakiwemo wakuu wa idara wenye tabia ya kuwachonganisha madiwani na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndugu Adam Misana, "watumishi mnaofanya mchezo huo nitawaondoeni" Alisema Manyanya. 

Manyanya aliyasema hayo jana katika kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga alipotembelea kutoa salam zake za mwaka mpya kwenye baraza hilo. Alisema kuwa tangu Mkurugenzi huyo ateuliwe kuiongoza Halmashauri hiyo amekuwa akifanya vizuri katika udhibiti wa mapato jambo ambalo limekuwa kero kubwa wakuu wa idara na watumishi wa ofisi hiyo.

Alieleza kuwa Mkurugenzi aliyekuwepo kabla ya Misana alikua akikaimisha ofisi mara kwa mara kwa watu tofauti jambo ambalo lilizorotesha utendaji na kupelekea mambo kufanyika kienyeji na kwa mazoea bila kujali matumizi sahihi ya mapato ya Halmashauri. Ujio wa Mkurugenzi huyu mpya umerekebisha hali hiyo kwa kiwango kikubwa hususani katika matumizi ya fedha za halmashauri, aliongeza Mkuu huyo wa Mkoa.

Katika salam zake alilieleza baraza hilo kuwa mpaka sasa toka ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ameshatembelea kata 51 sawa na asilimia 80% ya kata zote Mkoani Rukwa. Alisema baadhi ya kata hizo ameshazitembelea zaidi ya mara tano kutokana na umuhimu na matukio yaliyojitokeza.

Aliwata madiwani, viongozi wa chama na halmashauri pamoja watumishi kwa ujumla kutoa uongozi uliotukuka katika maeneo yao kwa kushirikiana katika kutoa huduma bora kwa wanachi na kuwafikia mara kwa mara pale inapowezekana na kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Katika hali nyingine Mkuu huyo wa Mkoa alishangazwa kwa Wilaya ya Sumbwanga kutokuwa na Hospitali yake ya Wilaya na badala yake kutegemea huduma katika Hospitali  Kuu ya Mkoa. Alisema mwaka huu 2014 ni mwaka wa afya na kwamba Halmashauri za Wilaya ya Sumbwanga zijipange kuhakikisha zinakuwa na hospitali yao ya Wilaya ili kuweza  kutoa nafasi kwa hospitali kuu ya Mkoa kuhudumia wagonjwa wa rufaa kuliko ilivyo hivi sasa ambapo ambapo inabebeshwa mzigo mkubwa na Wilaya hiyo.

Katika salam zake Injinia Manyanya aliwashauri madiwani na viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kujipanga kuhakikisha wanahamia katika Mji mdogo wa Laela uliopo takribani kilomita 100 kutoka mjini Sumbawanga. Alisema zipo faida kubwa za kufanya hivyo ikiwemo ya halmasahuri kuwa na mji wake watakaouendeleza kisasa na kujiwekea mikakati mbalimbali ya kimaendeleo. Aliongeza pia kuwa itakuwa fursa ya kuwasogezea wananchi huduma.

 Akielezea kuhusu jengo kubwa la kisasa la Halmashauri hiyo linaloendelea kujengwa mjini Sumabwanga alisema linaweza kutumika kama kitega uchumi cha Halmashauri ambapo litawapatia fedha nyingi za kujiendesha na kwamba wataomba fedha nyingine TAMISEMI ya kujenga ofisi kubwa kama hiyo Laela kwa lengo la kuwasogezea wananchi huduma.

Akizungumzia kilimo na ufugaji aliwataka viongozi wa halmashauri wakishirikiana na madiwani kuhakikisha wanajiwekea utaratibu maalumu wa maeneo ya wakulima na wafugaji na kuhakikisha kunakuwepo na idadi maalum ya mifugo inayotakiwa kufugwa katika maeneo yaliyotengwa na kuwekewa alama maalum za utambuzi.

Kwa upande wa ONYARU - Ondoa Nyasi Rukwa alisema kuwa mpango huu umekuwa na mafanikio makubwa kwani maeneo mengi wananchi wamehamasika kwa kuondoa nyasi na kuezeka kwa bati nyumba zao. Aliwataka viongozi na wasimamizi wa halmashauri kuendelea na uhamasihaji huo kuhakikisha nyumba za nyasi zinauhama Mkoa wa Rukwa.  

No comments:

Post a Comment