Monday, February 17, 2014

KATIBU MKUU WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII AKEMEA DAWA ZA KULEVYA, ASEMA WATANZANIA ZAIDI YA 500 WASHIKILIWA NCHI ZA NJE,WENGINE 100 WASUBIRI KUNYONGWA NCHINI CHINA

Katibu Mkuu Anna Maembe akisalimiana na akina mama wanakikundi cha kutunza Mazingira katika kata ya Matai wilayani Kalambo Mkoani Rukwa jana. PICHA ZOTE NA RAMADHANI JUMA.......................................................................
KATIBU Mkuu wa wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na watoto Anna Maembe amewataka vijana nchini kuachana kabisa na biashara ya dawa za kulevya kwani inawasababishia matatizo makubwa katika maisha yao badala yake wajiunge na kutengeneza vikundi vya kijasiriamali ili serikali iweze kuwasaidia kujikwamua kimaisha na kufikia ndoto zao.
Amesema takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa, zaidi ya vijana 500 wa Kitanzania wako kizuizini katika nchini tofauti duniani walikokamatwa wakisafirisha dawa hizo, huku vijana wengine wapatao 100 wakiwa wamehukumiwa kunyongwa nchini China.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na makundi mbalimbali ya kijamii wakati wa ziara yake katika kata ya Matai wilayani Kalambo Mkoa wa Rukwa jana, ambapo alisema biashara hiyo inachafua sana jina la Tanzania katika Jumuia ya Kimataifa kutokana na idadi kubwa ya vijana kujihusisha na biashara hiyo.
Akizungumzia sera ya Jinsia inayotekelezwa na wizara yake, Katibu Mkuu huyo alisema haina lengo la kuwafanya wanawake kuwatunishia misuli wanaume katika familia bali ni kuwawezesha wanawake kushiriki katika uzalisha na kukuza kipato cha familia na taifa  kwa ujumla ili kukabiliana na gharama za maisha ambazo zimepanda sana kwa sasa.
Vilevile alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanatenga muda wa kukaa na kuzungumza na watoto ili kujua changamoto zinazowakabili ikiwemo unyanyasaji wa kijinsi na kisaikolojia wanazokumbana nazo na pia kuwapatia haki zao za kimsingi kama elimu, afya na kusikilizwa kama  ambavyo sera ya watoto hapa nchini inavyoelekeza.
Katika kuimarisha vikundi vya wanawake mkoani Rukwa, katibu mkuu Maembe ametoa shilingi milioni 43 kutoka katika wizara yake, ambapo vikundi kutoka katika Halmashauri za wilaya ya Nkasi, Kalambo, Sumbawanga Vijijini na Manispaa vitanufaika kwa mtindo wa wanachama wa vikundi hivyo kupatiwa mikopo kwa ajili ya kutekeleza shughuli zao za kiuchumi.
NA RAMADHANI JUMA,
AFISA HABARI OFISI YA MKURUGENZI-KALAMBO

No comments:

Post a Comment