Tuesday, March 11, 2014

HABARI KUTOKA OFISI YA MKUU WA MKOA RUVUMA - WAZAZI MKOANI HUMO WATAKIWA KUWAPELEKA SHULE WATOTO VIZIWI

 Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu akiongea wakati alipofungua mkutano  mkuu wa mwaka wa chama cha viziwi mkoa wa Ruvuma (CHAVITA) leo katika ukumbi wa Maktaba ya mkoa.Kushoto ni mwalimu Rehema Nyagawa ambaye ni mkalimani wa kujitolea.
 Grevas Komba na Bahati Nyoni ambaye ni Katibu wa Viziwi mkoa wa Ruvuma wakisoma risala ya viziwi kwa mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu akiwa katika picha ya pamoja na wananchama wa Chama cha Viziwi Mkoa wa Ruvuma mara baada ya kufungua mkutano wa mwaka wa chama hicho hivi leo mjini Songea. Picha na habari  na  Revocatus Kassimba.

...........................................................................................................
Habari na Picha: Revocatus A.Kassimba
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa

Ruvuma
................................................................................

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu amewataka wazazi wenye watoto walemavu wa kusikia (Viziwi) kutowaficha ndani badala yake watoe taarifa kwa viongozi wa serikali za vijiji na mitaa ili wasaidiwe kupatiwa huduma muhimu ya elimu.

Ametoa wito huo leo wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha Viziwi mkoa (CHAVITA) ambapo  amewahakikishia kuwa serikali inathamini na kuwatambua viziwi kuwa ni kundi maalum katika jamii linalohitaji elimu maalum.

Ameongeza kusema kuwa huduma zote anazohitaji binadamu pia zinahitajiwa na watu wenye ulemavu wa kusikia na kusema kwani hayakuwa matashi yao kutaka ulemavu huo.

“Ulemavu wa kutokusikia au kutokuzungumza si laana kwani tatizo hili linaweza kumpata mtu yeyote yule” alisema Mwambungu
Amewasihi wazazi na walezi wote mkoani Ruvuma kuwapeleka shule watoto viziwi kwani elimu husika kwa  wasiosikia au kuzungumza ipo na inatolewa bure katika shule maalum za umma.

Ameitaja shule maalum kwa viziwi ya Ruhuwiko iliyopo Songea Manispaa kama mfano wa shule zinazotoa elimu wa watoto wasioosikia na kuzungumza hivyo ni vema sasa wananchi wakawapeleka watoto kupata ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kujikimu na maisha.

Mwambungu ameziagiza halmashauri zote mkoani Ruvuma kuhakikisha zinatoa kipaumbele  kwa walimu wenye taaluma za kufundisha watu wenye ulemavu ili kusaidia kufundisha katika shule zenye watoto viziwi  au wasioona ili walemavu hawa wapate mawasiliano stahiki.

Katika kusaidia jitihada za CHAVITA kujitangaza na kuunda umoja wao Mkuu wa Mkoa Mwambungu amewachangia shilingi laki nne (400,000/=) ili kutunisha mfuko wa viziwi mkoa wa Ruvuma na kuwasihi watu wenye mapenzi mema kuwasaidia walemavu wa aina zote.

Katika risala ya CHAVITA kwa mgeni rasmi iliyosomwa na Grevas Komba wameomba suala la elimu lipewe kipaumbele kwa viziwi kwani hakuna vituo vya kutosha kwa mafunzo kwa viziwi.

Pia wameomba serikali kudhamini walimu watakaosaidia kutatua tatizo la wasiosikia ili wapate wakalimani wenye ujuzi na utaalam wa mawasiliano.

Mkoa wa Ruvuma kwa mujibu wa takwimu za CHAVITA unao viziwi 256 waliotambulika kwa wilaya zote tano ambapo wengine hawajahesabiwa kutokana na kufichwa na wazazi na walezi wao.

No comments:

Post a Comment