Sunday, March 16, 2014

WAZIRI WA AFYA DKT. SEIF RASHID AMUWAKILISHA WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA KATIKA SIKU YA UTEPE MWEUPE TANZANIA MKOANI RUKWA

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid akiwa katika zoezi la ukaguzi wa mabanda mbalimbali yaliyoandaliwa kwa ajili ya kutoa elimu na huduma za mama wajawazito na watoto wachanga katika maadhimisho ya siku ya Utepe Mweupe Tanzania yaliyofanyika kitaifa Mkoani Rukwa katika Tarafa ya Mtowisa. Dkt. Seif Rashid alimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Mizengo Kayanza Peter Pinda ambae awali alikubali kushiriki maadhimisho hayo ambapo amekabiliwa na majukumu mengine ya kitaifa. Kushoto kwa Dkt. Seif Rashid ni Mratibu wa Taifa wa Utepe mweupe Mama Rose Mlay. Kauli Mbiu ya maadhimisho hayo ikiwa ni "WAJIBIKA MAMA AISHI"
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid akihutubia katika maadhimisho hayo ambapo aliwapongeza wadau wote wanaopigania na kusaidia afya ya mama na watoto na kuahidi kutoa kipaombele katika bajeti kwa ajili ya kusaidia kuokoa maisha ya mama wajawazito na watoto nchini. Aidha amezitaka Halmashauri nchini kutoa kipaombele kwa kuongeza bajeti zao katika kuhudumia afya ya mama wajawazito na watoto wachanga.
Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Ndugu Smythies Pangisa akitoa salamu za Mkoa wa Rukwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Injinia Stella Manyanya katika Maadhimisho hayo ya kitaifa. Katika Salamu hizo alisema zipo changamoto nyingi  katika sekta ya afya zinazohitaji ufumbuzi wa haraka ikiwemo upungufu wa watoa huduma, vifaa tiba, dawa, magari ya kubebea wagonjwa, vituo vya kutolea huduma za afya na vingine kuwa mbali na maeneo ya wananchi kwa baadhi ya maeneo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Rukwa Daktari John Gurisha akifafanua baadhi ya mambo katika sekta ya afya Mkoani Rukwa.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta akikabidhi kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid maoni na maombi ya wakazi wa Wilaya yake katika kuimarisha sekta ya afya katika Wilaya yao na Taifa kwa ujumla.
Maadhimisho hayo yalitawaliwa na hali ya hewa ya mvua ambayo hata hivyo haikuathiri mwenendo mzima wa ratiba iliyopangwa, baadhi ya wananchi walilazimika kutumia miamvuli na wengine kuonyesha uzalendo mkubwa na kuamua kunyeshewa hadi kukamilisha maadhimisho hayo, hata hivyo mvua hiyo ilikatika karibu na kufikia mwishoni mwa maadhimisho hayo.
Bi Adrianne Strong ambae nae ni mdau wa afya ya mama wajawazito na watoto wachanga akitoa salam zake na kujitambulisha. Hivi karibuni Bi Adriane Stong kwa kushirikiana na waumini wenzake wa Kanisa la University United Methodist Church la Washington DC Marekani walitoa msaada wa boti na life jacket kwa ajili ya kusaidia huduma za afya ya mama wajawazito na wagonjwa mwambao wa Ziwa Rukwa.
Balozi wa Utepe Mweupe Tanzania ambae pia ni mwanamuziki Sara Thomas akijumuika na wanawake wengine kuimba wimbo wa kuihimiza Serikali na wananchi kutimiza wajibu wao katika kuhakikisha wanaokoa maisha ya mama wajawazito na watoto wachanga.
Zoezi la uchangiaji wa damu salama lilikua likifanyika katika kila Wilaya za Mkoa wa Rukwa katika wiki ya maadhimisho hayo ya utepe mweupe ambapo chupa za damu zaidi ya alfu moja zilichangiwa na wananchi wa Mkoa wa Rukwa.

No comments:

Post a Comment